MCHANGO WA MWANAMKE KATIKA HUDUMA.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 18, 2017
- 3 min read

Bible Group Reading Together
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi..
Leo nataka nikutazamishe tofauti na vile ulivyozoea au tofauti na vile watu walivyozoea kuwatazama wanawake maana wapo watu wanao watazama wanawake kama watu wadhaifu,au kama watu fulani hivi wasioweza kitu,au kama watu wasio na huduma ! Mtazamo huo sio sahihi na ni mtazamo wa kishetani,Mungu hatazami hivyo,bali Mungu anafanya kazi sana na wanawake tofauti na mitazamo hiyo.
Ukitaka kuakikisha kwamba mwanamke ana nafasi kubwa katika huduma,nenda kaangalie huduma yoyote ile iliyofanikiwa kama hutakosa kuona wanawake waliojitambua ndio wamekuwa chachu ya kufanikiwa kwa huduma hiyo. Au nenda kaangalie kanisa la Bwana lililofanikiwa kama hutaona wanawake walivyohusika katika mafanikio hayo.
Mimi ninaekuandikia ujumbe huu sio mwanamke,lakini baada ya kujifunza kwa ukaribu juu ya huduma tuzifanyazo kila siku,nilimuona mwanamke ndiye mwenye nguvu ya kusimamisha huduma na pia ndiye mwenye nguvu ya kuangusha huduma ikiwa kama atajisahau au kutokujua wajibu wake.
“Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.” Mwanzo 3:20
Neno linatuambia “ Hawa,yeye ndiye mama yao wote walio hai” hii ikiwa na maana kwamba mwanamke amepewa neema ya kubeba kile kilichoanzishwa na Mungu. Mfano uhai wa mtoto awapo tumboni umetoka kwa Mungu,lakini ni mwanamke tu ndiye amepewa dhamana ya kuushikilia. Katika miezi tisa tumboni,mwanamke ushikilia mtoto na uhai wake.
Tunaona baadae mtoto akizaliwa bado anamuhitaji sana mama kuliko hata baba,kwa maana hata kama baba hayupo mtoto ataendelea vizuri;lakini ikiwa mama asipokuwepo mtoto atapitia kwenye shida sana. Na ndio maana hata katika wokovu,kanisa linafananishwa na“ mwanamke ” kama bibi harusi hii ikiwa na maana kwamba kanisa la Bwana ni mwili wa Kristo kilichobeba uhai wa kiroho. ( Waefeso 5:22-23)
Kama ilivyo kwa mwanamke kubeba mimba,kuzaa na kuendelea na majukumu makubwa ya kelea ndivyo ilivyo hata kwenye kanisa,ni wanawake ndio wenye kuiatamia mimba ya huduma au kanisa kwa njia ya maombi na kujitoa kwao hata inafikia wakati kanisa linazaa maono yake,lakini bado ni wanawake hao hao ndio utakaowaona wakiangaika huku na kule kuyalea maono hayo. Utaniambia kivipi?
Ni hivi; kila kanisa au huduma ya Mungu ina malengo,na maono yake. Hayo yote huwa kama mimba kwa sababu bado hayajazaliwa/hayajafikiwa,hivyo ni wanawake wengi kiidadi kuliko wanaume ndio utakaowaona wakiwa kwenye maombi kuombea malengo na maono hayo. Tena hata ukiamua kuangalia idadi tu ya wanawake katika kila idara yapo kanisani kwenu,utagundua wengi ni wanawake tena hata wale wanaojitoa kwa shughuli mbalimbali ni wanawake bado. Na ndio maana nakuambia hao,wana nafasi kubwa sana katika huduma ya Bwana Yesu.
Kuna mambo ambayo mwanamme hawezi kuyafanya ipasavyo kwenye huduma isipokuwa mwanamke tu. Kwa mfano,mwanaume mtumishi hawezi kuwafundisha ipasavyo wanawake mabinti kwenye mambo ya kike isipokuwa mwanamke mwenyewe ndiye atakayeweza kuwafundisha kwa undani mabinti hao. Na ni mambo muhimu sana kwa kanisa,sababu mabinti wasipofundishwa na kanisa basi ujue duniani itawafundisha,nao watapotea !!
Mwanamke anaweza kuibadilisha familia na kuanza kumcha Mungu kama kanisa la nyumbani. Na ndiye kisababishi cha kumgeuza mumewe amuelekee Mungu. Mimi nataka nikuambie leo,kwamba hata kama mwanamke fulani aliyeokoka vizuri,kisha akawa na mume ambaye hataki kuokoka,mwanamke akizidi kukaza kwa Bwana,haitachukua muda jamaa ni lazima aokoke tu,tena sio kwa mabavu! Bali mwenyewe ataomba apelekwe kanisani na huyo mwanaume ataokoka tu. Mungu anasikia maombi yako wewe mama na Mungu anafanya kazi sana na wewe,cha msingi ni kuendelea kuomba.
Sijawahi kuona huduma nzuri iliyokosa mwanamke,au huduma yenye upako bila mwanamke,ikiwa wewe umeiona basi nipigie kisha uniambie ipo wapi hiyo duniani!. Mungu anapenda mtu ambaye huamini kwa haraka. Na mojawapo ya tabia nzuri ya wanawake ni kuamini neno la Mungu kwa haraka zaidi ya mwanaume. Mimi nafikiria kama Yesu anarudi leo na gafla tusikie yupo sehemu fulani na anahitaji awanyakue watu wote watakamkimbilia nakuambia ni wanaume wachache sana watakao kwenda kuliko wakina mama na wanawake,nao ndio watanyakuliwa.
Kwa hili,pata picha uwapo kanisani kwenu kisha mkaambiwa wote sala na maombi yenu yamesikiwa sasa umshukuru Mungu,hata hapo utaona ni wanaume wengi watakuwa na maswali kwamba hivi kweli inawezekana? Hali ni hao hao wanaume waliokuwa wakiomba,lakini kwa upande wa wanawake utaona wengi wakiamini na kuanza kushukuru.
Wanawake sio viumbe dhaifu,bali ni watumishi wa Mungu kama ilivyo leo kwa wanaume. Kwa sababu ukizungumzia kanisa leo hii unazungumzia wanawake. Ukizungumzia praise and worship (vikundi vya sifa na kuabudu) unazungumzia wanawake,ukizungumzia vikundi vya maombi bado unazungumzia wanawake,ukizungumzia ushers/wahudumu wa kanisani unazungumzia wanawake. Si,haiwezekani watu wa namna hii wakawa wadhaifu hivyo inavyosemwa na wengine. Maana ikiwa wanawake ni dhaifu,je huduma ya Kristo ni dhaifu? Kama huduma ya Kristo si dhaifu basi na wanawake si dhaifu maana unapozungumzia huduma ya Kristo leo,unazungumzia sehemu kubwa sana ya wanawake!’ Umeona hapo 😀😀😁
Sasa,ikiwa kama unataka kanisa lenu liwe active/ na nguvu basi wape nafasi wanawake wenye karama mbalimbali na anza kuwatumia kisha utaniambia mabadiliko ya kanisa lako yatakavyokuwa. Hata injili ya ufufuko wa Bwana ilihubiriwa na mwanamke ( Yohana 20:17-18). Naye Yesu alihudumiwa zaidi na wanawake ( Luka 8:2-3)
Hivyo tunawahitaji sana wanawake kwenye kila huduma ya Bwana,maana wao ndio wameshikilia huduma kwa sehemu kubwa sana.
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments