top of page

MWANAMKE NI JESHI KUBWA.


Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;” Zab. 68:11

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Ukweli ni kwamba mwanamke yeyote ana nguvu ambazo mwanaume hana. Uwezo wa nguvu za mwanamke upo ndani yake wakati uwezo wa nguvu za mwanaume uonekana nje,mfano mwanaume ana maumbile ya misuli,kifua kipana( mbavu Nene)sauti nzito,mkono uliojazia,( ngumi jiwe!!!) n.k

wakati mwanamke hana mambo hayo yote,kitendo cha kukosa hayo mambo ya nje hakina maana kwamba hana nguvu,bali nguvu zake zi ndani yake mwenyewe. Hivyo mwanamke awe aliyeokoka ama asiyeokoka,awe anayejitambua au asiyejitambua lakini ujue ana nguvu ya kugeuza vitu tena kwa haraka zaidi hata ya mwanaume.

Biblia inamwita mwanamke mwenye kutangaza habari njema kuwa ni “jeshi kubwa “ Nini biblia imeona kwa mwanamke hata kumfananisha na jeshi kubwa? Unajua unapozungumzia kuhusu jeshi kubwa una maana ya watu waliokuwa na mafunzo ya kujilinda na kushambulia, Watu wenye uwezo wa kutumia silaha zote,watu wenye kujua mbingu za kupambana na adui,watu wenye uvumilivu mkubwa,watu wenye ngome N.K ( Sifa zipo nyingi za jeshi)

Kule nchini Israeli katika askari wa juu ambao ni “mashushu / wapelelezi” wenye vyeo vikubwa,idadi ya wanawake ni wengi. Nao ndio hufanya kazi kubwa za kulinda taifa katika mipaka yake,tena wao hawabebi silaha nzito au wakati mwingine hawabebi silaha yoyote.

Mfano ukienda airport mjini TelAviv utaona wadada warembo hivi kwa mwonekano wa nje lakini hao ndio walinda usalama wa airport. Wamefundishwa mbinu zote za kivita na kila mbinu ya kushughulikia ugaidi. Tena wao ni rahisi kumgudua mharifu. Sisi waswahili husema “ hakuna mwanaume mgumu mbele ya mwanamke ”  Basi akiwepo mtu mbaya mwanaume,ujue anakamatwa kilaini tu,bila hata kutumia silaha.

  1. Mwanamke ni mjenzi wa nyumba yake.( Mithali 14:1)

Kumbuka;Jeshi lina uwezo wa kujenga kitu kwa haraka na kwa muda mfupi,hata watu wakashangaa! lakini pia lina uwezo wa kubomoa kitu ndani ya dakika chache mno na kila mmoja akapigwa na butwaa!! Mwanamke ambaye ni “jeshi” ndiye hasa mwenye kuijenga nyumba yake akiwa na “hekima” kwa muda mfupi sana. Watu wengine hata wakashangaa.

Lakini huyo huyo,ndiye mwenye kuiharibu nyumba yake akikosa hekima,tena kwa muda mfupi tu. Hata kama mwanaume utatumia misuli ya kumpiga lakini kamwe hutamweza. Kwa maana mwanaume atatumia mabavu kama sehemu ya nguvu zake, lakini mwanamke silaha yake ya kwanza ni “mdomo” . Maneno elfu moja na hasira kali ya mwanaume,italipwa kwa neno moja kutoka katika kinywa cha mwanamke na huyo mwanaume atakuwa Chali!!!kwisha habari yake! Kuonesha kuna kitu cha namna yake ndani ya mwanamke

Nenda kasome kwa muda wako juu ya watumishi wa Mungu wakubwa walivyoangishwa na mwanamke,Kisha uone! Sasa nikuulize swali,hivi ikiwa mwanamke hana nguvu anawezaje kumwangusha mwanaume? Jijibu mwenyewe tu. 

Hivyo; mwanamke yeyote akikaa katika nafasi yake ipasavyo,huyo mwogope kwa maana aweza kufanya Jambo lolote hata ulimwengu wa roho ukashangaa!!! 

Biblia isemapo mwanamke ni jeshi Ina mzungumzia mwanamke ambaye amejitambua,Yesu ni Bwana kwake. Huyo,ni jeshi kubwa katika ulimwengu wa roho. Kwa maana huduma ya mwanamke ina neema tofauti sana na ya mwanaume. Kwa maana mwanamke amepewa “roho ya kuomboleza” hali ya kiroho yake ipo juu sana, mwanamke ni mwombaji 

  1. Wanawake sio dhaifu!

Kuna watu wanawatazama kuwa wanawake ni watu dhaifu hivi. Au ni watu wa kijinga kijinga hivi,watu wa kutumiwa kwenye mapenzi na kuachwa! Hapana huo sio mtazamo sahihi wala sio mtazamo wa kibiblia. 

Neno “dhaifu”  ni linaeleza ya kuwa na mapungufu, lakini tukumbuke Kila mmoja ni mdhaifu kwa mwenzake ( mwanaume ni mdhaifu kwa mwanamke,na mwanamke ni mdhaifu kwa mwanaume). Hivyo hakuna mdhaifu aliyemzidi mwenzake,kwa maana wote wanahitajiana. Unajua wengi wenye mtazamo huo ni kwa sababu wamemwona mwanamke kama “ msaidizi ” hivyo,wakatafsiri Neno hilo msaidizi kama mtu dhaifu. Lakini nataka nikuulize swali wewe, ;

Hivi akiwepo mwanaume ambaye ameambiwa anyanyue jiwe,ambalo kwa kweli linamshinda. Kisha akapewa msaidizi wa kumsaidia kunyanyua jiwe Hilo. Halafu,alipokuja msaidizi gafla jiwe Hilo likainuliwa pamoja,sasa msaidizi hapo ni mdhaifu? Mtu asiyekuwa na nguvu? Au vipi? Kwa maana jiwe limenyanyuliwa baada ya kuja msaidizi! Bila shaka hapo msaidizi ndiye hasa amekuja kusababisha jiwe linyanyuliwe,naye msaidizi ana nguvu kaja nazo,la kama angelikuwa dhaifu asiyekuwa na nguvu,Basi jiwe lisingeondolewa! Jifunze hapo.

  1. Mwanamke ana neema ya nguvu kiroho 

Ebu fikiria hivi; Ikiwa jambazi au mwizi ataingia kwenye nyumba nani wa kwanza kumfunga? Bila shaka jambazi atakwenda kushughulika na mwenye nguvu na kuhakikisha anamfunga vizuri,ili awe salama katika ujambazi wake. ( Soma: Marko 3:27,Mathayo 12:29)

Katika ulimwengu wa roho hali iko hivyo hivyo,kama shetani anataka kuipiga familia yako,hutafuta kwanza yupi mwenye nguvu,Kwa maana naye anajua kama akimpiga mwenye nguvu,ujue hapo  kafanikiwa kuipiga familia yote. Na kwa sababu hiyo, adui akitaka kuivuluga familia hutafuta kwanza nani mwenye nguvu,

Kisha kupitia huyo, akifanikiwa kumvuluga basi hapo ujue wote mtavuligwa mpende msipende. Na mara nyingi adui ukimbizana na mke / mwanamke katika ndoa au familia. Akijua kabisa kupitia huyu,mwanaume hana ujanja!!! Anajua nguvu ya ulinzi iliyopo kwa mwanamke,

hivyo akimkamata sawa sawa mwanamke na kumvuluga,basi ujue baba / mume naye lazima avulugwe,yaani atavulugwa hadi ofisini kwake,naye atayumba vibaya sana. Kwa sababu mwenye nguvu kakamatwa na kuvulugwa !

Alikwenda kuwapasha habari njema mitume ( Soma Yoh.20:16-18). Hii ina maana kwamba Yesu alitambua nguvu iliyopo ndani ya mwanamke kwamba ni nguvu ya kipekee.

  1. Kusudi la Mungu kwa mwanamke.

01. Awe msaidizi kwa mumewe ili kukamilisha huduma ya Mungu kwa pamoja. 

BWANA Mungu akasema, `` Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Mwanzo 2:18. Neno la Mungu linatuambia kwamba mwanamke amefanyika msaidizi kwa mwanamume.

Tena neno hili “ msaidizi” lina maana ya yule awezeya kukifanya kitu kuwa kamili au ni yule awezaye kuwezesha hata kukafikia utimilifu. ( Roho mtakatifu naye ni msaidizi wetu,anayetukamilisha hata tufikie viwango vya utakatifu anaoutaka Bwana )

02.Kusababisha nguvu ya ongezeko katika huduma ya Mungu.

Maongezeko ya watu kwenye nyumba ya Mungu hutegemea sana mwanamke. Kwa maana mwanamke amepewa uwezo mkubwa wa kuatamia washirika kwa maombi,ushauri,ucheshi na ukarimu. Ndio maana huduma zote zinatoa kipaumbele kwa wanawake,mara nyingi zinakuwa ni huduma kubwa sana.

03.Kutawala pamoja na mwanaume 

Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale...” Mwanzo 1:28

Pamoja na kwamba mwanaume ndiye kichwa na nguzo ya familia tena ndiye baba kiongozi hasa wa familia, lakini bado Mungu anamkusudia mwanamke asimame kwenye nafasi ya kiutawala juu ya mambo ya nyumbani mwake,awe pamoja na mke wake.

03. Kuilinda ndoa yake.

Imeandikwa  “…mwanamke atamlinda mwanamume.” Yeremia 31:22. Hivyo mlinzi wa mume ni mke,mke ana wajibu wa kumlinda mumewe kwa njia nyingi kama vile Kwa maombi,kumtii, kumpenda,kumtimizia haya ya moyo ya mumewe n.k. Mwanamke mwenye kujielewa haibiwi mume! Hata iweje!!! Maana atamlinda mumewe.

  1. Nyongeza ya wajibu wa mwanamke.

Kuanzia agano la kale tunamwona mwanamke katika nyanja mbali mbali za kihuduma,kijamii na kifamilia. Mfano katika agano la kale,mwanamke mbali na kuwa mama wa watoto alikuwa akihusika na huduma pamoja na mwanaume. Hili tunaliona kupitia sheria za kiyahudi zilizowaagiza wanaume kujihudhurisha mbele za Bwana mara tatu kwa mwaka.

Wanaume walipokuwa wakienda wanawake walikuwa pamoja nao. Angalia kwenye matukio kama Kumb. 29:10-11,1 Samweli 1:3-9 ( Hana akiwa pamoja na mumewe Elkana walipoenda Shilo). N.K Hivyo wajibu wa kwanza na wa kipekee kabisa kwa mwanamke wa agano la kale ni;

 Kushiriki ibada pamoja na mwanamume.

Mwanamke hakutengwa tengwa bali alipewa nafasi katika ibada au huduma. Katika hili tunaweza kuliona kwa Miriamu ( Dada yake Musa). Miriamu alikuwa mmoja kati ya wanawake mashujaa wa agano la kale naye alikuwa na huduma ya uimbaji katika kusanyiko. Tunamuona akiongoza ibada kwa kundi lote la wana wa Israeli walipokuwa wakitoka Misri utumwani,

walipovushwa katika bahari ya shamu sasa wanamfanyia Bwana ibada Miriamu mwanamke nabii mke mashuhuri akiongoza kundi; ( Kutoka 15:20-21)

Kuilea familia.

( Akina  Sara,Ketura,Rebeka,Lea,Raheli n.k walikuwa ni akina mama wa familia katika jukumu la kulea watoto na familia zao) 

 Kutangaza injili.

Katika mtazamo wa mwanamke wa agano jipya,ulikuwa ni kwa kusudi la kupeleka injili ya Yesu Kristo. Tunamuona mwanamke mwinjilisti aliyekuwa kisimani na akakutana na Yesu. Hatimaye alipofumbuliwa macho yake akaingia mjini kueneza habari njema ( Yoh. 4:28-29). Lakini si hilo tu,

bali kulikuwepo na wanawake wengi waliofanya kazi ya injili kwa mali zao. Hawa walimuhudumia Yesu kwa mali zao ( Luka 8:2-3). Hata leo,wanawake wanaendelea kupambana na kazi ya uinjilisti kwa sababu Bwana anawatumia.

Kumbuka ikiwa wewe ni mwanamke mshukuru sana Mungu aliyekuumba kuwa mwanamke. Jikubali na usimame katika wajibu wako,maana una kitu cha kipekee kwa ajili ya Bwana.

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe,pamoja na MAOMBI piga sasa kwa +255 683 877 900

What’s app namba +255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page