top of page

MWANA-KONDOO WA MUNGU (Yoh.1:29)


Na mch.Madumla

Na mchungaji Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe….

Kwa ufupi,

Dhambi ilipoingia ulimwenguni ilimtenga mwanadamu na Mungu wake. Mtu yule aliyekuwa shirika na Mungu sasa hana shirika tena,yupo mbali na Mungu wake kwa sababu ya dhambi.

Dhambi siku zote husimama kama ukuta utengao magharibi na mashariki au kaskazini na  kusini hata kushindwa kuonana na ndivyo tunavyotengwa sisi na Mungu wetu pale dhambi ikichukua nafasi ndani yetu.

Adamu na Hawa wakafukuzwa kutoka bustanini (Mwanzo 3:24) kwa kuwa walikosa. Hata vizazi vilivyoongezeka vyote vikawa vimepotoka.

Toka mbinguni BWANA aliwachungulia wanadamu,Aone kama yuko mtu mwenye akili,Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja,Hakuna atendaye mema,La! Hata mmoja.” Zab.14:2-3

Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani akauzunika moyo  (Mwanzo 6 :6). Akasema kuwafutilia mbali wanadamu wote,kwa kuwa ni waovu tu siku sote; Lakini tazama,Nuhu alipata Neema machoni pa Bwana. Hata hivyo bado kizazi kilichofuata nacho kilikuwa kiovu vivyo hivyo. Biblia inasema;

Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;” Warumi 5:12

Tazama,kwa kosa la mtu mmoja tu,sisi sote tulihesabiwa wenye dhambi. Hii ina maana kwamba kila aliyezaliwa alikuwa tayari amehesabiwa dhambi hata kama hajatenda chochote. Ulimwengu wote ulihesabiwa kosa la Adamu hata mauti. Kumbuka hili; mshahara wa dhambi ni mauti ( Warumi 6:23) kwa lugha nyepesi ni kwamba sote tulihukumiwa mauti kama pato la dhambi zetu kwa sababu ya kukosa kwake mtu mmoja.

Kila mtu alikuwa na dhambi sasa,hakuna yule aliyesalimika kwa maana tumeingizwa dhambini. Hii ni hatari,sababu hata ungelikuwa ni mtu wa matendo mazuri kiasi gani lakini bado wewe umehesabiwa dhambi hata mauti.

Dhambi ilileta mauti.

“….kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:17 Hivyo ndivyo alivyosema Bwana. Mauti ikaingia kwanza mauti ya kiroho,hata mauti ya kimwili     “…; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.“Mwanzo 3:19.Tazama hapo sasa dhambi ilivyoharibu maisha halisi ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.Kumbe hata wewe hauko salama nje ya wokovu.

Mambo manne uliyoyapata bila kupenda.

Kuna baadhi ya mambo ambayo mwanadamu amezaliwa na kuyakuta tayari yameandaliwa kwa ajili yake pasipo hata kushirikishwa au pasipo kupenda. Mambo haya ni kwa kila mtu,nayo ni;

a) Jinsia ( unazaliwa ukiwa una jinsia ya kike au kiume pasipo kushirikishwa. Hakuna uchaguzi wowote bali ulivyozaliwa ndivyo utakavyokuwa upende usipende na hakuna mahali pa kushtaki)

b) Majina ( majina unayoitwa hivi sasa umezaliwa tu ukapewa wala hukushirikishwa,yaani unajikuta tu ukiitwa fulani bin fulani. Inawezekana baadae ukabadilisha jina lako, lakini majina tunapewa hata mengine hatuyapendi,basi tu ili mradi!)

c) Ukoo (Unajikuta tu umezaliwa katika ukoo fulani,yaani hukupenda lakini ndio hivyo tena umeshazaliwa kwenye ukoo fulani. Wala hakuna pa kushtaki kwamba kwa nini umezaliwa katika ukoo huo.)

d) Dhambi (Hii ndio mbaya zaidi! vile umezaliwa lakini umekwisha hesabiwa hatia kwa sababu kwa kosa lake mmoja wewe nawe umejumlishwa.) Hapa ndipo nataka tupaangalie kiundani tunapojifunza kuhusu mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.

Kwa mujibu wa sheria zilizowekwa hapo zamani pale mtu alipofanya dhambi ilimbidi alete mnyama wa kuteketezwa awe sadaka ya dhambi badala yake. Mnyama huyu aweza kuwa ni mwanakondoo,mbuzi au ng’ombe wa sadaka ya dhambi. Kuhani utekeleza kufanya upatanisho.

Hivyo;mtu akifanya dhambi ilimbidi asongeze sadaka ya dhambi ya mnyama mfano mbuzi kwa sadaka ya dhambi. Kisha uenda kwa kuhani,mwenye dhambi huweka mikono yake yote miwili kichwani mwa mbuzi (sadaka ya dhambi).

Pale mwenye dhambi awekapo mikono yake kichwani mwa mbuzi,dhambi za mtu huyo huama kutoka kwake mwenye dhambi na kuingia kwa mbuzi,kisha kuhani humchinja na kupeleka damu ya mnyama madhabahuni (nyingine uimwaga pembezoni mwa madhabahu na nyingine madhabahuni)

Hapo sasa kuhani hufanya upatanisho. ( Mambo ya walawi 4:27-30). Kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti,ilimbidi mwenye dhambi afe kwa sababu ya dhambi zake,lakini mwana kondoo hufa kwa ajili yake,au mbuzi hufa kwa ajili yake. Damu ya mbuzi ilikuwa haiwezi kuondoa dhambi isipokuwa ilikuwa ikifunika dhambi na ndio maana kulikuwa na kumbu kumbu la dhambi kila mwaka ( Waebrania 10:3-4). Ni damu ya Yesu tu ndio yenye kuweza kuondoa dhambi zetu (Mathayo 26:28).

Hivyo basi; kila aliyekuwa ametenda dhambi,ilimbidi achukue kondoo wa kuchinjwa sadaka ya ondoleo la dhambi kwa kipindi hicho. Damu ilihusika katika kufanya upatanisho kwa mtenda dhambi na Mungu wake. Tena damu ni uhai wa mwili;

Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.” Mambo ya walawi 17:11

Sasa,tazama kwa makini tena zile hatua za kwanza za upatanisho kwa njia ya damu ya mwanakondoo,mbuzi au ng’ombe. Zilikuwa kama ifuatavyo;

a)Ilihitajika kuwepo na mwanakondoo wa dhambi,atakayefanyika dhabihu ya dhambi.

b) mwanakondoo wa sadaka ya dhambi hupelekwa kwa kuhani tayari kwa sadaka ya utakaso.

c) Mikono ya mwenye dhambi huwekwa kichwani ili dhambi zake ziamie kwa mwanakondoo naye awe huru na dhambi hizo.

d)Mwanakondoo kufanyika dhabihu ya kuteketezwa.

e) Damu yake kupelekwa madhabahuni kwa ajili ya utakaso kamili.

Je kwa Bwana Yesu ilikuwaje?

Kumbuka kipindi cha ubatizo wake Bwana Yesu. Yohana alitaka kumzuia Yesu ili yeye Yohana abatizwe na Yesu (Mathayo 3:14),lakini Yesu alimwambia; “Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.” Mathayo 3:15

Yohana hakutambua kwamba yeye ndie aliyepaswa kumbatiza Yesu,ili Yesu naye awe mwana-kondoo wa sadaka ya dhambi. Biblia inaposema “ kutimiza haki yote”  ina maana kwamba huo ndio ulikuwa ni mpango wa Mungu kutimiza kusudi la kumuokoa mwanadamu katika mauti aliyopokea kutoka kwa adamu wa kwanza.

Sasa angalia kwa makini hili; Yohana alifanyika kuhani pale alipombatiza Yesu.( Kama ilivyokuwa hapo kwanza.) Kwa kuwa ulimwengu wote umehesabiwa dhambi,basi ilimbidi Yohana kuweka mikono yake kichwani mwa Yesu ikiwa na maana ile ile kwamba dhambi ya ulimwengu sasa inahama na kuamia kwa Yesu. Kumbuka kwamba,Yesu hakutenda dhambi lakini alihesabiwa dhambi zetu akafanyika laana kwa dhambi ya ulimwengu.

Tazama kile kilichotokea; Yohana akaweka mikono yake kichwani mwa Yesu,dhambi ya ulimwengu ikaibeba Yesu. Kisha Yohana akambatiza, naye Yesu alipobatizwa , Yohana sasa asema wazi wazi kwamba;

Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! “Yoh. 1:36

Linganisha zile hatua za kwanza hapo juu,(hatua za upatanisho kwa damu ya mwanakondoo wa kawaida asiyeweza kufuta dhambi moja kwa moja) pamoja na hatua za Yesu mwana-kondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu,mwenye kufuta dhambi kabisa-Tazama;

a) Yesu amefanyika mwana-kondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu.

b) Yesu mwana-kondoo yupo mbele ya kuhani Yohana (Kabla ya kuwekewa mikono na kubatizwa.)

c) Yohana aweka mikono yake kichwani ( Dhambi ya ulimwengu inaama na kuingia kwa Yesu)

d)Yesu amefanyika dhabihu ya dhambi yako (ulimwengu)

e)Yesu naye apeleka damu yake  madhabahuni. (Pazia la hekalu lapasuka.)

Imeandikwa;

Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba….” Yohana 20:17

Hivyo basi Yesu ni mwana-kondoo wa Mungu aliye hai kwa ajili yako,yupo hai hata sasa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako (Mathayo 26:28). Kumbuka jambo moja usilisahau kabisa; dhambi zako haziwezi kusamehewa nje ya damu ya mwana-kondoo wa Mungu. Ukimpokea Yesu,umepokea samaha la dhambi zako. Kumbuka Yesu amekufa na kufufuka pale msalabani kwa ajili yako wewe,mwamini sasa ili uwe na uzima sasa na wa milele.

Damu ya mwana-kondoo wa Mungu i hai,inaishi na ina nguvu ya ajabu ndani yake. Yesu ni mwana-kondoo wa Mungu sadaka ya dhambi zako. Laiti ulielewe neno hili umpokee Yeye afute dhambi zako leo,nawe uondokane na mauti iliyoingia kupitia adamu wa kwanza. Kumbuka;

Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.” Warumi 5:18.

Fanyika mwenye haki kwa kuanza kumpokea Bwana Yesu Yeye mwenye haki,mwenye kufanya upatanisho wa kweli.

Usisite kabisa kunipigia simu hizi,ili niombe na wewe. Piga sasa; +255 683 877 900

Mchungaji G.Madumla.

What’s app +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page