top of page

MWAKA MPYA NA MABADILIKO

Updated: Sep 29, 2022



Mwaka mpya ni mabadiliko ya tarehe/Kalenda,lakini upya wa kitu uanza ndani Yako!”

Nilipokuwa mdogo hivi,nikiwa mimi na wadogo zangu na dada yangu tulikuwa tuna tabia ya kuushangilia mwaka mpya kwa kelele za kupiga madebe,mabati usiku. Hivyo ilitulazimu kulala mchana kwenye ile siku ya tarehe 31 December. Ili usiku tuweze kushangilia bila usingizi! Hatukuwa peke yetu,bali mtaa mzima wa Sinza white-inn ndio ilikuwa desturi yetu. 

Na mwaka mpya ukifika,ile tarehe moja kama utanitembelea siku hiyo,jambo moja utakaloliona kwangu ni kuchoma makaratasi au manguo fulani hivi ambayo siyavai. Nikiamini kwamba nimebadilika na kuingia mwaka mpya. Hivyo nimebadilika kwa kuyachoma mauchafu ya zamani!


Lakini sasa nimekuwa,nimegundua kwamba sikuwa sahihi kwa maana badiliko huanzia moyoni mwangu na si kuchoma makaratasi wala si kwa kushangilia mwaka. Kumbe mwaka mpya ni badiliko tu la kalenda,lakini mwaka mpya ni zaidi ya hapo. Najua hata wewe yamkini ndivyo ufanyavyo hata sasa.!! Nami nimekuandikia kukupasha habari kwa lengo la kubadilisha ufahamu wako leo kwa maana tunaelekea mwaka mpya hivi punde.


Hivi,unafikiri mwaka mpya una thamani gani ikiwa wewe upo vile vile? Unafikiri mwaka mpya una maana gani kwako? Au unafikiri hatma ya maisha yako unategemea kubadilika kwa mwaka? Au unafikiri utafanikiwa ikiwa wewe mwenyewe hujabadilika? Weweza kujijibu mwenyewe hayo maswali,lakini mimi leo nataka nikuambie kwamba mwaka mpya unamaana ya mabadiliko ya kalenda kitarehe na mabadiliko mengine. Lakini mabadiliko hayo hayana maana yoyote kwako ikiwa wewe hujabadilika!


Fikiria ulivyokuwa mwaka jana,na.ulivyo leo. Alafu fikiria kama ulikuwa hujafanya maamuzi sahihi ya kubadilika wewe mwenyewe,utaona upo palepale,wala hujasogea kimaendeleo ya kiroho na kiuchumi isipokuwa miaka imebadilika. Jambo moja kubwa la kujifunza ni wewe uwe mpya sasa,na hapo ndipo utaona thamani ya mwaka mpya.Kumbe hata leo inaweza ikawa mwaka mpya kwako ikiwa utafanya maamuzi ya kubadilika!

Maamuzi ya kubadilika ni yapi hayo?


01. Kukubali kukaa kwenye njia ya Bwana.


Ebu,jiangalie umesimamaje na Bwana? Ibada zako mwaka huu zikoje? Ukiona unamtumikia Mungu kwenye kiwango cha kawaida,basi ujue mwaka utabadilika na utakuwa vivyo hivyo.  Yeyote aliyeamua kukaza na Mungu,huyo ndiye amekuwa mpya na thamani ya mwaka mpya ataiona. Wengi leo tunaona mabadiliko ya kalenda tu,lakini tukiwa tumebaki vivyo hivyo kwa sababu hatujaamua kukaza kwa Bwana. Usikubali mwaka ubadilike nawe ukiwa bado upo palepale kiroho. Ikiwa kama bado hujazaliwa upaya/kuokoka inakulazimu uokoke sasa ili upya uanze leo. Mwaka mpya haukufanyi uwe mpaya hata kidogo


Badiliko la kweli linategemea moyo wako. Na yule awezaye kukubadili ni Mungu tu kwa Roho wake wa milele. Ikiwa ni hivyo basi ili uwe mpya unamuhitaji Mungu sana. Na kanuni ya Mungu ya kukufanya uwe mpya ni inaanzia ndani yako pale unapokuwa na shauku ndani yako ya kumuhitaji zaidi Mungu.


02.Ni hali ya kukubali kuwaacha baadhi ya marafiki ambao huwezi kwenda nao katika mafanikio yako. 


Marafiki wengi uliokuwa nao hawakupeleki kwenye hatma angavu. Huwezi kutembea na marafiki wenye mashauri mabaya. Ukiona rafiki akushauriye mambo kinyume na Mungu,basi ujue ya kwamba hawezi kukupeleka katika hatma yako. Biblia inasema “mazungumzo mabaya huaribu tabia njema” 1 Wakorintho 15:33. Tabia njema ni tunda zuri la kufanikiwa kwako. Tabia njema ni badiliko zuri. Ikiwa umeamua kubadilika huna budi kuwapunguza marafiki wabaya ambao ni chachu ya tabia mbaya. 


Wale wote wenye badiliko halisi ni wale tu waliofanikiwa kuwapunguza marafiki wabaya. Sijawahi kuona mtu aliye kuwa na upya na papo hapo ameambatana na marafiki wale wale wenye kuchoche mabaya. Usihangaike kujua mabaya ni mambo yapi,kwa maana kila jambo lenye shina la uovu ni baya. Ukiona mambo ambayo unayapokea kwa rafiki yako yanasintofahamu na kweli ya Mungu,basi ujue hayo ni mabaya.


03. Hakikisha unajua kutumia vizuri muda,nguvu na pesa.


Mambo matatu “ muda,muda na pesa” ni mambo muhimu sana kwako na ndio mambo yanayohusika katika kufanikisha malengo yako. Lakini katika kipindi hiki cha mwaka,jiulize maswali yafuatayo; je unatumiaje muda wako? Je nguvu zako umezielekeza wapi? Je unatumiaje pesa zako?. Haya  mambo ukiweza kuyatumia vizuri basi ujue mwaka mpya kweli utakuwa mwaka mpya kwako. Kuna watu wanatumia muda wao vibaya sana,utakuta wakitumia muda mwingi kupumzika kuliko kazi,au muda.mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kazi alizonazo.


Wengine wanatumia nguvu zao nyingi kwenye vitu visivyo na faida kwao. Mfano nguvu inayotumika kulumbana mambo ya watu,kwamba fulani kafanya nini na fulani kavaa nini. Ukiwakuta watu wa namna hii wakiongea utaona hadi misuri inawatoka! Wengine pesa zao huzitumia ktk mambo yasio na maana hata kidogo. Nafikiri unanielewa nisemapo hivyo!

Neno la Mungu linatutaka tuweze kutunza muda kwa kuukomboa wakati. Alikadhalika tujue namna ya nguvu zetu mahali pa kuzielekeza zaidi pamoja na pesa. Unahitaji mwaka mpya? Anza kuwa mpya leo! Na inawezekana!

Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900


Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446


Mchungaji Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page