top of page

MWAKA 2018,NI MWAKA WA KUINULIWA.


Na Mch.Gasper Madumla.

“ Kila bonde litainuliwa,Na kila mlima na kilima kitashushwa;Palipopotoka patakuwa pamenyoka,Na palipoparuza patasawazishwa;” Isaya 40:4

Kuinuliwa nini nini ?

Kuinuliwa ni kitendo cha kupandishwa kutoka chini.  Kinachoinuliwa ni kile kilichopo chini na kilichokosa msaada wa kuinuka chenyewe,ndipo sasa kinahitaji kuinuliwa. Hivyo,kuinuliwa kama tendo linahitaji wahusika wa pande mbili.

  1. Anayeinuliwa sharti awe chini.

  2. Anayeinua sharti awe juu.

Kama alivyo Mungu wetu Yeye yupo juu sana,juu ya vyote vinavyoonekana na visivyooneka,muweza wa yote. Hivyo Yeye Mungu husimama kwenye uhusika wa “kuinua”. Wewe huwezi kujiinua mwenyewe bali unahitaji MUNGU akuinue katika Jina la Yesu Kristo. Na mwaka huu Bwana ameachilia neno la kinabii kwamba “mwaka wa kuinuliwa”. 

Kuinuliwa kumebeba kanuni moja kubwa na ya msingi nayo ni “kuinuliwa kunahitaji kuonekana”. Ili uweze kuinua kitu chochote unahitaji kwanza ukione ndipo ukiinue. Huwezi kuinua kitu usichokiona hata mara moja! Kumbe,“kuonekana” ni muhimu sana,vivyo hivyo ili MUNGU aweze kukuinua kwa mwaka huu 2018 kama akuambiavyo leo,unahitaji kuonekana kwake. Mungu hawezi kuinua bila kukuona kwanza kama kanuni ya msingi. 

Utagundua kwamba ili neno hili la kinabii liwedhahili kwako,basi kuna kazi fulani unayotakiwa kuifanya. Unajua watu wengi wametabiriwa au wamepewa nabii nyingi wengine wameambiwa watafaulu mitihani yao na kuwa vichwa,wengine wamepewa nabii za kuwa mabilionea,wengine kuwa watumishi wakubwa N.K. lakini hawajui kwamba ili ufikie kwenye huo unabii kuna kazi ya ziada ya kufanya,yaani ni kuacha kazi na kufanya kazi,kukubali kulipa gharama. Hakuna jambo zuri lisilokuwa na gharama!

Vivyo hivyo,mwaka huu Bwana anakuambia sasa ni mwaka wako wa kuinuliwa kwenye maeneo yote,lakini usisahau kuna kulipa gharama ili uinuliwe. Usitishike na hayo,bali ujue kwamba Bwana atakuinua. Kumbuka;ili Mungu akuinue kwenye eneo lolote ni lazima akuone kwanza,na ikiwa ni mmwaka wako wa kuinuliwa ujue Bwana ameliona teso lako,Bwana ameyaona mahangaiko yako,Bwana amekiona kilio chako. Yeye ni Mungu ashikaye maagano yake sana. Tazama aliwainua Wana wa Israeli kwa sababu kwanza aliwaona kisha akalishika agano lake -( Kutoka 4:24-25)

Maangaiko yako ya mwaka jana,Bwana anakwenda kuyaondoa. Kilio chako kimemfikia Bwana,amini tu;kama vile Waisraeli walivyoinuliwa kutoka utumwani ndivyo utakavyoinuliwa wewe katika hali yako. Mungu ni mwaminifu sana,hatakuacha na wala hajakuacha kwa neno lake atakuinua utoke kwenye hilo gereza,atakuinua kutoka kwenye huo ugonjwa,amini na upokee kuinuliwa kwa mwaka huu 2018. 

Waisraeli walimlilia Bwana ( Kutoka 4:24-25),hawakuacha,Na Mungu akasikia. Kumbe Yeye Mungu hujishughulisha sana na mambo yetu naye hutusikia tuombapo ijapokuwa ni kwa machozi mengi lakini Yeye yupo nasi,nami ninakuambia utainuliwa kwa viwango vya juu. Utapaa juu kama tai,biashara yako itainuliwa katika Jina la Yesu Kristo.

Ni kawaida ya Mungu kuwainua watu wake hasa wanyonge. Namtazama Mungu aliyemuinua mwanamke Hana mke wa Elkana kutoka katika kilio cha utasa hata Hana akanyonyesha ndipo Hana akamuimbia Bwana akisema;

“Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,Humpandisha mhitaji kutoka jaani,Ili awaketishe pamoja na wakuu,Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA,Naye ameuweka ulimwengu juu yake.” 1 Samweli 2:8 ( soma pia Zaburi 113:7-8)

Bwana atakuinulia watoto wewe mama usiyekuwa na watoto. Bwana atakuinulia mibaraka yako kwa watoto wako uliowazaa amini na upokee katika Jina la Yesu Kristo. Lakini ninampenda huyu mwanamke Hana kwa kuwa alikuwa ni muombaji asiyechoka hata Bwana akamkumbuka. Kumbe hata wewe ili uinuliwe zaidi huna budi kuwa muombaji usiyechoka katika mwaka huu na miaka mingine yote. Jifunze kwa Hana. 

Je nichukue hatua zipi ili niinuliwe?

  1. Kwanza ujikubali na uwe na utayari wa kuinuliwa.~ usijidharau kwamba hufai,au usijione kwamba huwezi,bali jikubali jinsi ulivyo hivyo hivyo. Jifunze kwa Bartimayo kipofu,alijikubali kisha akawa na utayari wa kuinuliwa ajapozuiliwa bali alikaza kumuitia Bwana ( Marko 10:46-52)

  2. Amini kuinuliwa ~ lipokee neno na ona tofauti kuinuliwa.

  3. Itengeneze njia ya Bwana ~ Mungu atawainua wale wanyenyekevu,waliokubali kumuishia Yeye. (Isaya 40:3)

  4. Kataa muambatano na watu wasio sahihi kwako.~ watu ambao hawatakusababisha kuinuka,wakatae kwa gharama yoyote ile.

  5. Ni lazima ufunguliwe ikiwa upo kwenye vifungo~ Ukiona umefungwa eneo lolote,basi unahitaji kufunguliwa kwanza. Ni muhimu sana kukimbilia kwenye maombi ya ukombozi uwe huru ndipo uinuliwe na Bwana.

Ukiinuliwa katika eneo lolote lile usisahau kwamba“umeinuliwa”wala hujanyanyuka mwenyewe bali“ umeinuliwa tu”. Hivyo Lazima nawe uwe sababisho la kuwatia moyo na kuwasaidia wengine wainuliwe. Pokea neno hili la kinabii kwa mwaka huu 2018,ni mwaka wa kuinuliwa katika Jina la Yesu Kristo.

Ikiwa unahitaji mambo haya kwa kina,au ikiwa unahitaji maombi naomba usisite kunipigia,

Piga sasa kwa +255 683 877 900/655 111 149/762 414 446. 

Namba ya what’s app ni +255 655 111 149.

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page