MUUJIZA WA KIWETE – (MATENDO 3:1-6)
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 1, 2017
- 3 min read
Updated: Sep 5, 2022

Iko habari njema ya uponyaji iliyoandikwa katika kitabu cha matendo ya mitume sura ya 3:1-10 Ndani ya habari hii,tunajifunza mambo mengi sana. lakini nataka tujifunze mambo matano tu kwa ufupi,nayo ni
BWANA ni mwenye huruma
Jina la Yesu laokoa
Ibada ina muda maalumu.
Umoja katika kazi ya Bwana
Kumsifu Bwana baada ya muujiza.
01.Bwana uhurumia watu wake.
Najaribu kufikiria pale yule kiwete alipowaangalia Petro na Yohana huku moyoni mwake akitaraji kupata msaada wa fedha lakini Petro na Yohana hawakumpa msaada huo mdogo wa kimwili bali wakampatia kilicho bora zaidi.Huruma ya Mungu inakuja pale watumishi hawa (Petro na Yohana) kuamua kusimama japo kwa dakika chache kumsikiliza huyu mlemavu kwa maana wangeliweza kumpita na kuendelea na safari yao kwa maana walikuwa wakiwahi ibada. Ni huruma tu ya Bwana hata kuwafanya watumishi wake kutumia muda wa kumsikiliza na hatimaye kuachilia uponyaji.
02.Yesu atenda muujiza.
Ukisoma katika Matendo 3:1-10,utagundua kwamba kiwete hakuponywa kwa nguvu yoyote ile isipokuwa kwa nguvu za Mungu,kwa jina la Yesu tu. Hii imeandikwa ili wewe na mimi tujue kwamba jina la Yesu tu limebeba miujiza yetu yote,lakini si hivyo tu,lazima tujue kwamba hatupaswi kutumia jina lingine ikiwa kama tunataka kupata miujiza ya kweli.
Mlemavu huyu alipokea muujiza wa aina yake ambao haujawahi kutokea kabisa Israeli yote kwa maana miujiza yote iliyotangulia ilihusisha imani ya mtendewa muujiza,lakini haikuwa hivyo kwa huyu kiwete kwa maana kiwete hakuwa na imani ya kuponywa kabisa! isipokuwa alichokuwa nacho kichwani mwake ni kusaidiwa pesa ya kula ugali. But Yesu ni zaidi ya ugali,alipotajwa,akaponywa mtu aliyekuwa hajawahi kutembea kutoka kuzaliwa kwake.
03.Ibada huzingatia muda maalumu.
Biblia inataja muda maalumu ambao Petro na Yohana walikuwa wakienda kusali (Matendo 3:1). Hii ni kuonesha wazi kabisa kulikuwa na muda maalumu wa ibada waliojipangia na katika muda huo kazi ilikuwa ni moja tu nayo ni ibada. Hivyo kama ungelimtafuta Petro na Yohana katika muda huo basi ni wazi kabisa ungeliwapata kanisani maana ndio mida hiyo ya ibada.
Kutajwa kwa muda katika mstari huo kunaonesha ni kwa namna gani akina Petro walivyokuwa wanavyozingatia muda wa ibada. Na kwa sababu hiyo muujiza huo ulipangwa kutendeka katika muda huo huo, Watu wengi hawajajua kwamba miujiza nayo ina mida yake iliyopangwa na Bwana. Kuzingatia muda wa ibada ni kukutana na muujiza wako.
04. Umoja katika kazi ya Bwana.
Neno linasema “tutazame sisi” Matendo 3:4 Neno “sisi” linaonesha umoja waliokuwa nao Petro na Yohana. Walitambua hawako peke yao bali wako na Bwana,kwa hiyo neno “sisi” humtaja wao pamoja na Bwana wakiwa katika hali ya umoja. Na kama unavyofahamu kwamba Mungu wetu hupenda umoja hasa katika kazi yake,hapo Yeye hushuka na kutenda miujiza. Siri hii Petro na Yohana walikuwa wakiijua
Hata leo ukitaka kuona mkono wa Bwana ukitenda,basi jaribu kutengeneza umoja katika Bwana. Chochote ufanyacho fanya na mwingine mwenye kumpenda Mungu kama ulivyo,basi ujue katika umoja huo mtayaona makubwa.
04. Kumsifu Bwana baada ya muujiza.
Yule Kiwete alipokwisha kupokea muujiza wake,akaingia hekaluni akimsifu Mungu (Matendo 3:8). Hivi tuulizane hapa mimi na wewe kwamba huyu aliyekuwa kiwete alifundishwa wapi kumsifu Mungu? Bila shaka muujiza ule aligundua aliyemponya ni Mungu wala si Petro au Yohana. Na aliojua hilo hakuwa na cha kumpa Mungu zaidi ya sifa zake naye akaanza kumsifu Bwana aliyemtendea.
Hata kwako,unapotendewa na Bwana kumbuka kurejea kwake kwa kumsifu kwa maana ni Bwana alikutendea na jambo hili ni kubwa sana.
Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,pia nifahamishe kama neno hili limekubariki ili tumshukuru Mungu pamoja.
Namba zangu ni +255 683 877 900.
What’s app number ni +255 746 446 446
NaMch.Gasper Madumla
UBARIKIWE.
コメント