MUNGU NA MWANADAMU KAMILI ASIYETENDA DHAMBI – YESU
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 11, 2017
- 3 min read

Na Mch.G.Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
Ni muhimu kujua hivyo kwamba Yesu ni Bwana MUNGU kamili pia ni mwanadamu lakini Yeye hakutenda dhambi,Yeye ni mtakatifu wa watakatifu,Bwana wa mabwana. Hakutenda dhambi.
Ninakuandikia kwa ufupi vile biblia inavyomuelezea Yesu,sasa ; tukianza kuziangalia injili nne. Utagundua kwamba kila mwinjilisti alikuwa na mapana ya kumuelezea Yesu jinsi alivyoongozwa na Roho mtakatifu. Lakini katika injili tatu za mwanzo yaani Mathayo,Marko na Luka hawa watatu wamezungumzia uanadamu wa Yesu katika nyanja tofauti tofauti,isipokuwa mwinjili Yohana yeye anamuelezea Yesu kama MUNGU halisi.
Tuanze kujifunza kwa ufupi kwa maandiko mawili ya msingi yenye kutufundisha uanadamu na Uungu wa Yesu.
(I) YESU (MUNGU)
“ Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” 1 Yoh.5:20
“huyu ndiye Mungu wa kweli” maneno haya yameeleza wazi kabisa ya kwamba Yesu ndie Mungu wa kweli. Ukiona katika biblia pameandikwa “Mungu wa kweli” basi ujue kuna “ mungu wa uongo” mahali pendine. Naipenda jinsi injili ya Yohana nayo ilivyoanza kuandika habari za Yesu Kristo. Yeye Yohana kaanza kueleza Uungu wa Yesu moja kwa moja katika hali ambayo kwa wengine ni fumbo hata sasa,anasema;
“ Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yoh.1:1,14
Huyu neno ambaye alikuwako kwa Mungu,alikuwa Mungu naye akauvaa mwili kisha akaja duniani,akazaliwa kama mwanadamu kusudi atukomboe sisi tuliokuwa chini ya sheria. Na hivyo ndivyo alivyo Yesu. Yeye ni Imanueli,Mungu pamoja nasi ( Mathayo 1:23). Yesu alipouvaa mwili ilikuwa atupe kielelezo cha sisi kujifunza kwake.( Mathayo 11:29)Ukweli ni kwamba aliyemuona Yesu amemuona Mungu,kwa maana ni umoja hao.Yohana 14:9. Sasa jaribu tena kupitia ile habari ya Filipo (Yoh.14:1-9),pale ambapo Filipo alihitaji kumuona Mungu,lakini Yesu akamwambia yeyote aliyemuona Yeye Yesu amemuona Baba (Mungu).
Kwa sababu ya kushindwa kumfahamu Yesu vizuri,basi leo watu wengi wamechanganyikiwa kwa kushindwa kujua Yesu ana uungu ndani yake maana Yeye ni Mungu kamili.
(II)YESU (MWANADAMU)
“ Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;” 1 Timotheo 2:5-6 Hili ni moja kati ya maandiko yenye kueleza kwamva Yesu pia alikuwa mwanadamu. Ni vyema tukajua kwamba Yesu naye aliona njaa kama mwanadamu ( Mathayo 4:1-2),alilia ( Yoh.11:43). Katika yote hayo Yesu hakutenda dhambi “ Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” 1 Petro 2:22
Mathayo anaandika kwamba Yesu ni kama mfalme,Marko anamuandika kama mtumishi wa Mungu,Luka anamuandika kama mwanadamu halisi. Kupitia Luka anatueleza hata jinsi ya utoto wa Yesu pale alipokuwa na umri wa miaka 12 ( Luka 2:41-42)
Ni jambo la muhimu sana kujifunza kwa Yesu,kwa maana maisha ya Yesu yalikuwa ni mafundisho tosha ya imani ya kweli. Tunapojifunza somo la imani basi hatuna budi kujifunza kwa Yesu jinsi alivyoishi.
Kwa nini tunajifunza haya yote.?
01) Tuweze kujua ya kwamba Yesu alikuwa ni Mungj na pia alikuwa mwanadamu.
02)Tukifahamu ya kuwa Yesu ni Mungu,tutabadili mtazamo wetu pale tuombapo. Kamwe hatutajua kwamba tunamuomba mwanadamu bali Mungu.
03)Tupate kujifunza kieleleze cha kumuishia Mungu. Kwa maana tunapomuangalia Yesu tutajifunza jinsi itupasavyo kuishi kiimani.
04) Ni vyema kila mkristo na watu wote watambue kwamba Yesu alikuwa ni zaidi ya mwanadamu.
Ni mimi mtumwa wa Bwana; Mchungaji G.Madumla. Kwa huduma ya maombezi piga sasa +255 683 877 900
What’s app +255 746 446 446
Na Pst.Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comments