top of page

MUNGU AKIKUTUMA KAZI UJUE ATAKUPA NA MAELEKEZO SAHIHI.


IMG_20140730_165407

Moja ya mikutano ya injili vijijini niliyoifanya pamoja watumishi wa Mungu,hapa ni Tanga.


Ukweli ni kwamba Mungu anafanyakazi pamoja nasi hata sasa ( 2 Wakorintho 5:21). Amekuchagua ili ufanye kazi pamoja naye,lakini angeliweza kufanya kazi zote yeye mwenyewe bila uwepo wako. Hata hivyo ni utaratibu alioweka ili tumtegemee Yeye. Fundisho hili ni fundisho maalumu haswa kwa wale wanaotamani kumtumikia Mungu kikamilifu lakini hawajui waanzaje na wamalizaje.. 

Jaribu kupata picha ya baba anapomtuma mwanaye. Kitu gani baba atafanya kwa mwanaye? Bila shaka,atampatia maelekezo yote akihakikisha mtoto anaelewa vizuri,kisha na atampatia vitendea kazi kama vinavyohitajika,kisha atajaribu kumsimamia ili kuona kama anakwenda vyema au la. Endapo baba atakapogundua kwamba mwanaye afanyi kama alivyomwelekeza,kwa sababu ya pendo atamwelekeza tena na kumsaidia zaidi na hatimaye mtoto atajikuta amefanya vyema zaidi. 

Na ndivyo ilivyo kwa Baba yetu wa mbinguni. Ambaye kazi akukupa kazi yoyote uifanye,labda kazi ya kufungua huduma,kazi ya injili,kazi ya uimbaji basi uwe na uhakika atakuongoza vyema na hatimaye utamwona Bwana. Hivyo; leo tuangazie kazi ya kufungua huduma zaidi kuliko kazi nyingine. Na hapa pana mfano mzuri wa Nuhu,ingawa Nuhu hakufungua huduma kama huduma/ kanisa lakini kuna kazi fulani aliambiwa afanye,nayo ni kazi ya “ kutengeneza safina”

“14 Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami.22 Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya. ” Mwanzo 6:14,22

(Ukipata nafasi usome Mwanzo 6 yote.) Maandiko hayo hapo juu ni sehemu ndogo ya kile Mungu alichoanza kumwelekeza Nuhu kuhusu ujenzi wa safina lakini katika mstari wa 22 tunaona Nuhu “akafanya sawa sawa na vyote alivyomwamuru Mungu..” . Mungu alihakikisha anampatia Nuhu maelekezo muhimu yote ya namna safina itakavyokuwa,na pia kumsaidia . Ujenzi wa safina haukuwa ujenzi wa kawaida bali ulikuwa ni utengenezaji mkubwa sana kwa maana kwanza ulihitaji muda wa kutosha.

Utengenezaji uligharimu muda wa Miaka mia moja,usikivu wa hali yajuu,vifaa vingi kama miti n.k Hata hivyo hatujui kama Nuhu alijenga akishirikiana na watu au yeye peke yake,lakini kwa mujibu wa biblia,Nuhu pekee yake alijenga kwa msaada wa Bwana Mungu. 

  1. Utengenezaji wa Safina unatufundisha nini?

01. Maelekezo sahihi ya safina iweje yalitoka kwa Bwana.

Ikiwa Nuhu aliongozwa na Mungu hata akaanza kutengeneza safina,basi ni dhahiri Nuhu hakuwa na picha ya safina iweje isipokuwa Mungu aliifunua kwake,naye Nuhu akaingia kazini. Kwako,ikiwa unasikia mzigo wa kujenga nyumba ya Bwana / Kanisa, je umepata kusikia Mungu anasema nini? Kuna maelekezo gani ya Bwana? Kwa maana si nyumba yako bali ni ya Mungu. Uwe na uhakika Bwana kuwa amekupa maelekezo na kazi haitakuwa ngumu.

02. Uvumilivu.

Ndani ya miaka mia moja ya utengenezaji wa safina ni miaka mingi sana. Laiti Nuhu asingelikuwa mvumilivu,angeishia kati na kusema “ nimechoka” lakini Nuhu aliendelea kutengeza hata ikawa. Bila shaka Uvumilivu alikuwa nao. Wewe pia,lazima uwe na uvumilivu unapofanya huduma,unaweza ukawa unajenga kanisa sasa ni mwaka wa nne na bado kabisa,usichoke taratibu litaisha tu kwa kuwa Bwana mwenyewe atalisimamia. 

03. Imani.

Nuhu alikuwa na karama ya imani. Akiamini kuwa maelekezo yote asemayo Bwana yatatimia tu. Na siku moja gharika la mvua litashuka. Imani ni muhimu sana hususani kwako ambaye u mtumishi wa Mungu. Kuna mambo fulani hayawezi kutokea sasa aliyokuhadi Bwana Mungu, lakini baada ya muda yatakwenda kudhihilika. Hivyo,kuwa na imani katika kazi aliyokupa Bwana.

04. Usikivu mzuri.

Wengi leo wamefeli katika kukosa usikivu mzuri kwa kile walichopewa wafanye. Ikiwa kama umekosa umakini,usitegemee kuona udhihilisho wa nguvu za Mungu, kwa maana usikivu ni kitu muhimu sana. Fikiria Nuhu katika utengenezaji wa Safina, asingelikuwa makini kuelewa kwa usahihi juu ya aina za miti,vipimo mbali mbali,aina za madirisha,milango ya kuweka,kujua kiasi cha uzito stahiki wa safina, aina za maelekezo ya kuchukua wanyama,n.k. Hivi ingelikuwaje kama asingelikuwa makini kusikia? Mimi nafikiri ingelizama majini!!! Jiulize ni mambo mangapi Bwana Mungu amesema nawe lakini yanaingia sikio hili na kutokea sikio la pili pasipo hata kuelewa,halafu unajikuta upo pale pale??? Unahitaji usikivu wa hali ya juu.

05. Kumtegemea Bwana tu.

Nuhu hakuwa na ujuzi aliosomea wa kutengeneza masafina,bali alitegema kile alichokisikia kutoka kwa Bwana na hatimaye lifanikiwa. Kanisa unapoendesha,lazima umtegemee Kristo Yesu,Yeye ndiye kiongozi wa hilo kanisa / huduma. Kwa sababu wapo viongozi ambao huwategemea watu au hujitegemea wao wenyewe na mwisho wa siku wanafeli!!!

Hivyo,hayo ni machache niliyokuandikia kati ya mengi niliyonayo kuhusu namna stahiki ya huduma yako kwa Bwana. Tumemwangalia mtu mmoja tu Nuhu,lakini hata hivyo kuna wengi wa kujifunza kupitia wao. 

Ikiwa kama umebarikiwa nifahamishe,pia kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI nipigie kwa +255 683 877 900

Whats app namba .+255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page