MUDA AMBAO NUHU ALIUTUMIA KUKAA NDANI YA SAFINA
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 24, 2018
- 4 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Si watu wengi wanajua muda halisi alioutumia Nuhu ndani ya safina wakati gharika ilipokuwa juu ya nchi. Na kile kinachowafanya wengi wasijue ni kutokusoma neno na wakati mwingine kusoma bila uelewa. Nimekuwa nikijifunza kwa ukaribu juu ya Nuhu na safina kwa ujumla wake. Nikagundua habari za Nuhu zimeandikwa ili kutufunza mambo mengi katika imani tuliyonayo ndani ya Kristo Yesu
Moja kati ya jambo nililojifunza ni kwamba Nuhu alikuwa mwenye haki katikati ya waovu;hapo niliyaangalia maisha yetu ya leo na kuona jinsi tulivyozungukwa na uovu wa kila aina,lakini katikati ya waovu wa duniani hii bado waweza kuwa mwenye haki,inawezekana!. Ninapojifunza kwa Nuhu aliyepata neema machoni pa Bwana,nikamuona ni mtu aliyemtii,mwenye “ karama ya imani“, na mtu aliyewaambia watu wageuke lakini watu walikataa!
Ingawa biblia haituambii kwa mapana na marefu kuhusu habari za Nuhu na maisha yake ya kiimani,lakini Nuhu alikuwa na ushuhuda mkubwa sana,kwa sababu hakuwa mtu wa kawaida kawaida hivi! Na wala halikuwa jambo jepesi la yeye pekee na watu saba kuokoka na lile gharika,hii ina maana kuna namna fulani ya kipekee aliyokuwa nayo Nuhu. Mimi huwa najiuliza mwenyewe kwamba,ikiwa Mungu anaichungulia dunia ya leo,Je atamuona mtu kama Nuhu? Na Je watakuwa wangapi kiidadi? Hata hivyo ninajua wapo lakini ni wachache sana,lakini kiwango cha imani alichonacho Nuhu ni kiwango kikubwa sana! Ebu tujifunze pamoja sasa;
“ Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.” Mwanzo 7:6
Neno linatuambia muda ambao Nuhu alikuwa nao kipindi gharika inaanza,ni miaka 600. Ukiendelea kusoma hapo chini utaona mvua ikianza kunyesha kwa siku arobaini usiku na mchana.Maji hayakuwa ya kutoka juu tu,bali chemichemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu tena na madirisha ya mbinguni yakafunguka!(Mwanzo 7:11-12)
Sasa,ebu twende pamoja kuangalia muda halisi alioutumia Nuhu ndani ya safina kwa andiko lilo hapo juu (Mwanzo 7:6) kwa kulinganisha na andiko hili;
“ Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. ” Mwanzo 8:13-14
Utagundua kile tunachoanza kuelezwa ni kwamba;
Nuhu alikaa ndani ya safina kwa mwaka mmoja (Maana aliingia kwenye safina akiwa na umri wa miaka 600,tena ikaandikwa “ikawa mwaka wa 601” hivyo,huo ni mwaka mmoja. Ingawa biblia haituambii mwaka mmoja ulikuwa na siku ngapi kipindi kile,lakini sisi tunanajua mwaka mmoja wenye siku ndani yake)
Nuhu akaongeza “mwezi wa kwanza” ,hivyo nimeupa mwezi siku 30. Hapo uso wa nchi umekauka,lakini Nuhu hakutoka safinani,bali aliendelea kusubiri.
Nuhu akaongeza “ siku 27″ ya mwezi wa pili katika mwaka 601.
Hivyo,hesabu yake itakuwa ; mwaka mmoja+30+27=1.57. Hii ni sawa na kusema Nuhu alikaa ndani ya safina kwa mwaka mmoja na siku 57. ( Hivyo wengine husema siku 371 ikiwa na maana mwaka siku 300 na siku 57 + 14 za kutolewa kwa kunguru na njiwa)
Sasa hivi umeshawahi kujiuliza juu ya muda wote huo mtu kukaa ndani ya lichombo fulani kubwa lenye kuelea! Hivi,unajua ni muda mrefu sana huo? Lakini biblia haituambii kwamba Nuhu alimnungunikia Mungu labda asema kwa nini Mungu amemuacha muda wote huo.
Najiuliza kwamba,hivi angelikuwa mkristo wa leo ingelikuwa? Asingefanya maamuzi ya kutoka hata dirishani (maana mlangoni Mungu aliufunga Yeye mwenyewe Mungu) sababu Nuhu alikuwa na uwezo wa kufungua dirisha na ndio maana alifungua na kutoa kunguru na baadae alitoa njiwa! Hivi kweli kabisa ungelikuwa wewe na imani yako,ungeliweza kuwa kama Nuhu katika uvumilivu wa muda wote huo?
Tunajifunza nini katika hilo?
Mbali na kujua muda aliotumia Nuhu kukaa ndani ya safina,pia tunajifunza mambo yafuatayo;
01. Uvumilivu
Iwapo Mungu amesema kwako ujue atafanya tu,ikiwa amesema atakuokoa ujue atakuokoa tu,Yeye Mungu si mtu hata aseme uongo ( Hesabu 23:19). Sasa kwa nini unashindwa kuwa mvumilivu juu ya ahadi zake Bwana. Yeye ni Mungu yule yule aliyemkumbuka Nuhu katika uvumilivu wake Nuhu. Ukiwa ndani ya Yesu ni lazima uwe mvumilivu,ukivumilia na kusubiri wakati wa Bwana. Nuhu alikuwa ndani ya safina ni sawa na wewe ndani ya Yesu.
Lakini kuwa tu ndani ya Yesu haitoshi ikiwa kama utakosa uvumilivu. Jifunze uvumilivu huku ukiendelea kuomba,Mungu atakutoa tu kama Nuhu. Nuhu alikaa mwaka mmoja na zaidi,lakini alimuona Mungu zaidi,wewe je hupaswi kuvumilia kwa muda mrefu?
02. Kuisubiri sauti ya Mungu iseme nawe.
Muangalie Nuhu jinsi alivyoendelea kusubiri hata aisikie sauti ya Mungu ndipo alipotoka safinani. Ukisoma mstari wa 15 wa sura ya 8,Mungu anamwambia Nuhu “toka katika safina,wewe,na mkeo,na wanao,na wake za wanao pamoja nawe ” na hapo ndipo tunamuona Nuhu akitoka kama alivyoagizwa. Ni lazima ifike wakati ujue kuisubiri sauti ya Mungu iseme nawe juu ya maamuzi au mambo yako uyafanyayo. Mungu anasema nasi kwa njia nyingi sana,mfano kwa watumishi wake,ndoto,maono,kwa sauti,n.k
Wengi leo wameangamia kwa sababu hawakuweza kuisikia sauti ya Mungu nao wakafanya mambo yao wenyewe. EBU angalia hili kwa wale wana wawili wa Haruni Nadabu na Abihu waliouwawa kwa moto mbele za Bwana kwa sababu ya kutoa moto wa kigeni mbele ya Bwana,ambao Bwana hakuwaagiza,nao wakafa wote wawili ( Walawi 10:1-2). Jifunze kuwa msikivu sana,usubiri maelekezo muhimu ya Bwana katika hilo na katika maisha yako.
Kwa msaada zaidi na maombezi piga sasa kwa
+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE
Comments