top of page

MTU USIYEMJUA MWENYE KUTEMBEA NA WASAA WA HATMA YAKO – 01.


BE CAREFUL: A CERTAIN STRANGER YOU’LL MEET IS WALKING WITH YOUR DESTINY MOMENT

  1. [KUWA MAKINI: UTAKUTANA NA MTU AMBAYE HUKUWAHI KUMJUA ANAYETEMBEA NA WASAA WENYE HATMA YA MAISHA YAKO]

:::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::

Ni Jumatatu asubuhi mida ya saa tano. Hali ya hewa ni nzuri na tulivu; na licha ya jua kuwaka kwa nguvu, makali yake yanazuiwa na kivuli cha mti mkubwa ambao nimepumzika chini yake. Nimejilaza juu ya kibenchi kizuri cha mbao ambacho ni mahsusi kwa ajili ya abiria wanaosubiri kusafiri kwa gari moshi. Lakini leo gari moshi halipo na hivyo kuna utulivu sana tofauti kabisa na siku zenye safari za gari moshi zinavyokuwa hapa Stesheni ya Mwanza.Usingizi unaniijia kwa mbali hususan kwa sababu ya kile kiupepo cha asubuhi kinachovuma kwa kubembeleza. Lakini njaa inabishana na usingizi, hivyo nabaki katikati ya kuwa macho na kusinzia. Mbavu zinaumia kwa kulala juu ya mbao lakini ninaona bora kuvumilia maumivu ya mbao kuliko kukaa na kubakia macho kitu ambacho kitanifanya nianze kutafakari changamoto za maisha zilizonokuta mpaka kufikia wakati huu:

Nimemaliza kidato cha nne Makoko Seminari Musoma kwa kusoma kwa shida na kulipiwa ada kwa msaada wa mwalimu kutoka kidato cha pili hadi cha nne baada ya mzazi wangu kushindwa kulipa ada. Nimesoma sehemu kubwa ya kidato cha nne nikivaa shati moja suruali moja na kandambili nyekundu kabla ya mkuu wa shule kuingilia kati na kuhakikisha napata jozi ya viatu kama wengine angalau nifanye mitihani ya mwisho nikiwa na mindset iliyotulia. Nimerejea nyumbani baada ya kumaliza mitihani ya NECTA kwa “lift” tena kwa bahati kwa sababu ya kukosa nauli ya kurejea nyumbani. Nimefika nyumbani Ukerewe hali ni ngumu zaidi na hivyo naanza kujibidiisha na vibarua ili kusaidia familia na kujikimu kama kijana. Nimefanya vibarua migahawani na kukosa malipo kwa miezi kadhaa na hatimaye kuacha na kuanza kujiajiri kama machinga. Nimefanya umachinga na kupoteza pesa na kupata hasara. Matokeo yametoka nina ufaulu mzuri na nimechaguliwa kwenda Tabora Boys.

Lakini bado sina uwezo hata wa kumsaidia mzazi wala kujikimu. Ninaona kupambana kwenda shule ni kama kukimbia hali ngumu ya nyumbani au kumkimbia mzazi. Nitamsaidia kwanza mzazi shule nitaendelea tu mbeleni. Wenzangu wanaenda shule. Mimi napambana na umachinga. Inaniuma lakini ninaamua kuvumilia. Hatimaye naweza kusaidia familia na kujikimu kidogo. Napata pesa kidogo ya ziada namuaga mama namwambia naenda Mwanza mjini “KUTAFUTA” maisha kidogo ili nimsaidie zaidi kisha nitaenda shule asihofu. Anakubali maana ukweli hana cha kufanya. Sina nauli ya kupanda “meli” maana pesa zaidi nimemwachia mama. Ninapanda boti za uvuvi na kufika Mwanza kwa kukosakosa kuzama ziwani. Hii safari sitoisahau. And now niko Mwanza. Naanza kutafuta pa kufikia. Hakuna. Naanza kutafuta connection za ndugu wa mbaali nabahatika kukaa kwa muda lakini baadaye nalazimika kuhamia kwao na mtu tuliyesoma wote kwao Nyakato. Wazazi wake hawajawahi kunisikia. Anawaeleza nimetoka wapi na kuwaeleza hali yangu wanakubali kwa shingo upande. Kumbuka hawanijui. Na dunia ya leo mambo ni mengi. Wanaogopa nikipata matatizo itakuwaje. Wanakubali niwe naenda kulala tu. Baada ya muda rafiki yangu huyo analazimika kunipa connection kwa “masela” mtaani ili kuepusha changamoto na wazazi.

Naanza kuishi na “masela”. Natoka Nyakato kwenda mjini kwa mguu daily ili kutafuta vibarua. Nimezunguka maduka ya wahindi. Nimezunguka karakana na supermarkets na migahawani. Kinachoniletea shida ni mwili mdogo. Naonekana katoto kumbe nimemaliza kidato cha nne. Wanajua nimemaliza STD VII hivyo wanaogopa mkono wa serikali ajira za watoto😂.

Hivyo Jumatatu hii nimekuja Railway stesheni nipumzike kupoza uchovu wa kuzunguka kwenye maduka na kuambiwa HAKUNA KAZI. Ndiyo maana nalazimisha kulala ili nisikae macho nikaanza kukumbuka hayo yote. Nimekuwa nikija kupumzika hapo mara kwa mara nikiwa nimechoka au nikisubiri jua lipungue nianze kupiga mguu kurudi Nyakato.So back kwenye kibenchi. Nipo hapa sasa. Njaa, uchovu na usingizi vinashindana. Nani ataibuka kidedea? Naona kama usingizi unaanza kushinda. Huooo unakuja. Kama hauji. Kama unakuja. Naanza kusinzia…..

Ghafla naamshwa na sauti ya mtu nisiyemfahamu karibu na nilipojilaza:

“DOGO HUJAMBO?”

Nashtuka sana. Mpaka anajua nimeshtuka. Moyoni nakasirika kweli. Usingizi wangu umepotea! Halafu huyu nani. Huku nimekuwa irritated. Huku naogopa. Au askari?! Maana mimi siyo abiria wala leo siyo siku ya treni. Sijui cha kujibu:

“Shikamoo kaka!”

“Marahaba mdogo wangu! Haujambo?”

Anazungumza kiswahili kizuri sana, lakini lafudhi ya Kisukuma naisikia. Ila sauti yake ni ya upole uliochanganyika na huruma hivi kama upendo hivi. So calm. Amevaa vizuri sana kama afisa fulani wa serikali. Very smart. Mimi nimechoka mwili, roho, akili hadi mavazi.

Kiukweli bado nimekereka kwa ndani alivyonikatisha usingizi natamani niondoke pale. Lakini kuna kitu moyoni kinaniambia kwa nguvu:.


MSIKILIZE MTU HUYU. DON’T RUN AWAY FROM HIM. DON’T GET ANNOYED.

Woga unaondoka. Na ameongea kwa sauti ya upole sijapata kuona. Neno sahihi ni COMPASSIONATE. Ulishaona mtu anakusemesha kwa huruma? Sijui ni nini lakini moyo wangu unazidisha mapigo yake…. si kwa kuashiria hatari bali kwa kuashiria kuwa kuna kitu si cha kawaida kwa mimi kukutana na mtu huyu:

“Sijambo”

Namjibu nikiwa sasa natamani kujua anataka kuuliza nini. Anakaa kwenye kibenchi. Ninasogea pembeni zaidi kama unavyoweka “space” unapokaa ma mtu. Ghafla anauliza maswali mfululizo na majibu yangu yanakuwa ya mkato mkato tu ili amalize aondoke.

“Unakaa wapi?” “Nyakato” “Unakaa na nani?” “Kwa rafiki yangu” ndo jibu lililokuja “Umemaliza darasa la saba?” “Form Four”

Ndani kuna kitu kinaniambia “TRUST THIS MAN ANDREA” Na moyo unakubali maana moyo unasema mtu gani anaongea kwa UPOLE hivi kama malaika Gabriel? Kuna kitu kwa huyu mtu sijui nini lakini kipo kitu chema.

ITAENDELEA…

Ikiwa umebarikiwa,tufahamishe ili tumtukuze Mungu pamoja na kwa msaada zaidi wasiliana sasa kwa;

Semper Fidelis,

Andrea G. Muhozya Entrepreneur & Business Trainer Dar es Salaam, Tanzania East Africa +255 788 366 511. :::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page