MTAZAMO WA MAVAZI KWA WALIO-OKOKA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 13, 2017
- 4 min read

Mch.G.Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Kati ya mambo magumu ya kimjadala ni jambo la mavazi. Kwa maana suala zima la mavazi limeegemea sana katika “mila na utamaduni” na hapo ndipo ugumu unapojitokeza,kwa sababu kila mmoja ana utamaduni wake tofauti na mwingine. Mfano,Utamaduni wa nchi za magharibi(Ulaya),ni tofauti na utamaduni wa Kiafrika. Huko Ulaya sio ishu kwa mwanamke aliyeokoka,au hata wachungaji wanawake kuvaa suruali au kuvaa nguo fupi,ni moja ya utamaduni tu!
Lakini hata wanaume waliookoka wa nchi za magharibi kwao sio ishu kubwa kuvaa hereni au kusuka,wakati mwingine kujichora tatoo au kufanya ibada wakiwa wamevaa kofia tena wakiwa wamezigeuza mbele-nyuma,au kuvaa “suruali modo” n.k Lakini mavazi hayo hayo ukiyaleta kwetu Afrika hasa kwa watumishi wa Mungu ni ishu kubwa! Ebu fikiria hivi,ikiwa wewe ndio mchungaji mwanamke hapa Tanzania,
halafu umevaa suruali imebana mpaka nguo ya ndani inaonekana,au umevaa nguo fupi kiasi kwamba ukiinama inakuwa ni shidaaa!!!!,hivi unajua watu hawatakuelewa hata kidogo!!!! Au fikiria wewe ni mwanaume mtumishi (labda ni mchungaji),halafu,umesuka,au umevaa hereni,umejichora tatoo,hivi utaeleweka kweli? Kwa kweli nakwambia itakuwa ni shida!
Lakini hapo umeona,yaani mavazi yale yale waliyoyavaa wenzetu wa ulaya na kueleweka katika huduma zao,lakini huku kwetu hayaeleweki hayo,kwetu sisi ni uhuni mtupu! Kinachosumbua hapo ni suala zima la “utamaduni” unaotofautiana. Utamaduni ukipishana tu,basi ujue mtazamo utatofautiana kabisa,tena kila mmoja katika upande wake atajiona yupo sahihi kuliko mwenzake!!!
Yaani wewe Mwafrika utajiona uko sawa kabisa na uko sahihi kwa suala la mavazi,ila na mwenzako ambaye ni kutoka Ulaya atajiona yupo sawa ,sahihi kuliko wewe! Sasa nani yupo sahihi kati ya hawa wawili?,Kwa kweli ni mtihani huo usiokuwa na majibu kwa sababu ya suala la kutofautiana kwa mila na utamaduni
Lakini ifike wakati tuangalie Neno la Mungu linasema nini juu ya mavazi
Katika agano la kale,Bwana Mungu aliwataka wanawake wavae mavazi yao,na wanaume pia wavae mavazi yao ( Kumb.22:5). Lakini unafikiria kwa nini Mungu aliwazuia wanaume kuvaa mavazi ya kike,? na kwa nini aliwazuia Wanawake kuvaa mavazi ya kiume? Kulikuwa na hatari au shida gani ambayo Mungu alikuwa anaiona? Unaweza ukajiuliza maswali kama hayo.
Lakini,nataka ujue hili,mpaka Bwana Mungu anakataza hivyo,alikuwa anajua kwamba kuna mwingiliano wa mavazi,na kuona baadhi ya wanaume wanakimbilia mavazi ya kike na kuyavaa na baadhi ya wanawake nao wanaacha mavazi yao wanatafuta mavazi ya kiume. Lakini kwani kuna ishu gani hapo iliyojificha?
Moja ya siri kubwa iliyojificha hapo ni kwamba,Bwana Mungu alitaka wanaume wote wabaki na utambulisho wao wa kiume,(Yaani isitokee mwanaume hata mmoja akaonekana kama mwanamke ). Pia aliwataka wanawake wote wabakie katika utambulisho wao,kwamba mavazi yao yawatambulishe ( Asitokee mwanamke yeyote atakayeonekana kama mwanaume). Hii yote ni kuleta heshima ya kijinsia,yaani kila mmoja atambue jinsia yake kulingana na mavazi pia aweze kutambua jinsia ya mwenzake na kuiheshimu. Kumbuka hapo; Suala halikuwa uvaaji wa suruali wala sketi,bali suala ni kila mmoja abakie katika utambulisho wake.
( Unajua historia ya mavazi hubadilika katika kila zama mfano kuna zama zilizopita ambazo wanawake walikuwa wakivaa suruali pana kwa ajili ya kujistili vizuri,na wanaume ambao waliokuwa askari wa Kirumi walivaa sketi kama vazi la heshima. Zama zilipoendelea wanawake wakavaa sketi,wanaume suruali. ) Shida inatokea pale mwanaume kuvaa kama mwanamke na kupoteza utambulisho wake wa kiume. Mwanamke naye kuvaa kama mwanaume naye kupoteza utambulisho wake.
Uzuri mmoja ni kwamba kila utamaduni una namna ya kumwelezea mwanaume aonekanaje kimavazi,na mwanamke pia anapaswa atambuliweje. Kwetu afrika,utamaduni wetu unamtambua mwanaume/mwanamke kwa mavazi fulani na mtindo wa mwonekano wake,alikadhalika hata Ulaya mwanaume/mwanamke naye hutambuliwa kwa namna yake kama utamaduni ulivyo.
Sasa ikitokea mwanaume akavaa au akaweka mtindo wa kike kinyume na utamaduni wake hali anaishi ndani ya huo utamaduni,hapo atakuwa amekosea na hataelekeka kanisani hata nje ya kanisa. (Mfano mwanaume aliyesuka kwa utamaduni wetu Tanzania,hiyo ni shida tayari!) Biblia inakutaka uweze kujiheshimu kimavazi,;
ukiona umevaa nguo au umepiga mtindo fulani hafalu mara ukakosa Amani moyoni mwako kwa sababu ya kile ulichokivaa. Basi ujue hapo haupo sawa ,umekosea kuvaa,nenda kavue maana hautaeleweka kabisa! Kumbuka mavazi ni moja ya jambo muhimu sana katika utumishi wako. Wakati mwingine unaweza usieleweke kabisa hata kama ni mtumishi wa Mungu,kwa sababu tu ya mavazi yako uyavaayo,kwa maana mavazi yana sehemu kubwa sana katika utumishi wako.
Kwa sehemu kubwa mavazi yameathili huduma zetu,hata kuchochea roho ya uzinzi na uhuni makanisani /kwenye fellowship/majumbani na mitaani. Mfano ulio hai,tuanze tu kwa kumwangalia mwanaume aliyeokoka,ambaye amevaa vizuri kabisa ila kifuni kwake kafungua vifungo vya shati lake na kifua chake kwa sehemu kinaonekana,nywele za kifuani zinaonekana pia cheni yake shingoni inaonekana.
Sasa kwa hilo tu,ni shida kwa wadada/wanawake wachanga kiroho. Kwa maana wanaweza wakavutiwa na garden/nywele za kifuani au cheni,hatimaye wakahama kiufahamu na mara wakamtamani kimapenzi huyo mtumishi.
Na kwa Wanawake ndio mbaya zaidi katika uvaaji. Wewe ni shahidi namna ile baadhi ya wanawake wanavyovaa tena wakiwa kwenye ibada,wengine uvaa suruali za kulalia zile laini zilizobana sana yaani hata akitembea jamani!!!! huwezi hata kumwangalia,wengine sketi fupi kiasi kwamba hata hawawezi kuinama maana ni aibu, kiasi kwamba hata wanawake wenzake wanakosa amani,basi hapo ni rahisi sana kumshawishi mwanaume,ni kama vile kupromoti uzinzi na uasherati.
Neno la Mungu linatutaka sote tusifuatishe namna ya dunia hii,namna hata ya uvaaji anasema; Hivyo kuwa mwangalifu sana na uvaaji wako,kwa maana kuna sehemu unaweza usipokelewe kabisa,au unaweza ukapokelewa sivyo ndivyo kwa sababu tu ya mavazi yako!
“ Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Warumi 12:2
Tuwasiliane kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,au ikiwa kama kuna kitu umekipata. UBARIKIWE
Na Mch.G.Madumla.
Kwa huduma ya maombezi piga +255 683 877 900.
What’s app number ni+255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments