MTAZAMO WA KIROHO KUHUSU UMASKINI.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 17, 2018
- 5 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufipi.
Familia nyingi za kiafrika (na sehemu nyingine duniani) ni maskini hata mimi nimetokea kwenye familia ya kimaskini. Sijui wewe mwenzangu? Lakini bila shaka umaskini umechukua nafasi kubwa kwenye jamii zetu. Hivyo ni vyema leo tukajifunza kuhusu “ umaskini” kwa mtazamo wa kiroho. Ulishawahi kujiuliza kwa nini ulizaliwa na wazazi walio maskini? Au kwa nini wewe sasa ni maskini tena maskini wa kutupa! Je unafikiri uliumbiwa umaskini? Biblia inasemaje?
“ Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;)“ Kumb.15:4
Mtazamo mkubwa wa kiroho na wa kwanza ndio huu; “Mungu hakukusudia watu wake wawe maskini, bali wawe na maisha ya utele sawa sawa na baraka watakazopokea” maana katika andiko hilo,BWANA anasema “atakubarikia kweli..” hii ni sawa na kusema hukuumbwa kuwa maskini. Kumbuka,Bwana anawaambia ;
“ watu wake,watoto wake” Kuonesha kwamba wale wote watakaokuwa wa Bwana, hawajawekewa kitu kiitwacho umaskini. Sasa ikiwa watashindwa kumwishia Bwana, umasikini na fedheha ni sehemu yao ( Mithali 13:18). Na hapo ndipo aliposema
“ Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.“ Kumb. 15:11
Je umaskini ni nini basi?
Katika agano la kale,kwa mara ya kwanza neno “umaskini / poverty” linatajwa,kwa makusudi kabisa,ili kwanza kueleza maana ya umaskini na andiko lenyewe ni Mwanzo 45:11.
Kumbuka hili; miaka saba ya njaa ilipokuwa ikiwanyemelea wamisri wote kwenye uongozi wa Yusufu kama waziri mkuu. Wamisri wote waliingia kwenye hali ya “uhitaji” wa chakula. Neno “uhitaji” kama lilivyotumika kwa mara ya kwanza kwenye Mwanzo 45:11 lina maana ya “ umaskini / poverty “. Hivyo umaskini ni uhitaji wa chakula,mafavazi au malazi,pia umaskini ni hali ya kupungukiwa yale mahitaji muhimu sana. Na ndio maana ukisikia “mtu huyu ni maskini” basi ujue maana yake “mtu huyu ni mhitaji,amepungukiwa sana”
Kitabu cha Mithali ni kitabu cha kipekee kilichoeleza habari za umaskini sana kulinganisha na vitabu vingine,kwa maana takribani maandiko 13 ya kitabu cha Mithali kinaeleza umaskini na hapo ikiwa kwenye agano jipya umaskini umetajwa kwenye maandiko matatu tu ( 2 Wakorintho 8:2,8:9 na Ufunuo 2:9.) Kumbuka neno “umaskini,na sio maskini “ neno umaskini ndio hiyo takwimu yake.
Kumbuka mtazamo wa kiroho huu;
Mungu hakukusudia uwe na umaskini,bali uwe na maisha ya utele.
Tunaposema “maisha ya utele ” tuna maana maisha ya utoshelevu. Si lazima uwe na magari n majumba au maghorofa,ndio uwe na maisha ya utele,kwa maana maisha ya utele ni maisha ya kuridhika,ya kuwa na pesa zisizo za mawazo. Ni maisha ya utulivu kiuchumi. Tafsiri ya utele haipo kwenye magari wala maviwanja,majumba bali kwenye amani na utulivu katika hali ya utoshelevu. Jichunguze,je unayo hayo maisha?
Je ni nini kinachosababisha uwe maskini.?
01. Sababu za kiroho.
Zipo roho za kufisha katika kila unachofanya. Unapotaka kuinuka kiuchumi na unajikuta unarudi nyuma au upo pale pale. Mfano hai; kuna watu ambao hata wakipewa mtaji leo,ujue mtaji huo utakufa ndani ya miezi mitatu tu,na ukijaribu kumwuliza kafanyia nini,ujue hutapata majibu ya kueleweka. Na ukimwambia ajaribu kubalansi matumizi yake,basi ujue ukweli atabalansi vizuri,lakink pesa haionekaniki!!!! Ujue hapo sio tatizo la kawaida hilo,ni la kiroho.
Hujawai kuona mtu kila kishika kitu ni lazima kiharibike? Hata ungelimpa gari,basi ujue gari litagongwa au kugonga tu. Hiyo ni roho ya umaskini. Wale wenye kujua nini ninasema hapa watakubaliana na mimi, kwa maana nimeshuhudia mengi jinsi ambayo shetani anavyocheza na mind set za watu,kwa leo la kuwatupa kwenye ufukara.
02.Kodi,rehani na mikopo isiyokuwa na malengo. ( Nehemia 5:1-5)
Nehemia anaeleza siri kubwa sana,iliyowakamata watu wa kipindi kile,ambao walilia kwa umaskini wao uliokithili. Soma hilo andiko,utaona maskini wakilia kwa sababu hawana kitu,na wanahitaji japo chakula wale tu,wasije wakafa kwa sababu walikopa,wakaweka na rehani mashamba yao. Sasa angalia hapo, hata watoto wao waliingizwa kwenye utumwa ambao hawakuustahili kabisa.
Jiulize leo; ni watu wangapi walioingizwa kwenye utumwa kwa sababu ya mikopo ya wazazi wao ambao leo maskini hawapo duniani hao wazee? Au jiulize ni wangapi leo ni watumwa wa madeni ? kiasi kwamba ni maskini tu,maana hawana kitu. Jihoji sasa.
03. Kukataa maarifa ya kiungu. ( Mithali 13:18)
Biblia inasema tena “Bwana ndiye mchungaji wangu,sitapungukiwa na kitu…” Zab.23:1. Yaani ni sawa na kusema yeyote atakayeongozwa kikamilifu na Bwana, kamwe hawezi kupungukiwa na kitu. Ndio,na ndio ukweli wenyewe. Sasa wapo watu waliomkataa,na kukataa kuchungwa na Bwana, lah! Kama wamekubali basi wanaigiza igiza,sasa watu wa namna hii,lazima waingie katika uhitaji / umaskini.
04. Uvivu na uzembe.
Kuna watu kabisa wanastahili kuwa maskini,kwa sababu ni wavivu kupindukia!!! Wenyewe hawataki kujishughulisha kabisa,bali wanataka wale tu na kulala. (Cheki kile ambacho biblia kinasema – Mithali 20:13,28:19). Utagundua kwamba,kumbe kwa sehemu umaskini unachangiwa na uvivu tulionao. Nataka niweke wazi leo hapa;
Walokole tunashida sana katika eneo hili kwa maana wapo watu ambao hawataki kufanya kazi kabisa, wakati wote wapo tu kanisani wakijidanganya nafsi zao kwamba Mungu atafungua milango,sasa milango itafunguliwa,lakini ni lazima uwe na bidii katika kazi.Watu wa duniani kwa kweli wanatushinda kwa kuwajibika na katika tunawaona wakifanikiwa.
05. Kanisa kusahau wajibu wa kufundisha vijana mambo ya uchumi.
Kanisa la leo kwa sehemu kubwa limeacha wajibu wa kuwekeza nguvu kwa vijana katika nyanja ya uchumi. Utakuta kijana amepewa neema ya kuwa mwalimu mzuri wa kwaya / praise lakini kanisa ni kama vile halimwoni. Sasa mwisho wa siku dunia inamwita aende kuitumikia kwa kazi ile ile ya musiki kwa kuwa dunia itamlipa.
Vile ilivyotakiwa ni kwamba kanisa liweke utaratibu wa kuwasaidia vijana katika mambo ya kiuchumi hata kuwalipia ada,kuwapa allowances ili wasije wakaitwa na dunia. Sasa ikiwa kanisa limesahau kuwekeza kwa vijana basi ni dhahiri hali ya uchumi ya vijana wa kanisa itakuwa si nzuri. Ni vyema kanisa liwekeze kiroho kuwaombea na pia kuwatafutia kazi vijana.
Mfano ; kwenye kanisa wapo watu mbali mbali kikazi,sasa vijana waliokosa kazi watafutiwe humo humo ili umaskini usitajwe kanisani na kwa vijana. Lakini leo ni ajabu,kwa wamama,wala si kwa wababa wenye kazi maofisini utakuta wakiwatafuta watu wengine tena watu wa duniani hali wakijiu watoto wa mzee mwenzao wamemaliza chuo na hawana kazi. Lakini pia kanisa limeegama kwenye eneo moja tu la mafundisho ya kiroho,na kusahau mafundisho ya kiuchumi pamoja na biashara ili watoto wa Mungu watafute maarifa hayo ndani ya kanisa na wala sio nje.Tubadilike kwa kweli!!!
Nini kifanyike sasa?
Kumbuka, neno hili “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.“ 2 Wakorintho 8:9
Yesu alibeba umaskini pale msalabani na kukuachia utajiri,lakini hali hii haiji mpaka uamini kwanza. Kisha ukishaamini tambua kwamba kila roho ya umaskini si mali yako na ni lazima ivuliwe kama mtu avuavyo vazi. Ni kwa njia ya maombi maalumu hata unaweza kujitenga mbali na umaskini kwako,kwenye familia au kwenye ukoo pia.
Ikiwa fundisho hili limekubariki,basi ningependa kusikia kutoka kwako kwa kuniandikia msg au kunipigia kwa namba zangu zilizopo hapo juu. Pia kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,waweza kunipigia sasa.
Kwa mawasiliano ya maombi na maombezi,ushauri na mengineyo piga kwa +255 683 877 900
Na mch. Gasper Madumla.
What’s app ni+255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comentários