top of page

MTAZAMO WA KIROHO KUHUSU MADENI.

Updated: Sep 2, 2022

Na Mch Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…


Mojawapo ya kilio kikubwa katika siku hizi,ni kilio cha watu waliao kuhusu wimbi kubwa la madeni wanayodaiwa na hajui watayalipaje hayo madeni. Na bahati mbaya kati ya waliao ni wapendwa katika Bwana ambao walikopa nje ya ufahamu wowote wa kiroho kuhusu madeni. Sijui wewe unayesoma ujumbe huu hivi sasa kama umepona kwenye ili eneo! Na bahati mbaya kanisa la leo limeingiza mambo haya ya kukopa na kukopeshana kinyume na maarifa ya Kiungu,


na hatimaye kanisa likajipata kupoteza washirika wengi maana ni dhahiri kabisa ikiwa mshirika anayedaiwa na pesa hana kukimbia kanisa kwa kigezo cha kudaiwa na washiriki wenzake. Je huu ndio mpango wa Mungu kwenye kanisa lake? Hivyo ni vyema tuanze kutafakari pamoja tukijiuliza kwanza nini hasa maana ya “deni (debt)”


Deni ni fedha au mali iliyokopwa kwa dhumuni kubwa la kurejeshwa pamoja na riba. Kumbe unapozungumzia “deni” utakuwa ukizungumzia mambo matatu “fedha,mali na riba” Riba ni faida ya mkopeshaji,mfano mtu anakukopesha tshs 200,000/= na anataka arudishiwe 230,000/= mwisho wa mwezi,hivyo tshs 30,000/= ni faida / riba ya mkopeshaji.


  Na kwa sababu kuna faida inayopatikana kwenye suala la kukopa basi sasa imekuwa ni biashara (commercial issue with interest) na kupelekea  watu wengi kujihusisha na biashara hii hata serikali kuwapa dhamana watu wa namna hii,kwamba wafanye kwa mujibu wa sheria.


Na sasa ndipo tunaona wimbi la vikundi vya kukopa na kukopeshana hususani wakina mama mitaani. Kitu kikubwa cha ajabu wanaoshikiria hizo hatamu za kukopesha ni watu wasio mjua Mungu / watu wa imani nyingine / wasiookoka ! Sasa hapo ni lazima ushtuke kidogo,maana pesa hizo zinazokopeshwa kwa misingi ya imani ipi? Na ndio maana leo ni vyema ukajua haya mambo ya mikopo kiroho. Ikiwa umefanikiwa kuona jambo hili kwa ukaribu,utagundua kwamba kuna hila za adui kuwafunga watu.



 Mfano,unaweza ukaona kikundi cha waliokopeshwa wamekusanyika kuleta marejesho yao,wakiwa watu kama 10 hivi,na na huo muda uliopangwa au kupangiana ni muda wa ibada kwa mtu wa Mungu ambaye na yeye ni mmoja wa wanakikundi. Hivyo itamlazimu kwanza  awajibike kwenda kwenye kikundi kwanza,au la basi aanze kumtafuta mwenyekiti wa kikundi alafu ndipo aende kanisani,Je hapo Mungu amepewa nafasi ya ngapi? ,Na je mkopo umepewa nafasi ya ngapi? Jibu ni jepesi tu,kwamba Mungu atakuwa amepewa nafasi ya pili au mwisho maana anayedaiwa ameanzia kwanza katika kikundi mpaka kimeeleweka ndipo aende kanisani,Je si utumwa huo?


Je sheria ya agano la kale ilikuwa ikisema nini kuhusu kukopa?

Sheria iliwataka waisraeli wote wasimkopeshe mtu aliye maskini tena wao wao wasikopeshane kwa riba ikiwa kama watakubaliana. Bali masikini wasaidiwe kama kwa Bwana-( Kutoka 22:25-27,Kumb 23:19-20). Ingawa ilikuwa ni sheria kipindi hicho lakini hata wakati huu wa agano jipya,Yesu naye husisitiza kuwasaidia watu maskini haswa wale walio katika Bwana,na wengine bila deni kuwapo (Mathayo 5:42).


Ifike wakati ujenge tabia ya kusaidia muhitaji. Ebu fikiri kuna faida gani utakayoipata ikiwa utamsaidia ndugu katika Bwana kwa kumkopesha hali unamjua kwamba hajiwezi? Ukweli ni kwamba unapomuangalia ndugu yako ambaye kwa kweli ni muhitaji basi usifikirie kurudishiwa kitu,bali kama unaamua kumsaidia basi msaidie tu,fanya kama kwa Bwana,na hapo utabarikiwa. Hivyo Mungu aliwataka Israeli wasikopeshane bali wasaidiane kama ndugu katika Bwana. La kama wanakopeshana basi wasimkopeshe maskini wala wasiweke riba.


Riba ilitoka wapi katika mikopo?


Waisraeli walipochangamana na mataifa,ndipo ilipowalazimu kukopeshana kwa riba. Hivyo suala la kukopa likachukua sura nyingine,badala ya kuwa katika lengo la kusaidiana likageuka na kuwa suala la kibiashara ( commercial issue). Na hapo biashara ilipoanza,tunaona mama wa mtumishi akisumbuliwa na deni la marehemu mumewe mtumishi wa Mungu. 


 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” 2 Wafalme 4:1


Andiko hili ni moja kati ya maandiko yanayoonesha kwamba kumbe hata watumishi wa Mungu wanasumbuliwa na suala la madeni kwa sababu aliyekopa ni mtumishi wa Mungu ingawa alikuwa amekufa. Kufa kwa mtumishi huyu hakukufuta deni alilokuwa akidawa enzi ya.uhai wake bali yeye alikufa,deni lilikuwa hai. Inatuonesha kwamba wapo watumishi wa Mungu ambao wanasumbuliwa na madeni au deni na hawajui watoke vipi na bahati mbaya wakifa deni halifi. Ikiwa ndivyo basi unatakiwa utazame madeni kwenye mtazamo wa kiroho kwamba “madeni ni roho hayafagi hata kama anayedaiwa amekufa,ila kufa kwa deni ni kulipwa.”


Mwanamke huyu mke wa nabii mumewe nabii alifariki akiwa amemuachia watoto wawili wa kiume,wafulana pamoja na deni aliachiwa. Ingawa biblia haituambii ni kiasi gani mumewe alikuwa akidaiwa,lakini hata hivyo inaonesha wazi kwamba mwanamke huyu hakuwa na uwezo wa kulipa deni hilo. Ikambidi amlilie Elisha mtumishi wa Mungu,maana hana msaada popote pale. Biblia haituambii kwamba alienda kwa waganga wa kiejeji bali kwa mtu wa Mungu.


Kumbe hakuna ufumbuzi wowote utakaoupata unapokimbilia kwa waganga isipokuwa kwa Mungu tu. Haijalishi ni kiasi gani unadaiwa bado msaada wako ni kwa Mungu!

“ mwanamke akamlilia Elisha” kilichomfanya alie sio upako wa Mungu kwa mtumishi wake. Bali uchungu na hali ya sintofahamu ya kulipa hilo deni maana anayemdai amefika na anataka pesa / mali yake ilipwe aondoke zake.


Hivi unajua ni mazingira magumu sana aliyokuwa nayo huyu mjane! Kumbe tunajifunza wengi leo wanalia mbele za Bwana sio wanalia kwamba upako umeshuka hapana! Bali wanalia kwa sababu ya kukamatwa na madeni na hawajui wafanyeje maana wanaowadai wanataka pesa zao. Jiulize je huu ndio mpango wa Mungu? Ni kweli tunapaswa tumlilie Mungu katika mambo yetu yote,lakini Je kulia huku kunaashiria ibada katika roho na kweli au kwa sababu ya uchungu? 

Kwa sababu ya madeni kufikia hapa ndipo tunaona kwamba;


  1. Madeni ni roho ya utumwa kwako-Mithali 22:7

  2. Madeni kiroho yanakunyima nafasi ya ibada-2 Wafalme 4:1

  3. Madeni kiroho yanakufanya uwe ni mtu wa kulia kila wakati -2 Wafalme 6:5 ( Mtumishi wa Mungu alianzima chuma cha shoka,na kilipopotea “ akalia” akifikiria kwamba si cha kwake,maada amekikopa atasemaje huko wakati wa kurudi kwake)


Je nini mpango wa Mungu?


  1. Kukubariki na kukupa nguvu ya kutawala ili kusudi ukopeshe na sio kukopesha. – Kumbukumbu 15:6

  2. Uwe na maarifa sahihi ya ki-Mungu ili unapotaka kukopa,upate faida,hivyo anakufundisha upate faida – Isaya 48:17


Je kukopa ni dhambi kibiblia?


Biblia haizungumzii kwamba kukopa ni dhambi,bali biblia inakutaka wewe ndiwe ukopeshe mataifa,uitawale pesa wala pesa isikutawale wewe. Kitu kibaya ni kujiingiza kwenye madeni kinyume na ufahamu wowote,maana ikiwa ni hivyo basi ujue utifika wakati fulani utalia tu kama waliaovyo wengine. Kumbuka suala la madeni ni suala pana sana sababu leo hali imebadilika kiasi kwamba ukishindwa kulipa utajipata ukifilisiwa mali zako. Hivyo ni heri usikope ikiwa huna malengo sahihi ya mkopo huo!


  • Mtazamo wa kiroho katika madeni.


Madeni yamebeba mtazamo wa kiroho leo maana shetani hufanya kazi kubwa sana kuleta mafarakano,ugomvi,visa,chuki,hasira n.k katika eneo hili la mikopo. Tumeshuhudia ndoa nyingi zikivunjika kwa sababu ya uwepo wa mikopo na madeni. Sasa ni lazima ujiulize,Je mambo haya ndivyo atakavyo Mungu? Jibu ni hapana,Mungu sio wa mafarakano! shetani ameingiza wengi kwenye utumwa pasipo kujua. Madeni madeni ni roho kamili ya shetani kwa kukuaribia uhusiano wako na mwenzi wako wa ndoa,Mungu hata kibiashara. Tuliangalie jambo hili kiroho;


01. Anayedaiwa sana si mtoaji wa sadaka nzuri,pamoja na mafungu ya kumi.


Ukimuona mshirika ambaye hatoi zaka / fungu la kumi / sadaka kikamilifu ebu cheki suala la madeni,kisha utaona. Ukweli ni kwamba mtu anayedaiwa hujitahidi sana kulipa deni kwanza kisha zilizosalia ndio hutoa kanisani,sasa inategemea na unalipa deni la kiasi gani maana ikiwa unapokea pesa fulani hivi mwisho wa mwezi alafu unajikuta una watu kama watano wanaokudai na wote wanasubiri upokee pesa tu kisha walipwe sasa angalia hapo utaigawanyaje hiyo pesa


maana kwanza haitoshi kisha ujatoa pesa ya kula na familia. Kwa staili hiyo,unafikiri utaweza kulipa zaka,au kutoa sadaka nzuri kwa Bwana? Jijibu tu mwenyewe! Ikiwa huwezi kumtolea Bwana,Je hugundui kwamba ni mpango wa shetani kukufanya umkose Mungu? Angalia ikiwa utashindwa kulipa fungu la kumi,Je wewe si mwizi wa sadaka ya Bwana? Utabarikiwaje sasa? 


02. Anayedaiwa daiwa hukosa ibada halisi ndani ya moyo wake.


Bwana alisema na Musa kwamba aende kwa farao ili Israeli wapewe ruhusa waende kumtumikia Mungu (Kutoka 9:1)’. Kile alichokitafuta Mungu ni “moyo wa ibada ndani ya watoto wake”  Maana alijua hawawezi kumuabudu Mungu katika roho na kweli ikiwa bado wapo utumwani Misri. Hivyo hata wewe kamwe huwezi kumuabudu Mungu katika roho na kweli ikiwa kama upo utumwani. Madeni yakikushika ujue upo utumwani na hapo hakuna ibada ya kweli maana utakuwa ukilia lia kwa uchungu wa kudaiwa wala sio kwa furaha ya Bwana.


03. Anayedaiwa daiwa ni muongo siku zote.


Hata kama umeokoka lakini hali ya madeni inakufanya udanganye danganye,ukifikiri ndio ufumbuzi kumbe unajilimbikizia dhambi. Jiulize hivi ukifa ghafla katika hali hiyo,utakuwa mgeni wa nani huko mbinguni? Je utaiona mbingu. Ukweli ni kwamba wadaiwa ni waongo sana,utakuta  mtu kapokea mshahara lakini akiulizwa na anayemdai husema hajapata bado mshahara huku mwisho wa mwezi umekwisha pita!!!!😁😁😁 Ni lazima ujue kwamba uongo ni dhambi na mwisho wake ni kwenye ziwa la moto.


Sasa nini cha kufanya?

  1. Ikiwa unahitaji kukopa,jiulize kwanza utaweza kurudisha kiasi hicho cha pesa?

  2. Umuombe Mungu kikamilifu,kama utakosa amani ndani yako basi ni afadhali uache mkopo huo,hata kama wenzako wamechukua lakini wewe acha!

  3. Ikiwa umepata amani,Pata ufahamu sahihi juu ya  mikopo marejesho. Ikiwa umekosa maelezo sahihi acha  kukopa!

  4. Uwe na malengo maalumu mfano biashara,ujenzi ambapo ukikopa kwa ajili ya ujenzi ujue ni kama vile pesa kwenda kuichimbia chini hivyo usishangae ukalia kwa wakati fulani,lakini kutakuwa na kicheko baadae.

  5. Hakikisha unamshirikisha mwenzi wako wa ndoa kama unaye. Kama la mshirikishe wa karibu nawe ajue kwamba umejiingiza kwenye mkopo na unadaiwa.

  6. Uendelee kuomba hata kabla hujakopa maana mikopo ya leo kuna hila ya shetani. Madawa ya giza yanatumika sana kwenye mikopo.


Kuomba ni njia pekee itakayokuwezesha kuweka sawa.

Ikiwa unahitaji kukopa zingatia maelezo hayo muhimu kisha kuomba ili kama kuna nguvu za ushilikina kwenye hizo pesa zisifanikiwe kukukamata. Wakati mwingine unaweza ukakosa mkopo na hapo usishangae wala kunungunika au kuona kwamba Mungu hakusikii ikiwa umeliombea vizuri jambo hili. Bali ujue hivyo ndivyo Mungu amekujibu maana amekuepusha na nguvu za giza kwenye huo mkopo uliokuwa ukiufukuzia.

Ufanyeje ikiwa umekamatwa kwenye roho ya namna hii?

  1. Omba toba ikiwa mahali popote pale umejisahau na kujipata umedondokea dhambini.

  2. Tumia damu ya Yesu kufuta jina lako lilipoandikwa katika ulimwengu wa roho. Popote walikoimbilizia jina lako,futa kwa damu ya Yesu. (Mimi nitakusaidia hapa ukinipigia simu ) 

  3. Omba Mungu akusaidie upate wepesi wa kupata pesa na ulipe madeni yako. 

  4. Ikiwa unadaiwa na watu zaidi ya watatu,ni vyema ukope deni tena uwalipe hao ili udaiwe sasa na mtu mmoja huku ukimuombea mtu huyo awe na moyo wa kukuvumilia. Usiongeze mikopo mingine isipokuwa kwa njia hii tu.

  5. Hakikisha unaombea biashara yako ili ikuzalishie tena ni muhimu umshirikishe mtumishi wa Mungu mwingine pamba

  6. Kili ushindi kila wakati.


Nipigie simu tupanue wigo wa ushauri na maombeziKwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900


What’sapp ni +255 746 446 446


Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page