top of page

MSALABA NA DAMU YA YESU.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi;

  1. Msalaba ni nini?

  2. Tofauti iliyopo kati ya msalaba wa Yesu na misalaba mingine.

  3. Kazi saba za msalaba katika maisha yetu.

  4. Damu ya Yesu na kazi zake.

  5. Msalaba ni nini?

Katika jamii ya zamani ilikuwa ni jambo la kawaida la kutundika maiti ya mtu juu ya mti kama ishara ya adhabu na  kutoa onyo kwa wengine. Hapo mwanzo katika adhabu ya namna hii ilitumika mti uliyotayarishwa kwa madhumuni ya kuninginiza maiti ya mwalifu au kumiuangika mtu hata kufa. 

Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti; mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi wako.” Kumb.21:22-23 Soma pia Esta 7:9

Hivyo basi msalaba ni adhabu ya kifo ya kutundikwa juu ya mti mpaka kufa na kila aliyeangikwa juu ya mti alilaaniwa. Kristo Yesu alifanyika  laana kwa ajili yetu kwa maana Yeye naye aliangikwa juu ya mti. Kristo alibeba dhambi kwa ajili yetu ingawa Yeye hakutenda dhambi yoyote wala dhambi impasayo kulaaniwa. Wagalatia 3:14

Biblia inasema zaidi ;“Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.“2 Wakorintho 5:21

Msalaba katika agano la kale;Ilikuwa ni adhabu mbaya na yakudhalilisha inayotolewa hadharani kwa watu wote. Sheria ya Kiyaudi iliwataka Wayahudi kuondoa mzoga wa maiti ulioangikwa msalabani kwamba usikae usiku kucha juu ya mti kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu.

Katika agano jipya;neno msalaba linaanzia kwa Kristo Yesu Yeye ambaye ni kielelezo chetu. Alipigwa,na kuangikwa juu ya msalaba hadi mauti yake na siku ya tatu akafufuka katika wafu. Hivyo tafsiri ya neno msalaba katika agano jipya imepanuka zaidi. Kwa maana msalaba ni;

01. Ni nguvu ya Mungu iokoayo. –“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.” 1 Wakorintho 1:18~ Ikumbukwe ya kwamba thamani ya wokovu wetu ipo pale msalabani kwa maana nje ya msalaba hakuna wokovu. Na ndio maana msalaba kwetu sisi tunaokolewa ni tendo la muhimu kuliko maelezo.

02. Njia ya Mungu katika wokovu. – “ Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. ” Mathayo 16:24

Neno hili; Yesu akuambia wewe leo,kwamba ikiwa unataka kumfuata Yesu basi ni lazima wala sio hiyari kwamba ujikane mwenyewe yaani ukatae kufuata mambo yako bali mapenzi ya Mungu yachukue nafasi ndani yako. Na hapa ndipo kwenye kiini cha wokovu wako,kwa maana wokovu halisi ni kujikana mwenyewe na kuchukua msalaba wako kwa ajili ya Bwana. Wokovu ni uhusiano wa kwako na Mungu katika kuyafanya mapenzi yake tu.

  1. Tofauti ya msalaba wa Yesu na misalaba mingine.

Ni vyema tufahamu ya kwamba kuna misalaba mingine;lakini kuna msalaba wa Yesu. Hivyo si kila msalaba ni msalaba wa Yesu,hapana! Tunajifunza jambo hili kwa kuangalia pale golgota mahali ambapo Bwana Yesu alisulibiwa;mahali pale palikuwa na misalaba mitatu yaani miwili ya wanyanganyi na mmoja ni wa Yesu. “ Wakati uo huo wanyanganyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto.” Mathayo 27:38

Hivyo katika misalaba mingine haikuwa na Yesu,bali wanyanganyi ndio walikuwamo. Ndio ndio tofauti kubwa. Sasa usistushwe uonapo mtu amevaa msalaba,jiulize msalaba huo ni wa Yesu? Au wa wanyanganyi? Kumbuka dunia ya leo imejawa na wimbi la wanyangaji wenye kujitambulisha kama Yesu lakini sio bali ni wevi na wanyanganyi. Wengi leo wamekuja kwa jina la Bwana na kumbe sio,sasa si rahisi kuwatofautisha bali unamuhitaji Roho mtakatifu akusaidie.

  1. Kazi ya msalaba katika maisha yetu. ( Zifuatazo ni kazi saba za  msalaba wa Yesu katika maisha yako.)

01. Kutukomboa katika laana ya torati. Wagalatia 3:13,Warumi 6:14

Kabla ya Yesu kwenda pale msalabani sisi sote tuliikuwa chini ya sheria,ambazo kwa sheria hizo tulifarakana na Mungu. Kwa maa maagizo yalikuwa mengi kufikia 653 kiasi kwamba hatukuweza kuepuka laana hizo. Lakini kupitia msalaba wa Yesu umetutoa katika laana hizo zote.

02. Yesu alilipa adhabu ya dhambi pale msalabani.

Tulipaswa kulipwa mauti kama mshahara wa dhambi zetu ( Warumi 6:23)lakini kwa neema yake Mungu kwa njia ya msalaba tupo mbali na mauti kama mshahara wa dhambi zetu. Mtunga Zaburi anatuambia kama tungehesabu maovu yetu,nani angesimama? ( Zab.130:3) hii ikiwa na maana kwamba sote tulihesabiwa mauti tena kwa kosa lake  mtu mmoja ( Warumi 5:16-17) Soma pia Isaya 53:6

03.Kutupa kibali cha kuingia patakatifu pa patakatifu kwa njia ya maombi

Ikumbukwe kwamba baada ya Yesu kukata roho,neno la Mungu linasema ;“ Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;” Mathayo 27:51.Ikiwa ni ishara ya kupata ruhusa ya kuomba moja kwa moja kwa Mungu. Kibali au ruhusa ya namna hii ni kazi ya msalaba maana haikuwa hivyo. Leo umepewa kibali cha kuomba mbele za Mungu na Mungu kukusikia na kukujibu pia.

04. Kuvunjwa kwa nguvu za mauti. – “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.” Waebrania 2:14-15

Neno “ kwa njia mauti” ni sawa na kusema kwa njia ya msalaba. Kwa njia hii tu ndio imetupa nguvu ya kuvunja mauti itokayo kwa ibilisi maana ni kweli ibilisi alikuwa na nguvu hiyo ya mauti lakini nguvu hiyo imeshughulikiwa pale msalabani. Kwa sababu hiyo,leo unayo nguvu ya kuvunja kila mauti ijiinukayo kwako kwa sababu ilikwisha shughulikiwa msalabani.

05. Msalaba wa Yesu ulishughulika na huzuni na masikitiko yetu. Isaya 53:4

06. Kufutwa kwa hati ya mashtaka – akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;15 akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” Wakolosai 2:14-15

07.  Kuponywa magonjwa. 

Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” 1 Petro 2:24

Mathayo 8:17 ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu,Na kuyachukua magonjwa yetu. Soma pia Isaya 53:5

  1. Damu ya Yesu na kazi zake.

Kumwagika kwa damu ya Yesu Kristo msalabani kulikuwa ni muhimu ili sisi sote tupate msamaha wa dhambi zetu. Maana imeandikwa pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo la dhambi ( Waebrania 9:22)

Ondoleo la dhambi zetu hutegemea damu ya Yesu.“ kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” Mathayo 26:28(Soma pia Waebrania 13:12 ,1 Yoh.1:7,Waefeso1:7,Waebrania 9:26.)

  1. Matumizi ya damu ya Yesu.

01.Katika toba. Sasa tunapoingia katika toba,tukumbuke kuialika damu ya Yesu ikasafishe dhambi zetu. Katika toba,damu ya Yesu hufanya kazi kubwa mbili nazo ni;

  1. Kusafisha dhamiri na matendo mafu. ~“ basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” Waebrania 9:14

  2. Kufanya upatanisho ~Waefeso 2:13 “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.” Soma pia Wakolosai1:20 -22;

02.Katika ukombozi – Katika eneo hili ni lazima ujue kwamba ni damu pekee na jina la Yesu ndio yenye kuleta ukombozi. Hata sasa waweza kuitumia damu ya Yesu kukomboa mali zako,biashara zako,ardhi yako n.k. Biblia inaeleza ;

Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.1 Petro 1:18-19. Hakuna awezaye kulipa gharama ya ukombozi isipokuwa damu ya Yesu tu.

03.Katika ulinzi. 

Huitaji kitu kingine kikulinde dhidi ya uvamizi wa kiroho isipokuwa unahitaji damu ya Yesu tu. Kumbuka kile kilichowalinda wana wa Israeli wasipigwe na mwaribu,kilikuwa ni damu ya mwana-kondoo. Leo hii damu ya mwana-kondoo ni damu ya Yesu,inalinda hata sasa. ( Soma Kutoka 12:23. ) Chukua hatua ya kulinda mali,watoto,familia kwa kuzifunika kwa damu ya Yesu.

04.Silaha ya vita vya kiroho- Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” 

Kwa huduma ya maombezi usisite kunipigia sasa +255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page