KRISTO PASAKA WETU.
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 14, 2017
- 2 min read

Na mch. G.Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Biblia inatuambia kwamba pasaka wetu ni Kristo naye amekwisha kutolewa sadaka kwa ajili yetu. Hivyo biblia haisemi kuwa pasaka ni sikukuu bali pasaka ni jina la mwana-kondoo wa Mungu anayetolewa kama sadaka ya ukombozi kwa ulimwengu wote. Kwa namna hii tunaweza kuielewa pasaka vyema kwamba pasaka ni ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya Kristo katika mwili na damu ya Yake. Hivyo kama amekwisha kutolewa basi,hatuna haja ya kulia kwa kuangaika kutafuta ukombozi,bali tunauhakika na Yeye ambaye ndiye ukombozi wetu.
Tunapoadhimisha kumbukumbu hii ya pasaka kama ukombozi wetu,hatuna maana ya kwamba tarehe fulani ya mwezi fulani kwamba ndio Yesu Kristo anakufa na kufufuka kisha sasa tunasherekea! Hapana!! Bali tunaadhimisha kumbu kumbu tu,kwa maana pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka yaani Yesu,hatolewi tena kwa mara nyingine;ilikuwa mara moja tu kwa ukombozi wa wote.
Pasaka wetu hakutolewa kwa wakristo tu,bali kwa watu wote ulimwenguni kwa kila aaminiye anapokea ukombozi. Hili ni jambo muhimu sana lifahamike hivyo,maana leo pasaka amepewa taswira katika mlengo mmoja tu,mlengo wa wakristo, Yeye Yesu alikuja kuwaokoa wenye dhambi wote mmoja wao ni mimi na wewe;“ Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.” 1 Timotheo 1:15
Hivyo tunapoitazama pasaka tunapaswa kuitazama pasaka kwa jicho la ukombozi wa mwanadamu katika sadaka iliyotolewa pale Kalvari msalabani na hatupaswi kuitazama katika jicho la sikukuu ya kusherekea tu kama dunia ifanyavyo. Dunia wanashereke siku na kufanya anasa zote wakijua kwamba pasaka ni sikukuu ya kujirusha kistarehe,bali kila mkristo anapaswa aipokee pasaka kama ukombozi aliyoupata kwa damu ya Yesu na mwili wake.
Tuliangalie neno letu la msingi lililobeba ujumbe wa leo;“… Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;” 1 Wakorintho 5:7 . Kwa kuwa Kristo ndiye pasaka wetu,basi yeye amefanyika sadaka kwa ajili ya kila mtu. Sadaka ya namna hii inayozunzumziwa katika neno ni sadaka ya dhabihu kwa ajili ya ukombozi.
Ni Yesu tu ambaye ndie ametukomboa kwa kututoa katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa nuru ( Wakolosai 1:13-14). Ndani yake,Yeye Pasaka wetu tunapokea mengi katika uzima huu wa sasa na ujao. Kila mtu,ni lazima apate ufahamu kwamba hatupo tena chini ya laana ya torati kwa sababu Kristo Yesu alitukomboa na laana hizo ( Wagaratia 3:13)
Hapo zamani, adhabu ya dhambi ilikuwa mauti kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Hivyo ilibidi ulimwengu wote uadhibiwe mauti kwa sababu ya dhambi zetu,lakini kwa huruma zake Mungu akamtuma mwanae wa pekee ili afe yeye kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Kwa mtazamo huu ulio sahihi juu ya pasaka,unakufanya usiitizame pasaka kama siku bali kama ukombozi wako.
Fikiria laiti kama pasaka wetu,Kristo asingelitolewa kwa ajili yetu,Je ingekuwaje? Unaweza kuona kwamba ilikuwa kwa huruma zake Mungu tu juu yetu. Tunakumbuka jinsi pasaka ya kwanza ilivyofanywa ( Kutoka 12:1-28),Musa aliambiwa “ Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele” Kutoka 12:14. Hivyo basi neno linatutaka kuikumbuka pasaka kwa amri ya milele,hii ikiwa na maana kwamba pasaka ni moja kati ya ibada muhimu ya kuikumbuka kwa amri ya milele.
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa +255 683 877 900
What’s app number ni+255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments