DAMU INENAYO MEMA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 18, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 26, 2022

“ na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.” Waebrania 12:24 (KJV)
Katika andiko hilo tunaona mambo matatu muhimu.
01. “ Yesu mjumbe wa agano jipya”
Tafsiri ya neno “mjumbe” kama lilivyotumika hapo humaanisha “ mpatanishi ” kwa lugha ya kiingereza ni “ mediator” na sio “ messenger ” . Mpatanishi ni yule anayesimama katikati ya hakimu na mkosaji,Kwa kumsaidia mkosaji asihukumiwe. Musa naye alikuwa mpatanishi wa agano la Kale ambapo aliwapatanisha Waisraeli na Mungu mara nyingi ( Kutoka 32:11) . Kuonesha atakuja mpatanishi wa ajabu Hivyo Yesu ni mpatanishi wa agano jipya (1 Timotheo 2:5)
2. “ …damu ya kunyunyizwa..”
Matumizi ya damu ilikuwa katika “kupaka/kukipiga kizingiti – Kutoka 12:21″ Kwa ajili ya kuzuia uharibifu katika nyumba. Lakini pia ilikuwa kwa ajili ya “kutia” kama kuhani Haruni alivyosimikwa katika ukuhani wake,alitiwa damu sikuoni yeye na wanawe Kwa ajili ya kuwekwa wakfu yaani kutengwa Kwa kazi ya Bwana ya kikuhani. Matumizi ya damu ya namna hiyo yalimzungumzia Mwana-kondoo wa Mungu yaani Yesu ( Kwa maana agano la kale lote,linamzungumzia Yesu kama kiini cha agano)
03.”… inenayo mema kuliko ile ya Habili“
Hapa,lazima ujue kwamba damu imebeba sauti. Bila kujali ni damu ya mtu gani. Ndio maana damu hunena kwa sababu huwezi kunena kama huna sauti, hivyo Biblia inatuambia “damu ya Yesu inanena mema kuliko ya Habili” kuonesha kwamba damu ya Habili nayo ilinena ingawa haikunena mema kama damu ya Yesu. Neno “ kuliko” lina maana ya “ zaidi” hivyo damu zote hunena lakini ya Yesu hunena “zaidi” mema.
Kama damu ya Habili ilinena,ilinena nini?
Kwa mujibu wa Mwanzo 4:10 tunaona damu ya Habili mtu mwenye haki,nabii wa Mungu, damu yake ilinena “kilio” ambacho Mungu aliisikia kutoka katika ardhi.
Na Kwa kuwa Kaini ndiye aliyemwaga damu ya Habili Kwa kumuua,hivyo sauti ya damu ya Habili haikumwacha salama popote alipoenda.
Hii ina maana ukimwaga damu ya mtu yeyote,damu hiyo itakufuatilia popote uendapo,utakuwa salama tu kupitia damu ya Yesu itakayokuja kunena mema. Jifunze Kwa Kaini namna ambavyo sauti ya damu ilivyofungua “lango la mauti” kiasi kwamba kizazi chake chote kiliteswa na roho ya mauti,mauaji yaliwafuata kizazi Hadi kizazi.
Biblia inasema hadi kizazi chake cha tano kiitwacho Lameki nacho kiliua mtu – Mwanzo 4:23
Lakini pia hata ukitoa mimba,ujue “umemwaga damu ya mtu asiyekuwa na hatua kama vile damu ya Habili mtu asiyekuwa na hatua” sauti ya damu hiyo haitakuacha salama kwa sababu umeua,tena mbaya zaidi umeua kwa kukusudia!!! Pona yako ni toba halisi kwa damu ya Yesu tena itakuwa vyema urudishwe kundini na mchungaji kwa sala upya ya toba
Pamoja na hayo,hata hivyo leo kuna watu wengine wanaosumbuliwa na roho za mauti kwa sababu malango ya ukoo yameshikiliwa na sauti ya damu ya mtu mwenye haki kama Habili aliyeuwawa zamani na sauti hiyo haijashughulikiwa,hivyo inadai mauti. Ndio maana unaweza kuona roho ya mauti inavyosumbua kizazi hata kizazi kama ilivyotesa kizazi cha Kaini mtu mwovu.
Lakini biblia inasema damu ya Yesu inanena mema kuliko damu ya Habili. Yapo mema mengi yanayoachiliwa na damu ya Yesu katika maisha ya mwamini. Moja ya mema ni “ damu ya Yesu inanena juu ya ushindi – Ufunuo 12:11″ . Ushindi tuupatao katika damu ya Yesu ni mpana sana,yaani maeneo yote yanayohusu ushindi. Mfano eneo moja ni ushindi dhidi ya nguvu za mauti-( Waebrania 2:14)
Kwa kuwa katika damu ya Yesu kuna nguvu dhidi ya roho za mauti,hivyo Roho za mauti,nguvu za mauti hushughulikiwa kwa damu ya Yesu. Pale msalabani ibilisi alipigwa,na kuharibiwa nguvu za mauti, hivyo tunapoomba tutambue hilo na tuombe kwa imani huku tukiwa na mahusiano mema na Mungu.
Ikiwa unahitaji msaada zaidi pamoja na maombezi ili kusudi utoke kwenye vifungo vya ibilisi. Waweza kunipigia simu Kwa namba hapo chini.
Pia ikiwa umebarikiwa, nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.
Mawasiliano ni +255 683 877 900
What’s app number+255 746 446 446
Na Mch. Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comments