top of page

AMEFUFUKA KWELI KWELI

Picha kutoka google. “ Yesu amefufuka katika wafu”


Bwana Yesu asifiwe…

Heri ya sikukuu ya Pasaka mpendwa…

Kwa ufupi.

Yesu aliteswa akafa msalabani kwa ajili yako na siku ya tatu akafufuka katika wafu kama ilivyoandikwa ( Matendo 2:22-24,Mathayo 28:7). Hii ina maana kaburi halikumuweza,Yeye tu hai anaishi hata sasa. Katika sikukuu ya Pasaka unayosherekea ni lazima ujue ya kwamba Yesu amelishinda kaburi,Yeye yupo na anaishi hata sasa,ukimpokea ataingia kwako na mambo haya ninayokueleza si mambo ya kinadharia bali ni mambo halisi. Kwa mujibu wa biblia,leo nataka nikupitishe kwenye maandiko yenye kueleza juu ya kujidhihirisha kwa Yesu baada ya kufufuka katika wafu,ili kwamba uwe na cha kusema kwamba hakika amefufuka kweli kweli.

Watu wengi hawafahamu kwamba Yesu alijidhihirisha zaidi ya mara tatu, bale wengi hufikiri kwamba amejidhihirisha mara moja au mbili au mara tatu na kuona kwamba maandiko yamejirudia rudia kwa tukio moja tu. Hata mimi mwenyewe nilikuwa nikifikiri hivyo,lakini baada ya kuchukua muda na kuliangalia jambo hili kwa ukaribu zaidi,nikagundua kumbe Bwana Yesu alijidhihirisha mara nyingi tofauti na nilivyokuwa nikifikiri. Nami nataka na wewe leo upate picha hii mpya ujue kwamba Yesu alijidhihirisha mara nyingi katika nyakati tofauti tofauti na wakati mwingine kwa wanafunzi tofauti.

01. Yesu ajidhihirisha kwa Mariamu Magdalene huko Yerusalemu. ( Marko 16:9-11 & Yohana 20:11-18)

Mariamu Magdalene ndiye yule ambaye Yesu aliyemtoa pepo saba ( Luka 8:2). Lakini ndiye mwanamke wa pekee kabisa ambaye kwa mara ya kwanza baada ya kufufuka kwa Yesu,injili ya ufufuo inahubiriwa na yeye ( Mariamu Magdalene ) maana alitumwa na Bwana aende akawape mitume habari njema za kufufuka kwa Yesu. Tunajifunza kwamba Mungu wetu hana mipaka ya kututumia Yeye ni tofauti na wanadamu,Mungu huwatumia wanyonge kuwaaibisha wenyewe nguvu. Aliwaacha mitume na kumtumia mtu asiyekuwa mmoja wa mtume. Hata wewe ukikutana Yesu,uwe na uhakika atakutumia kwa viwango vya juu. Siku hii Bwana alipojidhihilisha ilikuwa ni Jumapili ( Resurrection sunday)

02.Kaburi li wazi huko Yerusalemu ( Mathayo 28:1-10,Marko 16:1-8,Luka 24:1-12,Yohana 20:1-9)

Udhihilisho huu ulikuwa wa kipekee kwa sababu umerekodiwa na wainjili wote wanne ukilinganisha na dhihilisho nyingine. Kaburi liko wazi,wanaemtafuta,wanaemfuata hayupo maana amekwisha fufuka tayari. Nayo siku hii ilikuwa ni Jumapili ( Resurrection sunday). 

03.Yesu ajidhihirisha kwa wanawake wengine huko Yerusalemu (Mathayo 28:9-10)

Katika udhihilisho huu,tunaona mwanamke mwingine akiwa pamoja na Mariamu Magdalene ( huyu alikuwa Mariamu wa pili). Akawatokea walipokuwa wakirudi kutoka kulitazama kaburi,wanawake hawa walipata nafasi ya kumshika hata miguu pamoja na kumsujudia. Hii ni dhahiri kabisa kwamba kulikuwa na kitu cha kipekee kwa wanawake maana ukiangalia ni wao ndio wamepewa nafasi kubwa wakati wote katika udhihilisho. Lakini na hata sasa ukweli utabakia pale pale kwamba wanawake wana huduma kubwa sana,Mungu kaweka ndani yao. Na siku hii ilikuwa ni Jumapili (Resurrection sunday)

04. Kwa watu wawili waliokuwa wakienda Emausi  huko kwenye njia ya Emausi ( Marko 16:12-13 & 24:13-32)

Hawa majamaa hawakujua mtu waliokuwa wakizungumza nae maana macho yao yalikuwa yamefumbwa. Lakini walipofumbuliwa wakamtambua, baada ya kushiriki nao meza ya Bwana. Na yenyewe ilikuwa ni Jumapili (Resurrection sunday)

05.Yesu ajidhihirisha kwa Petro huko Yerusalemu ( Luka 24:34,& 1 Wakorintho 15:5 ). Kefa aitwaye Petro naye alitokewa na Yesu pamoja na wanafunzi wake.

06.Kwa wale wanafunzi 11 waliokuwapo ghorofani huko Yerusalemu ( Marko 16:14 & Yohana 20:26-31, 1 Wakorintho 15:5)

Katika injili ya Marko,tunaelezwa vile wanafunzi wake hawakuwa na imani walikaa katika kuamini pamoja na mioyo migumu. Lakini ndipo tunaona pia kwenye injili ya Yohana,Tomaso aitwaye pacha hakuamini kabisa mpaka akahitaji kuona kovu za misumari,na tena mpaka kutia kidole chake kwenye hizo kovu. Lakini Yesu asema “ heri wale wasioniona wakasadiki” hii ni sawa na kusema “ wamebarikiwa wale wanaoamini pasipo kuhitaji kumuona kwa macho yao ya mwili”. Leo hatuna sababu ya kutokuamini kama Tomaso,ukiamini ya kwamba Yesu Kristo amefufuka katika wafu sawa sawa na yasemavyo maandiko matakatifu,ujue baraka ni juu yako. Ilikuwa ni siku ya Jumapili inayofuata.

07.Kwa wanafunzi 10 ghorofani huko Yerusalemu ( Luka 24:36-43,Yohana 20:19-25 ). 

Hili ni tukio jingine la Yesu kudhihirisha kufufuka kwake kipindi hiki wanafunzi walikuwa na hofu kubwa ya Wayahudi,lakini Bwana anawaondolea hofu maana imekwisha andikwa kwamba Yesu atakufa na siku ya tatu atafufuka katika wafu tena amekaa mkono wa kuume wa Baba. Ilikuwa ni siku ya Jumapili.

08.Kwa wale wanafunzi 7 waliokuwa wakivua huko kwenye ziwa Galilaya ( Yohana 21:1-23)

Tukio hili ni la kipekee na linaripotiwa na mwinjili Yohana tu. Yesu alijidhihirisha kwa wanafunzi wake 7 baada ya siku kadhaa,miongoni mwa hawa wanafunzi alikuwepo Simoni Petro pamoja Yohana mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda,na Yohana ndie alimtambua kwamba ni Bwana. Kitu cha ajabu ni kwamba walirudi katika kazi zao za uvuvi,lakini Yesu anakuja kuwatia nguvu kiimani kwamba Yeye bado yupo nao,hai na akiishi,na waendelee na injili kama kawaida. Jambo kubwa unatakiwa usikate tamaa,Bwana yupo pamoja na wewe siku zote.

09. Kwa wanafunzi 11 kule mlimani Galilaya ( Mathayo 28:16-20 & Marko 16:15-18)

Baada ya muda kadhaa,Yesu anawatokea mitume wake 11 na anawapa sasa “ agizo kuu” hapa ni muhimu uelewe kwamba wanafunzi wamepewa kazi ya kulifanya agizo hilo,hata sasa wewe na mimi tupo kwenye sehemu hiyo hiyo ya agizo kuu. Agizo kuu ni “ enendeni,mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho mtakatifu”

10. Yesu akiwatokea watu zaidi ya 500 ( 1 Wakorintho15:6 )

Baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja. Katika andiko hili,linatupa uhakika kwamba Yesu aliwatokea watu wengi zaidi ambao wengi hata sasa wanaishi na wengine walikwisha kufa,kwamba hata Yesu ameendelea kujidhihirisha.

11. Kwa Yakobo na mitume wengine Yesu akajidhihirisha kwao  ( 1 Wakorintho 15:7)

12. Kwa wanafunzi wake kwenye mlima wa Mizeituni karibu na Yerusalemu.( Luka 24:44-49 & Matendo 1:3-11)

Siku 40 baada ya kufufuka kwake Yesu anawatokea wanafunzi wake tena. Wanafunzi walitamani kujua kuhusu wao kupata ufalme warudishiwe,lakini Yesu akiwajibu si kazi yao kujua nyakati wala majira Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake. Lakini “watapokea nguvu za Roho mtakatifu”. Sasa ndipo kazi ya injili ikaanza kwa nguvu mpya ndani yao. Yesu akawabatiza katika Roho mtakatifu kuwaimarisha kwa kazi ya injili ( Matendo 2:4)

13. Yesu ajidhihirisha kwa Paulo huko Dameski baada ya miaka fulani ( Matendo 9:1-9)

Kumbuka katika kila tukio la kujidhihirisha kwa Yesu kulikuwa na lengo maalumu na ndio maana unaona akiwatokea wanafunzi wake kwenye mazingira tofauti na kusema nao. Lakini pale Yesu alipomtokea Paulo ilikuwa ni muhimu sana aweze kumgeuza Sauli hata kuwa mtume Paulo. Kwa lengo la kumfanya awe mtume mwaminifu kwa mataifa. Haikuwa kazi rahisi kwake Paulo maana alimuhitaji Yesu ambadilishe.

Nimekuandikia kwa ufupi kwa msaada wa Roho mtakatifu pamoja na kusoma kwangu vitabu hasa biblia ya NIV ( New International Version) hivyo taarifa zote nilizokuandikia zimehakikiwa. Lakini lengo kubwa ni kupitisha kwenye maandiko matakatifu juu ya kufufuka kwa Yesu,kwamba Tu hai hata sasa. Hata leo bado Yesu amejidhihirisha kwa watu wake wengi na kututia nguvu katika kazi hii ya injili.

Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page