MOYO WA SHUKRANI.
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 7, 2018
- 4 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Kulikuwa na mzee mmoja hivi kipindi cha miaka ya 70 ambaye alikuwa akimpenda Mungu sana. Alijitahidi asikosane na Mungu kwa namna yoyote ile. Ikiwa siku moja akaumwa sana hata kukosa kupumua,(kwa kweli alikuwa afe) lakini kwa neema ya Bwana alijikuta amepekwa hospitali akiwa katika hali mbaya maana aliumwa kwa dharula tu,na watu wake wakashangaa imekuwaje tena kwa kipenzi chao babu!!! Alipokuwa hospitali,madaktari wakamuwekea mipira ya kupumua ili waokoe uhai wake maana alikuwa hawezi kupumua. Hivyo wakamfunga vifaa maalumu vya kupumulia kupata hewa,oxygen. Naye akapumulia mipira hiyo’.
Baada ya masaa mawili kupita madaktari wakaona babu wa watu amekaa vizuri,hivyo wakachomoa mipira hiyo ya kupumulia naye babu mzee wa watu akaweza kupumua vizuri. Kabla ya kutoka hospitali,wakamletea bill / gharama ya kifaa kile alichokuwa akipumulia kwa masaa mawili tu. Na gharama yake ilikuwa tshs milioni moja na ( tshs 1,500,000/= ). Na kumbuka hiyo ilikuwa miaka ya 70,sio miaka ya 2000 kama ya leo;hivyo utagundua kwamba ilikuwa ni pela nyingi sana iliyodaiwa alipe pale hospitali. Yaani kwa masaa mawili tu gharama yake ikawa ni milioni moja na nusu, duh!!! Wote wakashangaa!!
Mzee wa watu akawauliza “ hii ndiyo gharama ya matibabu yangu ya kutumia kifaa hiki cha kupumulia hewa kwa masaa mawili tu? Jamani naomba mnijibu!” Wauguzi wakamwambia “ ndio maana yake,kifaa kina gharama hicho,kuvuta hewa oxygen inagharama mzee wangu”.. mzee wa watu akajiinamia na mara moja akaanza kumtafakari Mungu,kisha akasema;
Hivi ikiwa kwa masaa mawili tu niliyovuta pumzi kwa chombo hiki cha mwanadamu ninalipa tshs milioni moja na laki tano,yaani masaa mawili tu! Akajiuliza,kama Mungu angeliamua kunilipisha kiasi cha pesa kwa pumzi yake tangia nilipozaliwa ningelipa tshs ngapi jamani? Mbona mimi ninakosa shukrani kwa Mungu kwa ajili ya pumzi yake anipayo bure tena kila siku.
Mzee wa watu akatamani achukue calculator ( kikokotoa) na kuanza kupiga hesabu kwamba amevuta pumzi ya Mungu kwa masaa mangapi tangu kuzaliwa kwake azidishe na gharama ya milioni moja na laki tano kisha aone anadaiwa tshs ngapi na Mungu? Hata hivyo aliona atapata kiasi kikubwa kisichosomeka! Akamtazama Mungu kwa jicho la utofauti. Akawalipa pesa yao na kuondoka huku akiendelea kumtafakari Mungu kwa pumzi yake ya bure kabisa anayompa,maana kumbuka ameiacha milioni moja na laki tano hospitali kwa pumzi ya masaa mawili tu! Kuanzia hapo moyo wa shukrani ukajengeka ndani ya yule mzee,akawa akimshukuru Mungu sana kwa pumzi,uhai na maisha yake kwa ujumla.
Unaelewa lakini wewe usomaye sasa?
Fikiria wewe mwenyewe,ni mara ngapi unapumua kwa siku,tena bure? Na ni mara ngapi unamshukuru Mungu? Ni mara ngapi Bwana anakutetea dhidi ya adui zako?na ni mara ngapi unamshukuru Mungu katika hayo? Hivi unanielewa lakini? Unajua pumzi unayovuta sasa sio ya kwako? Unajua gharama yake? Je laiti kungelikuwa na luku ya pumzi,Je usingelikufa kwa kushindwa kumudu kulipia? Wewe unafikirije? Unadhani wewe ni bora sana kuliko waliokufa leo,ambao hawana pumzi hiyo? Muogope Mungu,uone kwamba umepewa neema tu na Mungu,unatumia oxygen yake bure alafu hata kumwambia Mungu mmiliki wa oxygen yake neno ASANTE huwezi,!!!
Mimi huwa sielewi,jamani nasema ukweli kwamba huwa sielewi elewi kabisa kwa mtu anashindwa kumshukuru Mungu kwa pumzi tu akupayo. Maana utakuta sisi wachungaji tukiongoza maombi mbele ya madhabahu ya Bwana MUNGU aliye hai,tukiwaambia watu “ haya,haya kila mmoja wetu aanze kumshukuru Mungu,tuombe….” lakini papo hapo utakuta kuna majamaa hata hawaombi,wenyewe wanakutazama tu!!! Jamani,hivi kweli huna la kumwambia Bwana asante. Ni kweli au unatania? Ni kweli au unafanya mizaha mbele za Mungu?
Ebu jiulize leo hii, wewe mwenyewe mbona mara nyingi au siku zote kwamba unalala tu bila hata ya kutafakari ukuu wa Mungu katika maisha yako. Hivi ni kweli kabisa Bwana MUNGU hajakutendea kitu katika maisha yako? Pumzi hiyo je unayoivuta si moja ya matendo makuu ya Bwana Mungu. Unataka utendewe nini sasa? Kwa nini huna moyo wa kushukuru? Au unataka mwenye pumzi yake aichukue ndipo uanze kumshukuru,inawezekanaje kwa hilo?.Mimi nakuomba usichukulie poa au kawaida kwa vile unavyoitumia hewa ya Mungu bure,au kwa vile uonavyo mambo yako yaendavyo bali ni lazima uende mbele za Mungu kwa shukrani siku zote. Ni muhimu sana.
Jizoeze kumshukuru Mungu kila wakati.
Ifike wakati uwe na moyo wa kushukuru mbele za Mungu. Ondoa tabia za kitoto toto zile za kuomba omba kila wakati kutaka Mungu akutendee bali uwe na tabia ya kiutuuzima ndani ya Kristo,kutanguliza shukrani zako zote kabla hata ya kuomba mambo mengine tena hata wakati mwingine unaishia hapo hapo tu,yatosha!. ( sikuambii usiombe mambo mengine,bali uwe na moyo wa kushukuru). Unajua hakuna kitu kibaya kama kukosa moyo wa shukrani! Na mara nyingi wale wanaotendewa zaidi ni wale tu wenye moyo wa shukrani.
Hivi kwa nini usifikirie kwamba yote uyapatayo ni kwa uweza wa Mungu ndani ya Kristo Yesu? Hakuna hata jitihada yako moja iliyokuwezesha kuwa hivyo ulivyo,na ufahamu hilo. Huyo mume uliyenaye sasa ujue ni Bwana tu,wala usifikirie eti kwa sababu ya uzuri wako,ingelikuwa hivyo basi wazuri wote wangeliolewa!! Huyo mke ulionao ni Bwana tu,na.wala moyo wako usiinuke ukadhani kwa sababu unajua sana kushawishi wanawake,au kwa sababu unapesa! Hivyo ulivyonavyo uone ni Mungu,ndipo uende mbele za Mungu kwa shukrani sana. Unafahamu wengi wanatamani kuwa kama wewe lakini hawakuweza,wewe ni nani?
Ukishindwa kumtafakari Mungu,ujue huwezi kuwa na moyo wa shukrani maana utaona ni uwezo wako katika yote uliyonayo na uyatendayo kitu ambacho ni makosa makubwa,lakini cha ajabu ndivyo ufanyavyo hata sasa. Lakini kupitia ujumbe huu mpendwa naomba ubadilike,mpe Mungu utukufu….Unajua masomo yako unayochukua sasa ni Bwana tu,au vile uonavyo watoto wako wasomavyo ni Bwana tu. Ni lazima umuone Mungu ndiye mtendaji wa vyote hivyo,hata kama unaona mambo yako hayaendi bali mtazame Mungu na umshukuru maana ni bora uwe na mambo yasiyoenda lakini una uzima!Usidhani ni uwezo wako,bali ni Bwana.
Moyo wa shukrani ni moyo unaomrudishia Mungu utukufu na heshima zote. Yeye Bwana ni wa kusifiwa sana,ndiye akutendeaye mema siku zote tena wakati mwingine hata hujaomba! Ukiwa na moyo huu,utajikuta ukimuinua Mungu kuona uweza wake wala hutaweza kujiangalia wewe. Wewe binti,mpe Mungu utukufu kwa vile ulivyo,mshukuru Mungu kwa matendo makuu na uone ni Bwana tu. Maana kuna mabinti ambao kwa kweli wanalingia urembo,uzuri wao wakidhania ni wao wao tu,hapana! Huyo ni Mungu na vivyo hivyo kwa vijana wakiume,mpe Mungu utukufu kwa vile ulivyo. Wewe unafikiri utakuwa na muda mwingine wa kumshukuru Mungu ikiwa muda huu hutaki kushukuru?
Ni lazima uwe na moyo huu wa kushukuru. Sasa anza mazoezi ukiomba Roho mtakatifu akusaidie kukujenga imara katika eneo hili la kushukuru kwa kila jambo maana yote ni mpango wa Mungu katika Kristo Yesu ( 1 Wathesalonike 5:18). Ebu ukiona unahitaji msaada zaidi nipigie sasa kwa namba zangu zilizopo hapo chini;
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Комментарии