MOYO WA KURIDHIKA
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 11, 2019
- 2 min read
Updated: Sep 29, 2022

Katika safari ya wokovu,Bwana anatutaka tuwe na maisha ya kuridhika / kutosheka katika kile tulichonacho. “ kuwa na moyo wa kuridhika ” hakumaanishi uache kutafuta,bali kuwa mwaminifu katika kile ulichonacho huku ukiridhika. Wokovu unazungumza hasa na kuridhika katika kila upatacho kutoka kwa Bwana, kwa maana ukiridhika ujue ni vigumu kuiba,au ni vigumu kuleta uharibifu.
Kumbuka,kinyume cha kuridhika ni “ ubinafsi” tabia mbaya!!! . Na hiyo (ubinafsi) ndio moja ya tabia sugu na tabia mama ya wanadamu wote. (Ubinafsi ni kujilimbikizia mali). Fikiria tu,mkiwa namna ambavyo watu hujipenda wao wenyewe na kujijali wao wenyewe,utagundua bado tu wabinafsi mno,na hatuna moyo wa kiridhika.
Bwana Mungu alifundisha somo hili kwa watu wa taifa lake la Israeli pale alipowatoa Misri kwenye kongwa zito la utumwa. Bwana aliwapitisha jangwani ili “ kuwatweza“.Hata walipomnungunikia Musa na Haruni,na kwa huruma zake Mungu, akawashushia mvua ya mikate na nyama ( Kutoka 17:1-3). Bwana bila kufanya kazi,Mungu akapa chakula cha mana lakini hata hivyo bado hawakuridhika na hatimaye wakawa na manunguniko. Ukweli ni kwamba chakula cha Mana walikitumia muda wa miaka 40 huko jangwani.
Uwezekano wa “kukinai“ chakula ulikuwepo mkubwa kwa sababu kwa miaka 40 walikula chakula cha aina moja. Hata kwako,ikiwa utakula chakula kimoja kwa muda mrefu,ujue itafika wakati utakinai. Lakini unafikiri kwa nini Bwana aliruhusu watu hawa wale chakula hicho hicho kwa muda mrefu kiasi hicho? Bila shaka Bwana alikuwa akiwafundisha “ moyo wa kuridhika/kutosheka kwa kila wanachopokea kutoka kwake“
Biblia ina kaza zaidi katika eneo hili “ Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.” 1 Timotheo 6:6,soma na mstari wa 8. Neno linatanguliza utauwa kama sehemu muhimu sana kwa mtu,kwamba utakatifu/uchaji wa Mungu ni vyema uwe wa kwanza. Lakini utauwa unastahilishwa na “ kuridhika ” ili kusudi kuifunga tamaa isichomoze kwa maana tamaa ni shina la dhambi kisha mauti pia. Paulo anafahamu fika kwamba mtu wa Mungu akifanikiwa kuwa utaua na kuridhika basi atakuwa amefauru kiasi kikubwa katika wokovu wake.
Mtu mwenye moyo wa kuridhika kwake hakimsumbui kitu cha mtu mwingine. Ajapomwona fulani kafanikiwa,yeye hawezi kujisikia vibaya kwa maana ametosheka na alichonacho hata kama kitakuwa kidogo. Kwani hujawahi kuona mtu ambaye haumii kabisa na mafanikio ya mtu mwingine? Ndio wapo baadhi watu wenye mioyo ya kutosheka na walichonacho.
Siri ya kuwa na moyo huu;
Roho mtakatifu ndiye amfanyaye mtu kutosheka. Unajua Yeye ni maji ya uzima yakatayo kiu zote. Ukiwa naye umepokea bubujiko kuu la kuridhika,kama ni kwenye ndoa ni lazima atakutosheleza tu,au iwe kwenye kazi atakutosheleza pia. Lakini kama ikiwa upo mbali naye, basi ujue kamwe huwezi kuridhika; mfano mdogo tu ni pale umwonapo mtu anayeshindwa kwenda kanisani kwa sababu ya kisingizio cha kukosa nguo nzuri.
Ukweli ni kwamba kuna watu ambao hukataa kwenda ibadani wakisema hawana nguo kwa maana kuna Jumapili kadhaa amerudia kuvaa nguo hizo hizo. Mtu wa namna hii amekosa moyo wa kuridhika kwa maana kwani kuna shida gani kurudia rudia nguo za Jumapili? Kwa nini uogope macho ya watu?
Mwenye moyo wa kuridhika anaweza akawa na suruali moja na shati moja lakini ibada ipo pale pale,tena na furaha yote,akiona mambo yakienda kama kawaida.Jiulize;una moyo wa namna hiyo?
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI,piga sasa kwa namba hizi + 255 683 877 900
Whatsapp namba +255 746 446 446
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments