top of page

MGONJWA HAOMBEWI KESHO, ANAOMBEWA LEO.



Bwana Yesu asifiwe…

Usiseme “ nitakwenda kumuombea kesho mgonjwa” bali sema “ nakwenda leo, tena sasa ” kwa maana ya kesho huyajui, ya kesho yamefichwa! Ni nani ayajuaye? Ebu fikiri dakika moja ijayo kutoka sasa, je hata hiyo waijua? Ukweli ni kwamba huijui, hata mimi sijui yajayo., ni siri!!! Najua Roho mtakatifu yeye hutujuza mengi tusiyoyajua, hilo sina shaka! Lakini ukisikia mgonjwa wa aina yoyote anahitaji kuombewa nawe, basi ondoa habari ya kusema nitamwendea kesho. Kwa sababu huna garantii ya maisha ya kesho, akifa leo usiku je, itakuwaje? Tena anaweza asife, lakini ni lazima ujifunze neno hili; “ linalowezekana leo lifanya leo, usisubiri kesho”. Ebu fikiri tena, Roho mtakatifu akitaka kufanya kazi sasa, je utasema ngoja baadae? Je hiyo kazi itafanyika baadae endapo umeizuilia sasa?

Siku moja, ndugu mmoja alitusihi wachungaji kwenda kumwombea bibi mmoja aliyekuwa amelazwa nyumbani. Nasi tulikuwa wachungaji wawili, tukafunga safari mara moja na kumwendea, kwa maana tunalijua jambo hili ya kwamba “mgonjwa haombewi kesho bali leo “ tulipofika tukamfanyia Bwana ibada katika nyumba ile, na kumwombea mgonjwa. Roho mtakatifu akatuongoza tumpake na mafuta kwa andiko la Yakobo 5:13-15. Tulipomaliza huduma, tulirejea ofisini kwetu. Muda si muda tukaambiwa mgonjwa amefariki. Sijui ilikuwa siku ya pili yake hivi, tukapata taarifa ya kufa kwake. Angalia mazingira kama hayo, utasema kana kwamba mgonjwa alikuwa akitusubiri sisi kwa kufanyiwa ibada ndipo afariki dunia. Sasa, jiulize kwamba ;endapo tungelaza damu na kusema tutakwenda kesho, je tungelimkuta hai? Umeona hapo!!!

Ukisoma vizuri huduma ya Bwana Yesu katika eneo hili, utagundua kuwa hakufanya makosa wala hakuchelewesha kumuhudumia mgonjwa yeyote isipokuwa alichelewa kwa Lazaro rafiki yake aliyekuwa hawezi ( Yoh. 11:6). Lakini mazingira haya yalikuwa yamebeba kusudi maalumu na ndio maana unaona Yesu akisema “ugonjwa huu, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. ” Yoh. 11:4 Hivyo Mungu mwenyewe alikusudia Yesu asiende kwa mgonjwa mara moja bali abakie pale pale ili kusudi la Bwana Mungu litimie. Sasa, usije ukakopi na kupesti kwamba na wewe utulie eneo moja hali unahitajika kwenda kumwombea mgonjwa ikiwa hujaambiwa na Roho utulie!!! Ikiwa umepata maaelekezo ya kuchelewa kutoka kwa Roho mtakatifu ni sawa, lakini ikiwa lah, basi usipoteze muda, wahi mara moja.

usiseme “ mimi sio mchungaji, siwezi kuombea mgonjwa, ngoja nimtafute mchungaji ” huku ukijua hali ya mgonjwa ni mbaya. Ni kweli unatakiwa umtafute mchungaji lakini kabla ya mchungaji kufika wewe uliye karibu na mgonjwa anza wewe kuomba kwa ajili yake, kisha mchungaji atafuatia. Kwa sababu unaweza ukaanza kumtafuta mchungaji, na wakati mchungaji anafunga safari kutoka huko aliko na mgonjwa akafa kabla ya mchungaji kufika alafu na wewe upo hapo hapo na mgonjwa, hapana!!! Anza wewe kwanza.

Kumbuka, hata kama mgonjwa si wa kufa lakini yafaa aombewe sasa na sio kesho. Kila jambo la Mungu ni sasa sio kesho nasema sasa, ni sasa! Jifunze kanuni mojawapo ya mwombaji, ambayo ni “ kuomba ni leo, sasa si kesho” ukiwa mwombaji huwezi kusema nitaomba wiki ijayo, au kesho, au baada ya siku kadhaa hapana! Ni leo ni sasa! Mara nyingi tumewakwamisha ndugu zetu kufika kwenye uzima kwa sababu ya kuhairisha maombi, badala sasa unamwambia nitakuja kesho nikuombee na Mungu amekukusudia wewe uombe sasa ili atende.

Maombi ya dizaini / namna hii hayahitaji ufike kanisani kwanza bali saa ile ile upokeapo simu ya mtu ambaye hawezi / mgonjwa basi, papo hapo mtamkie neno huku ukitafuta nafasi tulivu ya kumwombea vizuri. Mimi huwa siwaelewi walokole wenzangu ambao wanasikia aibu ya kutamka neno au kumwombea mgonjwa wakiwa kwenye daladala, au kituoni au sokoni, eti utawasikia wakisema “ sasa watanionaje, nikimtaja Yesu hapa, naogopa ” kha! Jamani!!! Kwani hao wanakupa kula? Wanakupa nini hata uwaogope kiasi hicho? Mimi ninakuambia leo, ikiwa utaogopa macho ya watu eti watakuonaje, basi wewe haufai kuitwa mkristo, wala haufai katika utumishi.

Nakutia moyo, wewe tamka neno, mwombee huyo mgonjwa katikati ya halaiki ya watu ikiwa ni kwa njia ya simu pokea kisha mtamkie neno na uombe kwa ajili yake. Lakini ikiwa unakaribia kufika eneo la utulivu iwe ni kanisani au nyumbani au eneo lolote, basi ni vyema ufike kwanza. Lakini ikiwa bado kana kana kaumbali hivi, basi endelea kutoa huduma ya kwanza papo hapo.

Ikiwa umepata kitu cha kujifunza, nijulishe kwa simu +255 683 877 900

What’s app ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Na Mch Gasper

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page