top of page

MFUNGO WA SIKU 40.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Biblia inatupa mifano ya watu wachache waliofunga kwa siku arobaini. Mifano hii inatuonesha kwamba suala la kufunga siku 40 linawezekana hata sasa kwa sababu ni Mungu yule yule aliyewasadia watu hao wakaweza na ndiye huyo huyo atakayekusaidia hata kuweza. Ni vyema kutambua kuwa,chochote kilichoandikwa kwenye biblia kimeandikwa ili wewe upate kujifunza,kuongozwa,kuadabishwa pamoja na kuonywa,tena kumbuka ; “kilichoandikwa kwa mfano,kinawezekana kwako leo,ukiamini tu“

“ Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.” Mathayo 4:2

Biblia inatueleza namna ambavyo Yesu alifunga siku 40 bila kunywa wala kula. Haikuwa rahisi jambo hili ndio maana hata mwishoe aliona njaa. Kitendo cha “ kuona njaa” kinatupa picha ya kuona uhalisia wa Yesu kwamba alikuwa ni mwanadamu 100%. ( ingawa pia alikuwa ni Mungu 100%). Ingawa funga ya Yesu ndani ya siku 40,ilikuwa ni funga ya bila kula wala kunywa chochote kwa siku hizo zote,kwa makusudi kukufundisha ya kwamba alikuwa pamoja na Mungu kwa maana hakuna linaloshindikana kwake Bwana. Biblia ingeliweza kunyamaza pale Yesu alipofunga siku 40 lakini haikunyamaza kwa kusudi la kuonesha umuhimu wa kufunga na kuomba. Tunaona “ ushindi ” alioupata Yesu dhidi ya shetani akiwa katika mfungo. Hii ina maana kwamba upo ushindi katika jambo lolote lile,liwe jaribu au chochote kwa mtu aliyekuwa kwenye mfungo na maombi ya kina.

Lakini kumbuka jambo moja,Yesu alipokuwa kwenye mfungo wa siku 40 kavu,ndipo mjaribu shetani alimfuata ili kumjaribu. Kile ambacho alichokusudia ibilisi ni kumwangusha. Na hali ndivyo ilivyo hata leo,kwa maana pale utakapofunga siku zote hizo,ujue kabisa mjaribu ni lazima atakujia kwa lengo la kukutoa kwenye kusudi la Mungu…Mfungo wa siku 40 ni aina ya mfungo wa kukamia maombi mbele za uso wa Bwana. Siku hizi ni nyingi lakini ni chache sana kwa maana Roho akiwa nawe utajikuta ukizimaliza kama maji vile!

  1. Mfungo wa siku 40,ni mazoezi ya kiroho mwanzoni mwa mwaka mpya.

Hapo zamani mwanzoni mwa mwaka,wafalme walikuwa wakitoka kwenda vitani ( 2 Samweli 11:1). Jambo hili lilikuwa desturi yao. Leo hii,mwanzo wa mwaka mpya,hatutoki na kwenda vitani ila tupo vitani katika ulimwengu wa roho kila siku. Hii ina maana tunatakiwa kupigana kiroho kila siku. Na moja ya silaha yenye nguvu katika vita tuliyonayo na maombi hasa maombi ya kufunga. Mfungo wa siku 40 ni mazoezi ya kupanda kiroho sana. Na mazoezi haya huchukuliwa hasa mwanzoni mwa mwaka mpya.

Wakati watu wengine wanapanga mipango yao ya mwaka mpya,waende wapi kustarehe!,wewe unapaswa kupanga mipango yako ya kiroho katika mfungo wa siku 40,kwamba ufanye nini upande kiroho. Pengine unatamani sana ukue kiroho,au unatamani sana uwe mtu wa rohoni ( uweze kusikia na kuona kile atakacho Mungu kwenye huduma / kazi / familia yako),na hapo huna budi kushuka mbele za Bwana kwa mfungo wa siku 40 kama maandalizi mazuri ya kufikia malengo yako ya kiroho. Ebu jifunze kwa mtu aitwaye Musa mtu wa Mungu. Yeye naye alifunga siku 40 mchana na usiku,biblia inasema;

“Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.“ Kutoka 3yako.

Ingelikuwa ni akili za Musa kama Musa,basi ukweli ni kwamba asingeliweza kuandika yale aliyoyaandika ndani ya siku 40,bali Mungu alikuwa naye. Na ndio ufahamu ya kwamba ukifunga siku arobaini ijapokuwa kwa kula jioni,Mungu hawezi kukuacha,bali atakuwa pamoja nawe. Biblia inasema Mungu alimpa maneno ya kuandika. Leo hii ukifunga kwa muda mrefu wa siku arobaini, ujue kabisa Mungu atakupa neno / maneno yake,yakuongoze kwenye maisha yako.

Biblia inazidi kueleza kile kilichotokea pale Musa alipofunga siku 40 kisha aliposhuka mlimani,kwamba “ngozi ya uso wake / paji la uswengine hii ina maana, Musa alifunikwa na upako wa Bwana. Sasa nguvu/upako wa namna hii ulitoka wapi? Bila shaka biblia imejibu vyema,kwamba ni kwa sababu Musa alikuwa akisema na Mungu kule mlimani kwa zile siku 40. Hali hii ndiyo ilivyo hivyo hivyo leo,pale utakapoamua kuongea na Mungu ndani ya siku arobaini, ujue hutakuwa wa kawaida. Ebu fikiri,hata akina Haruni na waisraeli wote walishindwa kumtazama kwa sababu ya kung’aa uso wake. Ukitoka mlimani mpendwa,ni lazima utan’aa tu kuonesha kwamba wewe si wakawaida sasa.

Mtu mmoja nilikuwa nikiongea naye na kumwambia kwamba unahitaji kufunga siku 40 kwa kufungulia jioni, akasema “Eeeh yaani mimi siwezi kabisaa!!” sikushangaa sana,kwa sababu watu wengi huogopa wanapotaka kufanya jambo la kiroho. Lakini nimemtia moyo na kumwambia kwamba, inawezekana kabisa kufunga siku arobaini ingawa si kama funga ile aliyoifanya Musa bila kula wala kunywa kabisa.

  1. Mwaka mpya,siku 40 za mfungo ni zako.

Ni lazima sasa uchukue hatua ya kufunga siku arobaini zote,kitendo hiki kinakusogeza karibu na Mungu hasa mwanzoni mwamwaka mpya. Kumbuka; Unataka Mungu akufanyie nini kipindi chote cha mwaka mpya? Unataka kuona nini kipindi chote cha mwaka mpya? Hivi ni kiu gani iliyopo ndani yako ambayo unatamani Mungu afanye kwa kipindi chote cha mwaka mpya? Ikiwa jibu ni ndio,basi huna budi kungangana na mfungo wa siku 40. Na unaweza kabisa. Labda swali unaloweza kuwa nalo sasa “…nitaombea nini siku zote hizo,? Mbona nitakaukiwa maombi,maana ni nyingi...” . Jibu lake ni jepesi kabisa,; maombi yapo mengi sana kiasi kwamba siku hizo ni chache mno. Mfano kitendo cha kumshukuru Mungu kinaweza kuwa wiki nzima tena hata wiki ni chache ukilingalinisha na yale aliyokutendea Bwana. Lakini pia yapo maombi ya toba,yapo maombi ya kuvunja hila za adui N.K

Unaweza ukaukamia mwaka mpya kuingia kwenye maombi mazito kwa ajili ya huduma yako. Ifike wakati utembee na Mungu kikamilifu,na hapo lazima ujitoe mhanga kwa maombi ya namna hii. Ebu angalia mambo yalivyofunga mpaka sasa kwenye kazi yako,kwa nini usichukue muda wa maombi kikamilifu kwa mwaka mpya? Iko nguvu ya Mungu ndani yako, ikiwa utaitumia,nakwambia utashangaa matokeo yake yatakavyokuwa.

Ukweli ni kwamba kuna nguvu sana tena ya ajabu katika mfungo wa namna hii. Inawezekana hukuwahi kufunga hivi,basi anza leo,anza sasa. Na utajikuta yale wanayoyazungumza wenzako waliofanya,nawe utayazungumza na kumshuhudia Bwana.

Ikiwa kama umejifunza kitu hapa,nifahamishe. Pia kwa huduma ya maombezi nipigie sasa kwa +255 6683 877 900

Whatsapp namba ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page