top of page

MBIO ZA IMANI. ~01

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Kwa kuwa mwaka huu 2019 ni mwaka wa ushindi,hivyo ni vyema ukajua kwamba ili ushinde ni sharti kwanza uwe kwenye mashindano. Ukweli ni kwamba hata sasa upo kwenye mashindano dhidi ya falme na mamlaka,dhidi ya wakuu wa giza hili,dhidi majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Hivyo itapendeza sana ujue mashindano yetu ni ya namna gani. “mbio za imani” ndio haswa mashindano tuliyonayo hata sasa.

  1. Lengo kuu la mashindano tuliyonayo,ni kupata ushindi.

Katika Yeremia1:19, biblia inasema “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe.” Neno limeweka wazi kwamba wapo watakaokuwa washindani wako,au watakaopigana nawe,lakini habari njema ni kwamba hawatashinda kwa sababu Bwana yu pamoja nawe ( Bwana yupo upande wako). Hivyo utagundua vita au mashindano ni lazima viwepo,lakini ikiwa Bwana atakuwa upande wako;hawatakushinda.

Ninapata shida na wahubiri wa leo,wale wanaohubiri kwamba “hautakuwa na vita,wala mashindano ya namna yoyote kwa maana wewe u mwana wa Mungu “ Mhh!!!! Biblia haisemi hivyo bhana ! bali inasema vita vitakuwepo,mashindano yatakuwepo,lakini utashinda katika hayo kwa sababu Bwana yupo upande wako, hivyo ndivyo biblia isemavyo.Vita lazima viwepo,na kushindana ni lazima kuwepo,lakini na ushindi ni lazima uwepo,Je una amini hivyo?

Mwanariadha wa mbio ndefu anapoanza safari yake ya kukimbia anajua fika kwamba lazima akutane na vikwazo vingi katika safari yake,vikwazo kama kuanguka, kuchoka hata kuishiwa nguvu,vichomi vya gafla, kukatishwa tamaa, hali ya kukinzana na nguvu ya upepo n.k Lakini katika vyote hivi,mkimbiaji akinguka atainuka mara moja na kuendelea na safari yake huku moyoni mwake akitarajia kushinda hata kama yupo mwisho mwisho,hata hapo ataendelea kutazamia taji.

Yupo mwanariadha mmoja maarufu sana katika mbio za imani. Yeyote ambaye ni mwana michezo wa imani hawezi kukosa kumjua mwanariadha huyu. Huyu si mwingine bali ni yule ambaye yeye ndiye mwanzilishi wa mashindano haya. Huyu ni Yesu,ambaye anasema “ Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” Yoh.16:33 kile asemacho Bwana, ni kwamba katika mbio zetu,kuna dhiki kubwa,kuna kuchoka pia,lakini katika hayo yote endeleeni kujipa moyo ( vumilieni mkiichuchumilia taji ya uzima) kwa maana Yeye alishinda katika yote hayo,naye ndiye sasa anatuongoza,kwa kuwa hakuna kikwazo katika mbio za imani alichokishindwa!

Lakini si hivyo tu bali Yesu alishinda zaidi ya kushinda.katika hili tunamtazama Yesu kama Yeye aliyezishinda mbio hizi. Paulo ni miongoni mwa wana mbio wa imani, Paulo anasema “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;” 2 Timotheo 4:7. Paulo anajaribu kusema nasi ya kuwa kuna vita alipigana,lakini si vita ya kimwili bali ya kiroho. “ mwendo nimeumaliza” neno hili hueleza kusudi halisi la Mungu ambalo Paulo alipewa,naye alimaliza kile alichopewa na Bwana. Mbio za imani za Paulo hazikuwa za kawaida kawaida,zilikuwa ni mbio zilizojawa na changamoto nyingi kwa kadri ya kiwango chake cha imani.

Hata hivyo,mwandishi wa kitabu cha Waebrania kwenye sura ya 11 yote inatueleza kuhusu “ imani” na si imani kama imani bali imani hasa katika matendo. Majasiri wa imani katika nyakati tofauti tofauti,mtu kama

  1. “Habili ” ambaye kwa imani alipiga mbio katika matoleo naye akatoboza katika eneo hilo,akahesabiwa haki.

  2. “Henoko“ambaye alipiga mbio za imani,akaenda na Mungu naye akatwaliwa vyema katika mbio zake.

  3. “Nuhu” ambaye alitembea na Mungu,akapiga mbio za imani,ambapo Mungu alimfunulia mambo yasiyokuwepo lakini hayana budi kuja,akatengeneza safina,akawahubiria watu,naye akaokoka.

  4. “ Ibrahimu” aliyezipiga mbio za imani kutoka kwenye nchi ya baba yake na kwenda asikokujua. Akaa huko pamoja na Isaka na Yakobo.Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

  5. Na wengine wengi kama vile Wafalme ( Daudi), Gedioni,Yefta,waamuzi ( Samsoni,Debora,n.k) n.k.

Watu wa namna hii,walitembea na Mungu kwenye mbio za imani katika nyakati tofauti tofauti….

ITAENDELEA…

Kwa msaada zaidi na mengineyo piga kwa +255 683 877 900

Na Mch.G. Madumla.

What’s app +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page