MBIO ZA IMANI -02 (Tamati)
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 8, 2019
- 2 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania 12:1-2,anajaribu kuweka hitimisho la sura ya 11 baada ya kuwataja watu majasiri wa imani ambao walihesabiwa haki kwa njia ya imani.Majasiri hao,akiwaita “wingu la mashahidi”. Akituonesha ni nini tunatakiwa kufanya ili tuweze kushinda mashindano yetu ya mbio za imani. Bila shaka,anatoa kanuni muhimu za ushindi wa imani katika kila hatua ya maisha yako,biblia inasema;
“ Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele ” Waebrania 12:1-2
Hivyo,ni kana kwamba wewe na mimi tupo kwenye uwanja wa kukimbia tukitazamwa na mashahindi wengi waliomaliza mbio zao.Kama ilivyo kawaida ya kutafuta kushinda kwenye mashindano yoyote,kuna kanuni au taratibu zipelekeazo ushindi. Na ndivyo ilivyo katika mambo ya kiimani,kuna taratibu za kuchukua ili tuweze kushinda. Maandiko hayo yanataja taratibu 4 muhimu za ushindi,nazo ni:
01.Weka kando kila mzigo mzito.
Mkimbiaji hawezi kushinda ikiwa kama atakimbia pamoja na mzigo,kwa maana atachoshwa mapema na ule mzigo alioubeba,na ndio maana hata nguo za wakimbiaji ni nguo maalumu,ili kupunguza mzigo.Katika mbio za imani ni vivyo hivyo,hutakiwi kubeba mzigo wa aina yoyote. Mzigo unachosha kiasi kwamba hutaweza kukimbia kwa uhuru. Kama mkimbiaji wa mbio,akishinda huku akiwa amebeba mzigo mzito,labda tuseme awe amebeba mfuko wa cement wa kilo 50,halafu kashinda mbio ndefu,basi itakuwa maajabu ya dunia kwa maana mzigo hukwamisha mbio. Mzigo wa mbio za imani waweza kuwa (01. Mapokeo ya dini/sheria na taratibu za kimapokeo Mathayo 23:4,Wakolosai 2:8,02.Hali ya mashaka/kutokuamini n.k)
02. Shughulikia dhambi ikuzingayo upesi – Warumi 7:21
Dhambi nayo ni mzigo wa kukwamisha mbio za imani. Lakini ipo dhambi ambayo mara kwa mara inakuzinga,hiyo dhambi lazima ishughulikiwe kwanza ili uwe huru katika mbio zako za imani unazozipiga sasa. Jiulize ni eneo gani unaloanguka dhambini haswa mara nyingi? Je ni dhambi gani ambayo umekuwa ukiitenda mara kwa mara? Jaribu kumwona mchungaji wako mapema,mkae na aishughulikie hiyo dhambi.
03.Piga mbio kwa saburi.
Katika mashindano ya imani “uvumilivu” ni jambo la muhimu sana ili uweze kushinda. Kuelekea kwenye ushindi juu ya lolote,unahitaji kuwa mvumilivu. Kumbuka,mbio za imani ni mbio ndefu,zenye kukatisha tamaa,zenye ukinzani mkubwa wa kila namna. Katika hayo yote,uvumilivu ni daraja muhimu sana. Katika mbio za imani kwenye eneo la ndoa yako,lazima uwe na uvumilivu ili ushinde.
04. Mtazame Yesu mwenye kuanzisha mashindano ya imani.
Kila unalopitia ni moja la shindano lako la imani,na ili ushinde katika hilo ni lazima umtazame Yesu. Usiende kulia wala kushoto bali kazi tu kwa Yesu maana hapo ndipo kwenye ushindi wako. Jifunze kwa Petro aliyetembea kwenye maji kidogo lakini alipotazama mbali na Yesu alianza kuzama. Watu wengi wanaanguka sio kwa sababu hawana imani bali kwa sababu ya kuamisha macho yao kwa Yesu. Kumbuka tena,hakuna jambo lolote utakalopitia leo asilolipitia Yesu. Yeye alipitia yote,zaidi ya hayo ya kwako na katika yote hayo alishinda (Yoh.16:33). Naye ndiye wa kutazamwa. (mambo hayo manne yametajwa katika Waebrania 12:1-2)
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe pia kwa msaada zaidi na mengineyo piga kwa +255 683 877 900
Na Mch.G. Madumla. What’s app ni+255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments