MAOMBOLEZO – KIFO CHA DEBORA
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 8, 2018
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Unamkumbuka Rebeka mke wa Isaka ? Bila shaka inawezekana hamkumbuki, ngoja nikukumbushe kidogo. Ibrahimu baba wa imani alikuwa na mtoto wa agano aitwae Isaka. Isaka ndiye aliyekuja kumuoa mjukuu wa Nahori, aitwae Rebeka binti Bethueli. Kilikuwa ni kipindi kifupi baada ya Isaka kufiwa na mama yake, ndipo Isaka alipomtwaa Rebeka kuwa mke wake.
Neno la Mungu linasema kwamba “… Isaka alifarijika baada ya kuoa ” Mwanzo 24:67. Unajua ni kama vile Isaka aliuona uso wa mama yake Sara aliyefariki pale alipomwangalia mkewe;inaonekana Rebeka alimpa kampani ya kutosha Isaka kana kwamba, Isaka hakujiisi mpweke.
Kumbuka tena kile kipindi ambacho Rebeka alipokuwa ameposwa na Isaka kwa mikono ya mtumishi Eliezeri ( Mwanzo 24:2-9), baada ya kumaliza shughuli zote za mambo ya ndoa kwa taratibu za kipindi kile, sasa Rebeka akatwaliwa kwao kwenda kuanza maisha mapya na Isaka kama mume na mke.
Kumbuka;Rebeka binti Bethueli; alipotoka kwenye nyumba ya babaye, hakuondoka peke yake bali aliondoka na vijakazi kadha . Mmoja kati ya vijakazi wake aliyetoka naye alikuwa ni Debora, huyu alikuwa ni “yaya wake” Mwanzo 24:59. Neno hili “ yaya” lina maana ya “ Mdada mwangalizi, mhudumu wa karibu, kiingereza huitwa a nurse”. Hivyo huyu Debora alimuhudumia Rebeka tokea huko nyumbani kwa babaye Labani ( baba yake Rebeka) ( Debora alikuwa mlezi wa Rebeka)
Leo hii mtu aitwae “ yaya ” anaweza kufananishwa na mdada wako wa kazi ambaye anakazi ya kukusaidia kazi zako za nyumbani pale weww unapokuwepo au usipokuwepo. Ninajaribu kumfananisha na mtu wako ambaye kwa kweli anakuhudumia kwa ukaribu mambo ya familia yako, watoto n. k. Debora alikuwa ni yaya wa Rebeka ( Mwanzo 24:59.) Lakini akina Debora (mayaya) wa leo ndio tunawatukana, tunawadharau hata wamejikuta wakiitwa majina ya ajabu ajabu
“ mara ohh beki tatu, mara ooh gori kipa, mara ooh washamba, mara ooh hawajasoma.… 🏃🏃🏃🏃” sasa jiulize kwa nini unamdharau mtu ambaye kwa kweli anakutunzia nyumba yako, watoto wako pale usipokuwepo? Kwa nini unamdharau mdada wa kazi na kumwona kana kwamba hana akili hata wakati mwingine haumlipi mshaara wake inavyotakiwa? Ujue ni dhambi hiyo, na Mungu anakuona, ohoo!!
Debora kama mfanyakazi wa ndani wa mambo ya Rebeka aliheshimika. Alikuwa kama mama mlezi wa Rebeka. Katika safari yote, alikuwa pembeni mwa Rebeka akimuhudumia. Ni nadra sana kwa mwanamke kutajwa kimatukio kwa taratibu za kiyahudi, na ukiona katajwa basi ujue kulikuwa na jambo muhimu sana la kujifunza kupitia huyo mwanamke. Debora alikuwa mmoja wao wa kutufundisha namna ya kuwachukulia watumishi wa ndani / wadada au wakaka wa kazi za ndani ambao leo tunawaajili kwa lengo la kusaidia kazi za nyumbani pamoja na kuwaangalia watoto wetu.
Katika safari za Rebeka pembeni alikuwepo Debora, na ikafika wakati Debora akafariki kipindi Yakobo alipokuwa safarini na kutuama huko “Luzu” katika nchi ya Kanaani ( Mwanzo 35:6). Ingawa biblia haituoneshi kifo cha Rebeka mke wa Isaka, maana inawezekana alifariki mapema kabla ya kifo cha Debora na ikiwa ndivyo basi ni dhahiri kabisa Debora alikuwa na nafasi muhimu sana kwa Yakobo. Yakobo alimwona Debora kama mama yake, hivyo ndipo maombolezo makubwa yakafanyika.
“ Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi.” Mwanzo 35:8
Neno “ Alon-bakuthi” maana yake ni mti wa maombolezo. Hii ni kuonesha kwamba kulikuwa na maombolezo makubwa kufuatia kifo cha Rebeka. Si hali ya kawaida kabisa kufanyika maombolezo ya namna hii kwa “ mdada wa kazi” lakini ndio walifanya. Biblia hajawahi kurekodi maombolezo makubwa kwa mwanamke tena ni mdada wa kazi mahali popote isipokuwa kwenye kifo cha Debora. Hata akina Sara, Rebeka na wengineo hawakufanyiwa kama Debora. Hii inaonesha jinsi gani Debora alikuwa ni muhimu sana. Jifunze hapo, kuwatendea wadada wa kazi kwenye kiwango cha juu kama Debora.
Leo unaweza ukaambiwa kwamba “… mdada wako wa kazi wa kipindi kilee ulipokua ukianza maisha, kafariki juzi tu na msiba upo kwao huko Iringa,.. ” alafu cha ajabu nawe ukasema “ sasa mimi inanihusu nini, kama kafa si basi bhana, kwanza mimi simkumbuki” hizo zinaitwa “nyodo! / dharau” eti kwa sababu umepanda kidogo kimaisha na kujifanya umemsahau mdada wako wa kazi, mtu ambaye alikusaidia sana kipindi unaanza maisha. Hivi kweli unaweza kumsahau mtu wa namna hii ambaye amekulelea watoto wako, mpaka leo watoto wako wamekua. Hivi kweli umefikia wakati unashindwa hata kwenda msibani na kuchangia mchango mkubwa, kwa sababu tu eti huyo mdada alikwisha ondokaga? Haa jamani vibaya hivyo, Jifunze kwa akina Yakobo walipofiwa na Debora.
Hivi nikuulize leo, kwa nini unamdharau mdada wa kazi? Unafikiri Mungu hakuoni? Kumbuka na yeye ni mwanadamu kama wewe, anamahitaji kama yako. Anapenda kula, kuvaa vizuri ; anahitaji kwenda kanisani pia unapoenda wewe. Lakini cha ajabu huyo mdada umemweka daraja la mwisho kabisa kwenye kila kitu. Hivi mimi najiuliza sana swali hili “ yupi mtu wa thamani kwako, Je ni rafiki yako au mtu anayekutunzia watoto wako kipindi chote unapokuwa kazini? “ Nafikiri mtu muhimu sana ni yule anayekutunzia watoto wako kwa kweli.
Siku mmoja kitasa cha mlango cha nyumba ya mama mmoja kiliharibika. Na ikamlazimu kutafuta fundi wa kutengeneza mlango wake. Fundi alipokuja alimtazama yule mama, kisha akamtajia bei ya kutengeneza kile kitasa cha mlango. Bei yake yule fundi ilikuwa “inapendeza” ilikuwa bei ya juu tofauti na kazi yenyewe. Lakini kwa sababu yule mama hakutaka kulala mlango wazi, ikamgalimu kukubaliana kumlipa fundi kwa bei ile ile.
Sasa, mdada wa kazi alikuwepo hapo hapi kwenye mapatano ya kutengeneza mlango. Mdada wa kazi, alishangaa kuona kazi ndogo malipo makubwa akilinganisha na kazi aifanyayo ya kuangalia nyumba na watoto wa yule mama na kuwapikia, kuwafulia, n. k kwa kila mwezi, alafu kamshahara kaduchu / kadogooo.
Jamani inaumiza sana hili!!! 😭😭😭 Hivi jiulize kipi hapo cha maana sana, mlango au watoto na nyumba nzima? Sasa kwa nini tunawasahau hao watu muhimu wanaofanya kazi kutwa nzima, na kuwalipa kwa manyanyaso tena wakati mwingine hakuna malipo kabisa mpaka waandamane ndipo ulipe!!!! Kumbuka na wao wanafamilia wameziacha nyumbani kwao. Sasa ikiwa Mungu amekubaliki kwa kazi uifanyayo kwa nini na wewe usifanyike baraka kwa mdada wako wa kazi kwa kumuhudumia vyema.
Wakati mwingine utakuta mdada anakosa hata nguo za ndani, anakosa hata vitaulo vya usafi katika siku zake, na wewe mama unayajua hayo, lakini kimya! Unajikausha, eti kwa sababu sio mwanao. Je kwa binti yako unaweza kumfanyia hivyo? Ikiwa huwezi basi usimfanyie huyo binti wa watu.
Na shida hizi zipo kwa wamama sio wababa, alafu cha ajabu ndio hao hao wanaosema “ nimeokoka nampenda Bwana ” Weeh muogope Mungu wako! Hakuna kumpenda Mungu kwa staili hiyo ndugu, Badalika bhana! Kumbuka neno hili alilolisema Bwana “ Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.” Mathayo 7:12
Kwa msaada zaidi pamoja mashauri, maombezi +255 683 877 900
Mch. Gasper Madumla.
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
コメント