MAOMBI / PRAYERS~3
- Mch. Gasper Madumla
- May 21, 2016
- 4 min read

Na mchungaji Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
03.Tunaomba kwa sababu ya kuimarisha imani zetu.
Kumbuka Neno la Mungu ni mbegu ( Luka 8:11),Na maombi ni maji.Hivyo kama vile mbegu isivyoweza kukua bila maji ndivyo ilivyo imani yako haiwezi kukua bila maombi. Kwa kuwa tunahitaji kukua kiimani basi hatuna budi kuomba mara kwa mara;maombi hupandisha imani kwa kiwango kikubwa,tazama mfano huu;
Inawezekana unamwamini Yesu katika uponyaji kama wengine waaminivyo,lakini kule kuamini tu hakutoshi ni lazima uchukue hatua ya kumuomba,angalia jambo hili kwa wanafunzi wake Yesu jinsi ilivyokuwa; `` [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Mathayo 17:21 & Marko 9:29. Hao wanafunzi walimwamini Yesu kama unavyomwamini wewe,lakini bado walihitajika waombe. Hapo utagundua imani ni muhimu sana kwa maana twaokolewa nayo,lakini kuomba ni muhimu pia. Kuomba kunaithibitisha hiyo imani.
Tazama hapo (Mathayo 17:14-21),wanafunzi wa Yesu walimuamini Yesu,lakini kilichokuwa kimepungua ni nguvu ya maombi ya mara kwa mara na mifungo. Na kwa sababu maombi huimarisha imani,hivyo kama yatakosekana kwako basi ni dhahiri kabisa kwamba hautakuwa na imani iokoayo,utakuwa na imani haba kama vile hao wanafunzi walikuwa na imani haba.
Ukiwa ni muombaji mzuri,basi kiwango chako cha imani hupanda kiasi kwamba yale yote magumu unaanza kuyaona mepesi. Mahali ambapo wenzako hawaoni njia bali wewe waiona kwa imani kwa sababu wewe ni muombaji.
Mimi nakumbuka,wakati fulani nalikuwa ninaaomba na wenzangu katika maandalizi ya mkutano wa nje. Kisha maombi yangu yakanipandisha imani kiasi kwamba nikasema hata kama kuna mchawi yoyote yule nataka aje kwangu nionane nae kwa macho ya damu na nyama,tuone atanifanya nini mimi mwenye nguvu za Mungu.
Wenzangu nao ndio kabisaa maana wao walisema akija tutampiga na mateke mpaka akome kuloga. Lakini imani yote ya ushindi ilijengwa katika maaombi. Hivyo basi maombi yana sehemu kubwa ya kukuza imani yako.
04.Tunaomba kwa sababu ya kupata udhihilisho wa nguvu za MUNGU.
Udhihilisho wa kiungu umefichwa katika maombi. Hata silaha zote za Mungu zimefichwa katika maombi,hii ni sawa na kusema ukitaka kuona uweza wa kiungu,kuona upako huna budi kuwa mwombaji. Unajua Huduma zetu haziwezi kusonga mbele kama zitakosa nguvu za MUNGU.
Tuangalie mfano huu;Luka 22:40-43.
“ Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.” Luka 22:43 Yesu alitiwa nguvu wakati alipokuwa akiomba. Si kana kwamba hakuwa na nguvu bali aliongezewa nguvu za kuukabili msalaba. Hii inadhihilisha kwamba Mungu hutia nguvu watu wake ambao wanajiandaa kukabili msalaba,lakini nguvu hizo zinaachiliwa katika maombi. Ukweli ni kwamba tunahitaji nguvu za kusonga mbele,ukiwa na tabia ya kuomba mara kwa mara ujue sehemu ya nguvu itakuwa yako.
05. Tunaomba Kwa sababu tupo vitani wakati wote.
Ufahamu kwamba maisha yako ni vita siku zote dhidi ya nguvu za giza,wafalme na wakuu wa giza. Ukifahamu hilo,huwezi kuwa kimya bali utasimama na kuomba. Vita yetu ni kubwa,hasa kwako wewe uliyeokoka,kwa maana kuokoka ni kutangaza vita dhidi ya wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho. Pona yako ni kuomba tu. Na salama yako ipo hapo katika maombi ya mara kwa mara. Na ndio maana Paulo anasema “dumuni katika kuomba” Wakolosai 4:2
Neno linatuambia tena“ Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” Yakobo 4:7 Moja ya njia kubwa ya kumpinga shetani ni kuomba. Na ukimpinga sawa sawa,ni lazima akukimbie tu maana Neno la Mungu ndivyo lisemavyo hivyo. Usipompinga,hawezi kukukimbia. Ukweli ni kwamba kama humtaki shetani na mawakala wake,basi huna budi kumpinga kwa kuomba.
06.Tunaomba kwa sababu sisi tu miungu,tunaendelea kuumba.
Ni ukweli usiopingika kwamba maombi ni njia ya kuumba vitu visivyoonekana na hata vile vionekanavyo. Mfano tazama pale unapopitia katika udhaifu wa mwili kwa sababu ya magonjwa,hapo ukiomba unaiumba afya iliyotoweka sasa unairejesha kwa upya,kuifanya iwe nzuri tofauti kabisa na vile ulivyo.
Yapo mambo mengi yaliyokufa katika maisha yetu,lakini kwa njia hii ya maombi tunayafufua na kuyaumba tena. Mfano; inawezekana ukaitengeneza nyumba yako vile utakavyo wewe katika maombi,hali wewe huna hata kiwanja.
Lakini ukamuomba MUNGU huku ukiiona nyumba yako katika ulimwengu wa roho jinsi itakavyokuwa hapo baadaye. Yaani twaweza kuumba vitu vingi ambavyo kwa sasa havipo kabisa. BWANA MUNGU ametuheshimisha mno,hata kutupa uwezo huu,wa kushiriki uumbaji kwa maana tu miungu.
Je nini asili ya maombi?
Ulikuwa ni utaratibu wa Mungu kama Baba kuzungumza na watoto wake pale bustanini Edeni,Mazungumzo yao yaliimalisha uhusiano wao. Bwana alimjua mwanadamu zaidi kwa maana Yeye ndiye aliyemwuumba,Alijua kwamba mwanadamu hawezi maisha bila Yeye Mungu. Hata pale mwanadamu alipoasi na kuvunja uhusiano huo,bado Mungu alimtafuta mwanadamu kwa lengo lile lile la kurudisha uhusiano wao wa mazungumzo. Akamwuuliza “Adam upo wapi?” -Mwanzo 3:8 . Mungu hakuchoka kurejeza mwanadamu katika uhusiano wake wa kwanza,hata ikafika akaweka mpango wa kumkomboa mwanadamu – Mwanzo 3:15. Hivyo asili ya maombi imetoka kwa Mungu mwenyewe.
Kumbuka;
Baada ya anguko,Watu wakaongezeka ulimwenguni, Maombi yakakauka kwa muda fulani. Lakini kipindi ambapo Adamu alipomjua mke wake tena alimzaa mwana mwanamume akamwita Sethi. Sethi naye akazaa mwana akamwita Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuendeleza maombi. Mwanzo 4:26
Biblia imetaja kwamba eneo hilo ndilo eneo la kwanza kabisa ambapo watu wameanza kuomba baada ya yote kutokea katika anguko la dhambi ya akina Adamu. Hivyo tokea hapo tunaona maombi yakianza tena,na kuendelea mpaka katika ujio wa Yesu,mpaka leo hii. Hii ndio asili ya maombi.
ITAENDELEA…
Kwa huduma ya maombi na ushauri wa bure,nipigie sasa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments