MAOMBI / PRAYERS~06
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 22, 2016
- 2 min read

Na Mch.Gasper Madumla.
(III) MAOMBI YA TOBA / REHEMA.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi..
Maombi haya ni muhimu sana kwa kuwa yanaonesha ubinadamu wako mbele za Mungu kwamba umekosea na unaomba msamaha. Tunaweza kusema kwamba haya ni maombi ya kujinyenyekesha mbele za Bwana na kuonesha udogo wako mbele za Mungu. Rehema za Mungu zipo maana Neno linasema kwamba Yeye Mungu yupo tayari kusamehe unapotubu,lakini angalizo ni moja tu,ni hili: usifanye dhambi kwa makusudi kwa kutegemea rehema za Bwana! ( Warumi 6:1)
Maombi ya toba yanapaswa kufanyika mara kwa mara,hasa pale unapoona kwamba umemtenda Mungu dhambi. Nakumbuka;
Siku moja katika ibada zetu,mchungaji kiongozi aliuliza swali kwa kanisa zima ( haswa kwa wale waliokuwa wameokoka) kwamba;ni nani ambaye hajadanganya kabisa tangu alipookoka? Anyooshe mkono! Ukweli ni kwamba hakuna aliyenyoosha mkono hata mtu mmoja hapo kanisani. Pamoja na kwamba tulikuwa tumeokoka,lakini kumbe tumeshadanganya sana. Hali hii inaonesha kwamba sote tulitenda dhambi,ingawa tulioshwa,tulitakaswa kwa njia ya toba. Nikajifunza kitu,kwamba kumbe mara nyingi huwa tunakosea na kutenda dhambi ingawa tumeokoka. Hapo sasa umuhimu wa maombi ya toba unachukua nafasi yake. tafakari sasa Neno hili ; (1 Yoh.1:8-9)
Ni kweli nakubali kwamba hatuwezi kuacha dhambi kwa kutumia akili zetu za kibinadamu bali tunaweza kuacha dhambi na uovu wote kwa msaada wa Roho mtakatifu. Lakini ni lazima wewe mwenyewe uchukue hatua madhubuti ya kuamua kuacha dhambi huku ukimuomba Roho mtakatifu akusaidie.
Bwana Mungu hapendi mtu apotee bali sote tufikilie toba.( 2 Petro 3:9). Mungu hapendi wewe upotee katika dhambi hiyo uifanyayo mara kwa mara bali anataka leo ufikirie kutubu na kuamua kuacha. Haijarishi ni dhambi ya namna gani,kwa maana kwake MUNGU yote yanawezekana.
Yeye Mungu aweza kukuondolea leo hiyo kiu ya dhambi,maana anasema wale wote wenye kiu ya dhambi waende kwake naye ataikata kiu hiyo na kukupea kiu ya Kwake (Isaya 55:1-2)
Je nini haswa asili ya toba na rehema?
Asili ya toba ni pale dhambi ilipoingia ulimwenguni. Kwa maana twatubu kwa sababu ya uwepo wa dhambi. Hali ya kiroho ya mwanadamu wa kwanza kabla ya dhambi ilikuwa sawa na hali ya Mungu kwa maana wote walikuwa rohoni,lakini Mungu ni Mungu na mwanadamu ni mwanadamu kwa kuwa Mungu Yeye hakuumbwa bali mwanadamu aliumbwa. Baada ya dhambi kuingia ulimwenguni,mwanadamu akapoteza mfanano aliokuwa nao hapo awali (Mwanzo 3:9)
Je kutubu ni mpango wa MUNGU?
Mpango wa Mungu sisi sote tuokoke na kuifahamu hiyo kweli (1 Wathesalonike 2:3-4),na kuishi katika utakatifu kama Yeye alivyo mtakatifu (1 Petro 1:15). Lakini pale tunapogundua kwamba tumemwacha Mungu kwa namna yeyote ile,basi yatupasa kurejea kwa njia ya toba / kugeuka kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi
Watu wengi ulimwenguni leo wamekwama katika eneo la kutosamehewa dhambi zao kwa sababu ya wao wenyewe kushindwa kuwasamehe wakosa wao.( Mathayo 6:14-15) Hili ni tatizo kubwa sana,kwa maana ukiwa unatubu ni lazima ukumbuke kuwasamehe wengine kwanza na kuwaachilia kutoka moyoni kisha sasa ndio usamehewe na wewe. Usisahau hilo hata kidogo. Ukiwa una neno na nduguyo,patana naye kwanza kabla hujaenda madhabahuni.( SOMA ZAIDI KWENYE SOMO LA TOBA)
Ikiwa umetubia dhambi lakini bado kila siku unairudia kuitenda hiyo hiyo,emu nipigie simu tuombe pamoja inawezekana tukaomba pamoja na ukatiwa nguvu ya ziada; piga kwa namba hii +255 655 11 11 49 / 0683 877 900.
ITAENDELEA…
Mch.Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comments