MAOMBI / PRAYERS~04
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 13, 2016
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
(i) Kwa nini tunaomba kwa Jina la Yesu?
Ni utaratibu wa Mungu kutupatia Jina la Yesu ili sisi sote tuombe kwa jina hilo kwa maana Mungu ni wa utaratibu,na ndivyo itupasavyo kufanya mambo yote katika uzuri na utaratibu ( 1 Wakorintho 14:40). Biblia inasema hivi : “ Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ” Matendo 4:12
Hilo ndilo Jina lipitalo majina yote. Nataka uelewe kwamba ni jina hilo tu la Yesu kila kitu hutiishwa. Tunafahamu kwamba majina yana nguvu,Jina la Yesu lina nguvu zaidi ya majina mengine yote kwa sababu ni jina la Mungu. Hivyo,tunapaswa kulitumia Jina la Yesu tu,nalo latosha kuliko vitu vyote.
(i) Ni jina lake Mungu~ Waefeso 5:19
“ mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo“ Waefeso 5:19-20
(ii) Ni jina lenye uwezo na uweza wa kutenda mambo makuu na ya ajabu. Yeremia 33:3,Matendo 3:6,Yoh.16:24
(iii) Ukamilifu wa Mungu upo katika jina la Yesu. Wakolosai 1:18-19 Kwa kuwa Yesu Kristo ni Mungu,basi ilimpendeza ukamilifu wake wote ukae katika Yeye. Na ndio maana biblia inasema pasipo Yeye hakikufanyika chochote (Yoh1:1-5
Ni makosa makubwa sana kutumia jina jingine pale uombapo kwa sababu majina mengine si Mungu,hatukupewa hayo majina na wala majina mengine hayana uweza ndani yake. Neno hili “uweza” ni nguvu ya kipekee na ya ajabu aliyonayo Mungu pekee. Hivyo majina mengine hayana “uweza“.
Hivyo basi hata Mariamu mama yake Yesu,anatambua kwamba anayepaswa kuombwa ni Yesu Kristo tu. Tazama andiko hili;“ Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.” Yoh.2:4-5
Mariamu anatuambia lolote atakalo tuambia Yesu,sisi tulifanye. Ukitindikiwa na jambo lolote muendee Yesu,na chochote akuambiacho wewe kifanye. Ni kama vile anasema mimi sina huo uweza,bali muendeeni Yesu,Yeye ndie mwenye nao.
03.AINA ZA MAOMBI.
Ukweli ni kwamba biblia haisemi aina za maombi,kwa maana maombi ni mombi tu bila kujali unaomba nini so longer unaomba basi ni maombi . Lakini tunaweza kupanga aina za maombi kwa kufuata taratibu zetu tulizojiwekea sisi wanadamu,na kwa taratibu hizo tunapata aina fulani za maombi tuyafanyayo mara kwa mara. Aina kuu za maombi yetu ni kama ifuatavyo:
(i)Maombi ya shukrani
(ii)Maombi ya sifa na kuabudu
(iii)Maombi ya Toba / rehema.
(iv)Maombi ya vita
(v)Maombi ya Nadhili
(vi) Maombi ya mapatano na maombi binafsi.N.K
(I.) MAOMBI YA SHUKRANI.
Aina hii ya maombi ni muhimu sana kuliko aina zote za maombi. Unapomshukuru Mungu unaonesha kukubalikazi yake aliyokufanyia. Wakati wote tunapaswa kuwa watu wa shukrani. Maombi ya kushukuru hutangulia mwanzo kila ombi na umalizikia mwisho wa kila ombi lako,kumbuka hilo. Neno la Kristo linatutaka tuwe watu wa shukrani
Ukweli ni kwamba,ilikuwa hatupaswi kufundishwa “kushukury” kwa sababu “neno la kushukuru” yapaswa kutoka moyoni mwako. Mfano wa kawaida kabisa; ikiwa mtu amekupa pesa,je utafundishwa kumshukuru mtu huyo? Jibu ; hautafundishwa kwa maana utajikuta ukianza kusema “ asante kwa msaada wako wa pesa” au “kwa kweli,ninakushukuru sana kwa kunisaidia maana nilikuwa sina kitu kabisa,ninakushukuru sana rafiki” N.K tena gafla unaanza na kumwita “rafiki” hata kama hakuwa rafiki yako.
Hivyo kushukuru kwatoka moyoni mwa mtu,huja moja kwa moja ( automatically). Sasa jambo la kushangaza leo,watu wamekosa shukrani mbele za MUNGU wao,mpaka wafundishwe maneno ya kusema,hii haiko sawa,kwa maana maneno hayo ya mdomoni hayatoki moyoni.
( Isipokuwa watu waweza kufundishwa maneno ya kusema kama sehemu tu ya muongozo ili mtu aweze kujua anaombaje,lakini kile akiombacho ni lazima kitoke moyoni ).Asili ya kushukuru ni moyoni,moyo ni lazima umshangilie BWANA,ndio maana tunasoma;
“ BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu.Moyo wangu umemtumaini,Nami nimesaidiwa;Basi, moyo wangu unashangilia,Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.“Zab.28:7
Hivyo basi,maombi ya kushukuru ni maombi ya kumshukuru BWANA MUNGU kwa yote uliyonayo. Neno “kwa yote” ina maana kwa mema na yale na hata yale magumu unayoyapitia,yakupasa kushukuru. Neno la Mungu linasema “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” 1 Wathesalonike 5:18
Aina hii ya maombi,ni muhimu sana kwa maana huwezi kuanza maombi yoyote bila kuanza na shukrani. Ni ukweli usiopingika kwamba kila mtu ametendewa makuu na BWANA MUNGU Yeye MUNGU amekuwa mwaminifu sana hata pale tulipokuwa dhambini,Yeye hakutuacha bali alisubiri tutubu na tuanze upya na Yeye.
Ukiyatafakari maisha yako,utagundua kwamba ni neema na rehema za MUNGU tu,zinazokufanya wewe uwe hivyo ulivyo sasa. Wewe si bora sana kuliko wote waliokufa,wala si bora sana kuliko wote waliopata ajali bali ni mkono wa BWANA tu.
Ikiwa ni hivyo,basi yakupasa kusema “ asante Mungu” kabla ya kuanza na maombi yoyote yale. Hapa napo pana shida sana kwa wengi maana watu wamekosa kuyatafakari maisha yao kwa kumtazama MUNGU bali watu huangalia shida zaidi kiasi kwamba wanaona kana kwamba MUNGU hakuwatendea chochote.
~ Maombi ya kushukuru yakitoka moyoni yana nguvu ya ajabu. Wote walioshukuru vizuri walitendewa zaidi ya yale waliyoshukuru. Mifano ipo mingi hata katika maisha ya leo, labda litazame jambo hili kwanza katika maisha yako binafsi. Pale ambapo ulipotendewa mema na mtu yeyote yule kisha ukarudi kumshukuru mtu huyo. Je mtu huyo uliyemshukuru hatajisiki vizuri akutendee mema mengine?
Mfano ;
wewe umemshukuru jirani yako kwa msaada wa usafiri/lifti aliyokupa labda ulipokuwa huwezi/unaumwa. Shukrani zako zinamfanya akufikirie tena hata kama ulikuwa hauumwi bali atakupa lifti tena. Tazama jambo hili kibiblia kwa wale wakoma kumi waliotakaswa kisha mmoja wao akarudi kushukuru tena alikuwa ni mgeni tu yaani ni msamalia “ Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.” Luka 17:19
Yesu anamwambia Msamalia situ kwa habari ya kuponywa bali pia kwa habari ya imani. Msamalia alipokea mara mbili zaidi ya wale tisa walioondoka bila shukrani. Msamalia alipata neema ya kupokea imani kwa Kristo Yesu pale aliporudi kwa shukrani,kwa maneno mengine alipokea na vya rohoni pia…
ITAENDELEA…
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa +255 655 11 11 49/0683 877 900
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments