top of page

MANABII ~ 02 ( Tamati)

Updated: Sep 2, 2022


… Hivyo basi manabii wa uongo ndivyo walivyotokea. Sababu kubwa ya nabii kuwa nabii wa uongo ni pale anapotabiri nje ya Neno. Nabii wa uongo ni wakala wa kawaida wa shetani, lengo lao kubwa ni kujipatia pesa na mali kwa njia ya udanganyifu. Lakini biblia inaeleza kuwa manabii wa uongo walikuwepo tangu zamani, hawa tunaowaona leo ni wajukuu tu,


lakini kuna mababu waliotangulia kabla yao. Manabii wa uongo hawakutumwa na Mungu ( Yeremia 27:15). Bila shaka wametumwa na shetani lakini pia wapo waliojituma wao wenyewe. Kulingana na hali halisi tuliyonayo leo, inaonekana kasi ya manabii wa uongo ikikuwa, lakini na ndivyo wanajilimbikizia hukumu ya siku ya mwisho.


  • Manabii wa awali katika Israeli na Yuda.

Kama inavyojulikana kuwa Israeli makabila 12 ya watoto wa Yakobo yalipangalanyika na hatimaye pakawa na pande mbili. Pande mbili hizi huitwa “ Israeli ufalme wa kaskazini -makabila 10” na “Yuda ufalme wa kusini, makabila 2” katika falme hizi mbili, manabii nao walikuwepo wakiwemo wa uongo na ukweli. Nami ninaangazia manabii ambao biblia imewataja pasipo kuchimba undani wao sana. Manabii hawa walihudumu katika nyakati tofauti tofauti chini ya wafalme tofauti tofauti. Wafuatao ni baadhi tu ya manabii wa huko Yuda na Israeli.


Manabii wa Yuda. ~ Isaya, Yeremia, Ezekieli, Habakuki, Sefania, Nahumu, Yoeli na manabii wengine kama vile nabii mke Hulda, akina Shemaya N. K

Manabii wa Israeli ~ Eliya mtishibi ( 1 Wafalme 17) Elisha ( 2 Wafalme 5:3-8), Yona, Hosea. Na wengine kama Amosi alikuwa nabii wa Israeli, Ahiya.


  • Nabii wa mwisho katika manabii wa agano la kale.


Bila shaka jina “Malaki” si geni maskioni mwa wapendwa wengi, maana wengi wanaposikia jina hili haswa pale neno linaposomwa katika kitabu hiki cha Malaki, wengi hukumbuka mambo ya utoaji wa zaka iliyokamili ( Malaki 3:10-11), na hapo ndipo mahali unapotonesha donda sugu la wakristo wasiotoa zaka. Kumbuka Malaki ndiye aliyemalizia kazi ya utabiri baada ya Hagai na Zekaria.


Kipindi cha Malaki kilikuwa ni kipindi cha watu waasi, waovu sana. Hivyo ujumbe wake mkubwa ni kuwataka watu wageuke kutoka kwenye hayo maasi na wamrudie Mungu. Alifanikiwa kutangaza hukumu ya Bwana ijayo kwa wote wasiotii.

Malaki alitabiri ujio wa mwokozi ( Malaki 3:1) kama njia ya watu waandae mioyo ya kupokea ahadi ya ujio wa mwokozi. Lakini haikuwa rahisi, kwa maana baada ya utabiri wake, ilipita kama miaka 400 kabla ya agano jipya. Wengi hufikiria kwamba katika miaka 400 ilikuwa ni miaka ya ukimya kwa sababu hakuondokea nabii wa aina yeyote mpaka agano jipya, lakini haikuwa ukimya uliokosa shughuli. Kulikuwa na shughuli za hapa na pale, watu wakiendelea na maisha.


  • Manabii katika agano jipya.


“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.” Waebrania 1:1-2

Yesu, Mwana amesema nasi yote aliyotumwa aseme. Wala hakutenda neno yeye mwenyewe bali alitenda lile Baba aLilolitenda kwa maana yote ayatendayo Baba ndiyo ayatendayo Yeye ( Yoh. 5:19).Yeye alikuwa zaidi ya nabii ( Luka 24:19,27).


Hii ina maana yote aliyoamuru yameamriwa na Mungu, hivyo Yesu pia ni nabii aliyesema badala ya Mungu kwa maana alikuwa mwanadamu 100% na Mungu 100%. Yeye huitwa nabii wa mwisho tangu kwanza kwa maana alikuwapo kabla ya Musa na amekuwa baada ya Musa ( Yeye ni mwanzo na mwisho).


Hata hivyo wapo manabii kadha wa kadha katika agano jipya; kama vile nabii mke Ana binti Fanueli ( Luka 2:36), Kundi la manabii wa Yerusalemu ( Matendo 11:27), Kundi la manabii la Antiokia ( Matendo 13:1), Nabii Agabo ( Matendo 21:10) , na wengine N. K. ( hata hivyo katika zile huduma alizotoa Yesu Manabii ni maja ya sehemu ya huduma -Waefeso 4:11)


  • Manabii wa sasa.


Iko dhana kwamba kila aliyeokoka ni nabii wa Bwana,lakini pia iko dhana kwamba manabii ni wale tu walioitwa kwenye ofisi ya kinabii. N. K Sasa ipi ni kweli? Maana swala la manabii leo limekuwa ni changamoto. Lakini ili tuweze kujua kweli ya unabii, hatuna budi kuliangalia Neno linasemaje kuhusu manabii. Tangu nilipokupitisha kwenye somo hili, umegundua kwamba “manabii ni wasemaji wa Mungu “.


Ikiwa ndivyo, basi nafasi hii ya kuwa msemaji wa Mungu ni nafasi nyeti na muhimu sana ambapo si kila mtu atakuwa ni msemaji wa Mungu. Hivyo si sawa kusema kila aliyeokoka ni nabii wa Bwana kwa maana kuokoka ni kitu kingine na kuwa nabii ni kitu kingine kama vile unavyoona utofauti wa mtu kuwa mchungaji na mtu kuwa ameokoka. Nabii kama nabii ni tofauti kabisa na wokovu wa mtu. Mungu aliwachagua watu wachache kuwa manabii kati ya kusanyiko kubwa, hata leo manabii wapo wakitabiri na kutenda kazi na Bwana.


Kumbuka ;


unabii ni kazi ya Roho mtakatifu ambaye humpa yeyote amtakaye. Unabii hausomewi bali mwenye huduma ya unabii anaweza kwenda shule kuongeza maarifa kama sehemu muhimu sana katika ofisi ya unabii. Manabii wa agano jipya na wale wa agano la kale walifanana katika ngazi ya kiroho kwa sababu ni Roho yule yule aliyetenda kazi na ndiye atendaye kazi hata sasa.


Wengi hufikiri kwamba Roho mtakatifu wa kipindi kile cha kina Musa ni tofauti na Roho wa kipindi cha leo. Ukweli ni kwamba Roho Mtakatifu hajawahi kubadilika na kamwe hawezi kubadilika maana yeye pia ni Mungu. Na Mungu hana kigeugeu.


Ikiwa kama umejifunza kitu, nifahamishe na Kwa msaada zaidi piga;


Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900.


What’sapp namba+255 746 446 446 .


Mch. G. Madumla.


UBARIKIWE.

Comentários


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page