MANABII ~ 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 30, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 2, 2022

Biblia tunayoisoma yenye vitabu 66 yenye muundo wa agano la kale na agano jipya, ni Biblia yenye vitabu vya manabii wa kubwa na manabii wadogo. Ukubwa na udogo wa manabii hutegemea urefu wa vitabu vyao, na si vinginevyo. Hivyo, jumla ya vitabu 16 vya kinabii hupatikana katika agano la kale ( soma hapo chini uchambuzi wa vitabu 66 vya biblia). Hata hivyo ni vyema kujiuliza “ manabii /nabii ni nani hasa? Wametokea wapi? Kazi yao ilikuwa ni ipi? N. K
Manabii ni akina nani?
Kwa mujibu wa biblia, manabii walikuwa wasemaji wa Mungu. Watu maalumu wenye kusema walioambiwa waseme na Mungu. Unakumbuka habari ya Musa na Haruni? Mungu alimtuma Musa kwa farao ili awatoe Waisraeli utumwani Misri. Lakini Musa aliogopa na hatimaye akamkatalia Mungu kwa kusema “mimi si msemaji tokea zamani“,Ni kwamba Musa alikuwa akikataa. Lakini Mungu akampelekea ndugu yake Haruni, ili Haruni awe msemaji wake, naye Musa asimame kwenye nafasi ya Mungu ( Kutoka 4:14-16).
Hivyo Haruni alikuwa msemaji wa Musa, alitakiwa aseme kile tu anachoambiwa aseme, hivyo yeyote atakaye kataa kumsikiliza Haruni atakuwa amekataa kumsikiliza Musa, na mtu huyo atakuwa pia amekataa kumsikiliza Mungu.Yeyote aliyekuwa msemaji wa Mungu aliitwa ni nabii. Wasemaji wa Mungu walisema na watu, kuonesha Mungu anasema na watu ( 2 Wafalme 17:13)
Lakini hata hivyo, nabii alikuwa ni |“mwonaji“( 1 Samweli 9:9). Watu walipohitaji kuuliza neno kwa Mungu iliwabidi wamtafute “mwonaji” ili waulize neno. Hata wafalme wanapohitaji kwenda vitani, walikuwa hawana budi kwanza kumwendea mwonaji waulize neno kwao kwamba vita vitaendaje huko, waende au wasiende? Mwonaji alikuwa ni nabii. Mtu kama Samweli alikuwa ni nabii na mwamuzi wa Israeli, aliitwa mwonaji.
Je manabii walitokea wapi?
Tofauti na sasa kumezuka wimbi kubwa la manabii kiasi kwamba hujui yupi wa kweli na yupi wa uongo, kwa sababu kila kukicha watu hujipachika majina nakujiita wao ni manabii. Lakini hali halisi haikuwa hivi tangu hapo mwanzo kwa maana nabii hakujiita nabii kwa sababu watu wanamwona kuwa nabii, bali nabii walichaguliwa na Mungu na akawatuma kunena sawa sawa na kile asemacho yeye. Kwa kuwa unabii ni kazi ya Mungu, Mungu aliwatumia wanawake na wanaume kuwa manabii.
Kulikuwapo na manabii wakike kama vile Miriamu (Kutoka15:30), Debora ( Waamuzi 4:4) N. K, lakini pia kulikuwepo na manabii wa kiume kama kina Isaya, Danieli, Yeremia n. K. Hii ni kuonesha kuwa Mungu wetu hana upendeleo kama sisi wanadamu. Wanawake nao walifanya kazi ya Mungu kama wanaume.
Manabii walifanya kazi gani?
01.Kutangaza mwaka wa kufunguliwa kwa watu wa Mungu waliofungwa ( Kutoka 7:1-7, Isaya 61:1-3)
Ikiwa watu wa Mungu wamefungwa, Mungu hutumia vinywa vya manabii wake wafunue kile Mungu anachopanga juu yao. Ukisoma habari za taifa teule Israeli namna lilivyopitia kwenye vipindi mbali mbali vigumu wakati wakiwa Misri na hasa walipokuwa wamekwisha kutoka na hali bado wapo jangwani. Mungu alisema nao sana kwa kinywa cha Nabii, akiwapa habari njema ya kukomeshkukomesha utumwa wao ikiwa wataisikiza sauti yake na kutii.
02. Kutabiri juu ya matukio ambayo hayana budi kuja. ( Zekaria 1:18-21,Amosi 8:11-13,n. K)
Kwa kuwa ni wasemaji wa Mungu, Mungu hutupa kujua mapema yale ambayo hayana budi kuja. Kila kinachotokea kwako, kilipangwa. Hakuna cha bahati mbaya!!! Ndio maana Mungu hutaka sana uweze kujua na mambo yajayo, ili ujipange kushughulika nayo sasa kabla hayajatukia.
03. Kutoa maonyo.(Mathayo 23 yote, Mathayo 11:21,Mathayo 3:10) -Kawaida ya lugha ya maonyo katika biblia hutumia neno “ole”, kuonesha kuna ghadhabu kali ijayo katika kila ole itolewapo.
04. Kufunua pendo la Mungu na kuwafanya watu watubu dhambi zao. ( Isaya 54:7,Isaya 1:18).
Kumbuka;
Unabii ulitoka kwa Mungu, hivyo wanadamu waliongozwa na Roho mtakatifu ( 2 Petro :1:21). Ni Mungu mwenyewe alivuvia neno lake na kuliruhusu lisemwe kwa kinywa cha mtu /nabii. Ikiwa kama nabii alitakiwa kusema kile tu alichoamriwa kusema, basi kama ataongeza au kupunguza katika neno aliloamriwa mambo mawili yalimpata. Kwanza alikufa papo hapo, au Mungu kumwacha, na hatimaye kuwa nabii wa uongo.
Manabii wa uongo walitokea wapi?
Kama nilivyokueleza hapo juu ya kwamba ikiwa nabii atapngeza lake au kupunguza basi Roho mtakatifu humwacha nabii huyo na kujikuta akawa ni nabii wa uongo. “ Tamaa za kupata fedha na mali” ndio sababu kubwa ya baadhi ya manabii kuwa manabii wa uongo. Chanzo cha manabii wa uongo kilitoka kwenye manabii wa kweli waliokosa uaminifu wakaangukia kwenye kupenda fedha na mali. Hapo zamani, mfalme humwita nabii na kumwuuliza habari ya vita itakuwaje?
Kisha nabii husema na Mungu na kupata ujumbe ya sahihi kabisa kutoka kwa Mungu. Mfano wa ujumbe huo tuseme ndio nabii ameambiwa na Mungu hivi “… Mwambie mfalme aende kupigana, kwa maana atawashinda hao adui zake” kisha nabii husema kama alivyoagizwa kusema. Na hatimaye mfalme anatoa fedha na kumpa nabii, kisha kweli mfalme anashinda. Inatokea siku ingine ambapo mfalme anahitaji kwenda vitani. Na nabii kama kawaida yake huenda kusema na Mungu, lakini safari hii ndio tuseme Mungu amemwambia “... Mwambie mfalme asiende kupigana, maana atapigwa “.
Sasa kwa tamaa ya fedha, nabii hasemi yote aliyoambiwa, na anajikuta akisema uongo kwamba “Bwana amenionesha kwamba utashinda, nenda tu kapigane” lengo la nabii asimwaibishe, na afanikiwe kuchukua mzigo wa fedha. Sasa mfalme anapigwa, na kuangamizwa watu wake. Kwa tabia hii ya kusema uongo, Roho Mtakatifu anajitenga na nabii huyo, huku nabii hajui Roho amemkimbia.
Hapo ndipo shetani hupanda pepo la utambuzi ndani ya nabii huyo hata kumfanya asikie kuendelea kutabiri lakini ni kwa njia ya udanganyifu….
ITAENDELEA…
Ikiwa kama umejifunza kitu, nifahamishe na Kwa msaada zaidi piga;
Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
What’sapp namba .+255 746 446 446
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments