MAMLAKA YA MWAMINI – 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 16, 2017
- 3 min read

Ni vyema ukajua kwamba kila mwamini katika Kristo ana mamlaka iliyo kuu dhidi ya nguvu za giza,falme na juu ya majeshi ya pepo wabaya wote,maana biblia inasema “ Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. ” Luka 10:19
Andiko hilo ndilo andiko letu la msingi katika fundisho hili. Ukitafakari sana utagundua mambo mengi ndani ya andiko hili,Hivyo ili kujifunza vizuri kwa utaratibu,ni vyema tukaligawa fundisho hili katika vipengele vifuatavyo;
Kwa ufupi,
Mamlaka ni nini?
Aina za mamlaka
Kwa nini mamlaka?
Mtaokeo ya kutembea na mamlaka
Tokeo baya ukiwa nje ya mamlaka.
01.Mamlaka ni nini?
Neno mamlaka ni neno la Kiyahudi lenye maana ya kutawala (dominion ).Hivyo mamlaka ni nguvu ya kutoa maagizo,kufanya maamuzi, na kulazimisha utii juu ya amri au sheria fulani. ( it is the power to give orders,make decisions and to enforce obidience)
Ni uwezo wa kufanya maamuzi kisheria
Pia mamlaka ni uwezo wa kuamua kufanya kitu au jambo fulani pasipo kuhitaji ushauri wa mtu mwingine, wakati mwingine mamlaka huitwa haki ya kuamuru kwamba kitu gani kifanyike na kitu gani kisifanyike.
Nguvu ya namna hii yaani mamlaka hutolewa na yule mwenye mamlaka,ni sawa na kusema huwezi kutoa mamlaka ikiwa huna mamlaka,hivyo mwenye kutoa mamlaka sharti apokee kwanza ndipo atoe.
Mamlaka ni serikali fulani,kwa maana mwenye mamlaka ana amri ya mwisho juu ya maamuzi ya juu. Mfano tunaweza kujifunza zaidi maana ya mamlaka tukimuangalia yule akida katika Mathayo 8;9,imeandikwa
“ Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.”
Katika andiko hili,tunaona jinsi akida akieleza juu ya mamlaka aliyokuwa nayo kwa maana akimwambia huyu nenda,huenda na huyu njoo,huja. Kumbe pia mwenye mamlaka ana sauti ya utiisho juu ya kufanya au kutofanya jambo fulani.
Hivyo,tabia mojawapo ya mamlaka ni utii bila kuuliza uliza tazama yule akida jinsi asemavyo;
“ nikimwambia huyu,nenda huenda,nikimwambia huyu njoo,huja“
Siku moja nilikuwa katika daladala inayotoka kibamba(mbezi) naelekea kimara baruti,tukiwa katika mwendo gafula mbele yetu alikuwa amesimama trafiki polisi,alikuwa ni binti mdogo tu,anaonekana ndio alikuwa ameingia mafunzoni si muda mrefu. Mwenye alionekana nadhifu,mrembo huyu trafiki. Akanyoosha mkono wake juu ishara ya kusimama kwa gari yetu.
Basi,dereva wa daladala letu kaanza kupunguza mwendo atimaye akasimama kushoto alipo trafiki polisi. Kumbuka ndani ya daladala,tulikuwa watu wengi ( gari lilijaa sana kiasi kwamba wengi walisimama na kukanyagana). Yule dada trafiki alikuwa yupo zake barabarani,kwa hiyo ilimlazimu dereva wetu wa daladala ashuke na kumfuata trafiki polisi,watu wote tulisubiri tukiwa ndani ya daladala.
Hapo ndipo nilipojifunza maana ya mamlaka! Tazama,ingawa yule trafiki polisi alikuwa mmoja tena mdada mdogo tu,lakini alilisimamisha bus lenye watu wengi na kumfanya dereva aliyekuwa mtu mzima sana kushuka na kumuendea alipo trafiki. Mamlaka inatiisha kila kitu.Hivyo mamlaka inaweza ikatafsiriwa pia kwa maana ya pili,kwamba ,
ni haki ya kufanya,au kutofanya,inayotolewa na yule mwenye haki hiyo na ndio maana Yesu Kristo anasema kwamba amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani ( Mathayo 28:18). Mamlaka aliyonayo Yesu ni juu ya vitu vyote,maana vitu vyote viliubwa katika Yeye na kwa ajili yake ( Wakolosai 1:16-17)
Katika lugha ya Kiyunani neno mamlaka limetumika kwa jina la exousia ( nguvu ya kutawala). Unapoweza kutawala kitu ni sawa na kuwa na mamlaka juu ya kitu hicho. Mfano,serikali ina nguvu juu ya mambo ya nchi kama ardhi,hiyo serikali ina mamlaka juu ya vitu hivyo. Tafsiri hii imekaa vizuri sana tunapojifunza maana ya mamlaka…
ITAENDELEA…
Kwa msaada wa maombezi piga sasa +255 683 877 900
What’s app+255 746 446 446
Mch. G.Madumla
UBARIKIWE.
Comments