MAMBO MATATU MUHIMU KATIKA KUTIMIZA NDOTO YAKO.
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 13, 2017
- 6 min read
Updated: Sep 29, 2022

Mwenye ndoto afanye nini aweze kuitimiza ndoto yake?
Bwana Yesu asifiwe….
Je una ndoto? Je una ndoto ya namna gani? Je umewahi kujiuliza kwamba ufanye nini uweze kuitimiza ndoto yako?
Mimi nami ninayo ndoto yangu ambayo natamani niifikie,lakini ni vyema nikajiuliza swali hilo kwamba nifanye nini ndoto yangu itimie. Na wewe usomaye una ndoto fulani katika maisha yako ambayo unataka itimie,lakini inawezekana kabisa hujui ni kwa jinsi gani hiyo ndoto inaweza ikatimia,au hujui nini cha kufanya wakati huu. Lakini kwa neema yake Mungu amependezwa siku ya leo uweze kujifunza tatu muhimu kuelekea katika kuitimiza ndoto yako.
Inawezekana ukawa una ndoto zaidi ya moja na hujui cha kufanya. Lakini ni lazima ujue kwamba ili ndoto itimie kwa namna yoyote ile inahitaji jambo moja la msingi nalo ni “ muda”. Muda ni msingi sana wa kutimiliza ndoto,ni sawa na kusema huwezi kutimiliza ndoto yoyote ile pasipo kuwa na muda. Muda unahitajika sana,kwa maana ukikosa muda huwezi kutimiza ndoto;mfano chukulia mwenye ndoto fulani amekosa muda gafula akafa,Je ndoto yake itatimiaje naye hakuwa na muda tena wa kuishi?
Nafikiria kwanza ujifunze katika kipengele hiki cha msingi kiitwacho “muda na nguvu” Ingia hapa usome vipengele hivyo https://njiakwelinauzima.wordpress.com/2015/07/02/nguvu-na-muda-vikiisha-mwenye-ndoto-atafanya-nini/
Muda na nguvu ulizonazo sasa, zikitumiwa vibaya ni dhahiri unaweza usifikie malengo ya ndoto yako. Mfano; unapokuwa una ndoto ya kuwa mtu fulani kama vile kuwa mfanyabiashara lakini unapoteza nguvu nyingi na muda wako katika mambo mengine kama vile starehe na anasa za kidunia hii,basi ujue unaweza usifikie malengo yako. Kumbuka kutunza muda na nguvu ulizo nazo sasa kwa maana huwezi kuzipata tena.
Jifunze kwa bondia wa ndondi,mtu ambaye hata kula kwake hupangiwa kipi cha kula na kipi asile ili chakula kisije kuharibu mwili wake na kumpotezea nguvu katika mapambano yaliyopo mbele yake. Sasa,na wewe ukumbuke una mapambano ya kuitimiza ndoto yako,hivyo ni vyema kujifunza namna ya kuutunza mwili wako ukizingatia kipengele cha kutunza muda na nguvu ili kufanikisha malengo yote.
Ukijua namna ya kuuweza mwili wako usitumike nje ya malengo yako,basi ujue utaweza pia kutunza muda na nguvu utakazotumia hapo baadae katika ndoto yako. Leo watu wengi wamejikuta wameingia katika ndoto zao wakiwa hawana muda maana muda mwingi waliutumia vibaya,wengine wameingia katika malengo ya ndoto zao wakiwa wamechoka ( wametumia vibaya nguvu zao). Jiulize wewe je,umefanikiwa kutunza vizuri muda ulionao kwa ajili ya ndoto yako? Je umefaulu kutunza nguvu uliyonayo kwa ajili ya ndoto zako?
Mfano mzuri ni huu;
Nimeona hatari kwa watu wengi hususani vijana ambao wanaichosha miili yao pasipo kujua wanapotesa nguvu na muda. Vijana wengi wanaichosha miili yao katika vyakula,vinywaji na starehe zisizo na maana yoyote. Mfano wengi utumia soda na vimiminika vyenye chemical kali mara kwa mara wakati wa chakula. Sasa matumizi ya soda ni mabaya kwa maana ndani ya soda kuna kiasi kikubwa sana cha sukari. Sasa chukulia mtu mwenye ndoto lakini ndio mpenda soda na makemikali ya majuisi ya kopo. Je unafikiria baada ya muda fulani mbele atakuwa wapi? Je hatapata magonjwa kwa kuwa anaujaza mwili wake makemikali kila siku kwa maana anatumia soda kila siku,anatumia juisi za madukani kila siku. Na je atatimilizaje malengo yake ? baada ya miaka kumi atakuwaje?
Ni muhimu sana kujifunza hili,vile utakavyoweza kuutunza mwili wako kwa ajili ya malengo ya ndoto yako ya baadae. Sasa,mtu asikudanganye kwamba ndoto zako zitatimizwa vizuri hata kama unautumia vibaya mwili wako. Bali jaribu sana kuenenda kwa kuunyima mwili mavinywaji yenye sumu,kuunyima mavyakula ya kutengenezwa yanayokaa muda mrefu katika maduka ya chakula (mfano: ma-super market).
Mavyakula ya namna hiyo si mazuri kwa afya ya mwili wako ikiwa kama unapendelea kuyatumia mara kwa mara kwani yamesindikwa na madawa mengi. Sasa unapoyatumia unauchosha mwili wako kwa maana mwili unaufanya kama dampo la kutupa sumu hizo (mwili wako unakuwa ndio end product ya kupokea makemikali yaliyopo katika machakula hayo)
Sasa, tujifunze hatua mbili muhimu sana pale unapokuwa na ndoto fulani katika maisha yako. Biblia imefaulu kwa sehemu yote kutufunza kwa wale waliokuwa na ndoto na hatimaye wakazifanikisha. Siku ya leo,emu tujifunze kwa mtu mmoja aitwaye Yusufu mtoto wa Yakobo aliyekuwa na ndoto kubwa.
Biblia inasema;
“ Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.“Mwanzo 37:5-7
Ukisoma habari nzima ya Yusufu,utaona jinsi ambavyo alivyofanikiwa kuwa sawa sawa na ndoto zake. Hatuambiwi hatua gani haswa za msingi alizozichukua mpaka kufanikisha ndoto hiyo,isipokuwa tunaambiwa hatua moja tu aliyoichukua Yusufu. Lakini ni vyema tujifunze hatua mbili kama sehemu ya kufanikisha ndoto hiyo. Hatua hizo ni kama ifuatavyo;
01. Ombea ndoto yako.
Hii ni hatua ya kwanza na msingi kwa ndoto yoyote uliyo nayo. Inawezekana ukaota unafungua makambuni fulani hivi,na hapo uotapo hivyo kwanza usimwambie yeyote hata kama ni mumeo/mkeo unayelala kitanda kimoja. Unapopata ndoto,jitahidi sana kuipeleka mbele za Bwana kusudi Mungu akufahamishe zaidi katika maombi. Hatari mojawapo ya kuisema ndoto yako mapema bila kuiombea ni kushindwa kuitimiza. Mfano umeota mumeo/mkeo amaanzisha biashara kubwa mjini,alafu gafula ukaamka na kuanza kumwambia,kitendo cha kumwambia bila kuomba kina kunyima nafasi ya kuitimiza maana yupo adui azuiaye.
Kumbuka ; awezaye kuitimiza ndoto yako ni Mungu tu,hivyo ni lazima uwe na muda wa kutosha kuiombea ndoto yako. Hatua ya kwanza pale Unapoota ndoto,au unapokuwa na ndoto katika maisha yako ni kuipeleke mbele za Bwana katika maombi kabla ya kumshirikishs mtu yeyote yule. Unatakiwa wewe mwenyewe uiombee kwa kutosha ndipo ufanye hatua nyingine.
Leo,watu wengi wameshindwa kutembea katika ndoto zao kwa sababu wanapokuwa na ndoto hawaombi bali husema sema kwa watu. Ukifanya hivi,utakuwa unakosea maana ukiomba ndipo utakapopata wepesi wa kuitimiliza.
02. Iandike ndoto yako.
“ BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.” Habakuki 2:2
Kitendo cha kuandika kinakupa nafasi ya kuwa na kumbu kumbu nzuri na ya kutosha katika ziku za usoni. Lakini pia,unapoiandika ndoto/malengo yako;utajikuta ukiweza kutiki moja hadi jingine kwa like lililofanikiwa tayari. Ni muhimu sana kuandika ndoto yako.
Habakuki anatuambia faida moja wapo ya kuandika ndoto,ni kuifanya hiyo ndoto iwe wazi sana. Kuwa wazi sana ni hali ya kuifanya ndoto iweze kusomeka na mtu wako wa karibu,mfano mume/mke/watoto. Ukumbuke itafika wakati usipoiandika,unaweza ukahisahau na hakuna wa kukumbusha kwa kuwa hukuiandika.Sisi waafrika wengi hatuna utaratibu mzuri wa kuandika mambo yanayohusu maendeleo yetu ya baadae tukidhani kwamba kama tukiandika basi tutakufa mara,kumbe ni hali tu ya ujinga wa kifikra unaotusumbua kwa maana kufa kupo tu. Sasa kipi bora ufe na ndoto zako au ufe ukiwa umezikabidhi ndoto zako kwa mume/watoto wako?
Wewe unaweza ukawa ni shahidi mzuri hapo ulipo,unapoangalia magomvi mengi yanayoendelea kila kukicha kwa sababu ya mwenye ndoto na mali amekufa pasipo kuandika vyema usia na maendelezo ya ndoto zake. Sasa watoto/ndugu wa karibu wanaingia katika magomvi na wanakosa muelekeo mzuri wa kuendeleza yale uliyoyataka yaendelee kwa sababu tu mwenye ndoto kafa bila kuandika chocote.Ukifanikiwa katika hatua hii ya pili ya kuandika maono/ndoto zako,basi ujue utakuwa na wepesi wa kukumbuka yote huku ukiendelea kuyaatamia hayo yote katika maombi.
Jiuleze wewe kwa sasa?;Je umefanikiwa kuandika ndoto zako? Je umeandika katika mpangilio mzuri unaoweza kusomeka vizuri kama maji? Je unaweza kuandika yote bila kuficha ficha?
Jijingee utaratibu wa kuandika ndoto zako ungali una muda na nguvu kwa sasa na ungali U hai ili ndoto hizo zikusaidie wewe pamoja na mwenzi wako. Tena kwa sababu umeichukua atua ya kwanza ya kuomba kwanza wewe mwenyewe,basi hatui hii uiandike na umpe yule mtu wa karibu nawe awe na kumbu kumbu juu ya hayo yote.
03. Iseme wazi wazi kwa watu wanaokuhusu.
Hatua hii ni muhimu sana kwa maana unapoisema unakuwa unaikiri. Na kuna nguvu katika kukiri jambo. Ukiikiri ndoto yako kwa maneno mbele za watu wako wa karibu na wewe ni vyema kwa maana utakuwa unafanya tendo kubwa kiimani,tendo hilo ni kuwajenga kiimani wale waisikiao tena utakuwa unaikubali kwamba ndivyo ilivyo.
Yeyote aliyeshinda vita ilimbidi aseme kwanza kwa sauti masna hata biblia inatuambia kwa kinywa mtu hukiri hata kupata wokovu ( Warumi 10:10). Hata Yesu alishinda majaribu yote pale shetani alipomfuata na kumjaribu alipotamka kwa neno la Mungu akamwambia ibilisi “imeandikwa” ( Luka 4:1-12)
Ndoto yako unaweza ukaisema kwa watu wako wa wakaribu nao wakaisikia kama alivyofanya Yusufu mwana wa Yakobo. Ingawa ni lazima ukubali kulipa gharama ya kukataliwa pale utakapoisema kwa hao ndugu,maana wengine wataikataa na kukubeza kwamba huwezi kufanya hivyo. Wengjne watakuchukia na kukupinga vikali hata kutaka kukuua kwa sababu ya ndoto zako.
Sasa,yanapotokea hayo usiogope bali ujue ni kawaida kabisa kwa maana sasa kuna mahali unaenda. Kwa sababu huwezi kwenda mahali fulani kimaendeleo pasipo na vita kuwepo. Kila katika hatma yako kuna vita fulani,lakini wewe kaza kusonga mbele ukijua kwamba ni mambo ambayo hayana budi kuja.
Kitendo cha kuisema ndoto yako ni moja ya hatua ya kuifanikisha hiyo ndoto yako kwa sababu ya kuikiri hadharani. Lakini ni lazima hatua mbili zilizopita zitangulie kwanza,kwa maana kuna hatari kubwa sana ikiwa kama utaisema ndoto yako na hujaiombea. Vita itakayokuwepo ni kubwa huwezi kuishinda kama hujaiombea vizuri ndoto yako.
Tunaona jinsi ya vita iliyoibuka kwa Yusufu pale alipoisema ndoto yake. Nduguye wa damu moja walimuinukia hata wakataka kumuua,lakini Yusufu alilindwa ns Bwana. Na ndivyo itakavyokuwa kwako ikiwa utafanya haya yote katika imani,utainukiwa na ndugu au jamaa wa karibu lakini uwe na uhakika utasalimika na utaifikia ndoto yako ikiwa utakuwa na mahusiano mema na Mungu wako.
Kwa msaada zaidi nipigie sasa kwa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments