top of page

MAJINA YALIYOBEBA SIFA ZA ROHO MTAKATIFU.

Omba kila siku,uwe uweponi mwa Bwana. Uvikwe nguvu.


 Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Roho mtakatifu ndiye mwalimu wa kweli,yeye huitwa pia ni “Roho wa kweli ( the spirit of truth) ” Yoh.14:17 ndiye atufundishaye na kutukumbusha yote ( Yoh.14:26). Wengi wamemwelezea Roho mtakatifu ni nani,lakini mimi nataka ubaki kwenye tafsiri hii moja “ Roho mtakatifu ni Mungu” ( Matendo 5:3-4) bakia hapo. Hivyo kwa haraka haraka yatazame majina yafuatayo yenye kueleza sifa na kazi za Roho mtakatifu.;

  1. Maji.

Kwa namna ya kipekee kabisa,neno linataja maji kumfananisha na Roho mtakatifu. Mara nyingi tumesoma neno “ maji ” yakitajwa katika kumwelezea Roho mtakatifu.

“ Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.” Yohn.7:38-39

Yeye ni maji ya uzima,maji yakatayo kiu. Kiu inapotajwa hapo juu,haina maana ya kiu ya chipsi na soda bali kiu ni “msukumo wa dhambi” kwa hiyo yeyote aliye ni msukumo wa dhambi / aliyekuwa mtumwa wa dhambi na amwendee Yesu naye atapewa Roho mtakatifu atakae kati hiyo kiu. Roho mtakatifu huitwa ni “ maji ” amefananishwa nayo.

Sote tunafahamu kazi ya maji kwa mwanadamu na hata katika vitu au viumbe mbali mbali. Huku kwetu uswahilini tuna msemo usema “ maji ni uhai ” na ni kweli. Lakini maji yanakazi nyingi mwili wa mwanadamu. Na Mojawapo ya kazi ya maji kwetu ni kututia nguvu. Pale unapochoka ukaishiwa nguvu,basi maji yanaweza kukutia nguvu na ukaendelea na safari yako. Tena maji yanasafisha taka na kuondoa uchafu wote. N.K

Na ndivyo Roho mtakatifu afanyavyo kazi yake kwetu. Yeye hututia nguvu,utupa nguvu za kushinda dhambi / uchavu wa kila aina. Hakika Roho mtakatifu ni maji n zaidi ya maji.

  1. Mafuta.

Hapo zamani mafuta yalitumika katika kuwasimika wafalme na watumishi wa Mungu ( 1 Samweli 16:13). Na baada ya hapo watu hao waliotiwa mafuta huitwa “wapakwa mafuta ” Lakini, jambo hili linaendelea mpaka sasa haswa kwa watumishi wa Mungu.

Mafuta yanabeba picha ya Roho mtakatifu. Lakini, pia ufahamu ya kwamba mafuta yamebeba kazi nyingi sana. Ebu cheki engine oil / mafuta ya injini za magari / vipuri. Ambayo yana kazi ya kulahinisha sehemu za engine / injini ili vyuma visisagike au kuharibika. Roho mtakatifu naye huitwa ni mafuta ambaye ufanya kazi ya kusimika watumishi wa Mungu na viongozi pia ni Yeye ambaye mwenye kutia wepesi watumishi waifanyao kazi yake. Hivi unajua pasipo Roho mtakatifu wewe huwezi kutumika wala kufanya chochote katika huduma uifanyayo sasa? Ndio huwezi bila yeye Roho mtakatifu.

  1. Moto.

Unakumbuka mstari huu ?“BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.“ Kutoka 13:21-22

Ukweli ni kwamba; maongozi yote haya,ilikuwa ni Roho mtakatifu akiwaongoza Waisraeli. ( Kumbuka ; kipindi hicho kabla ya Yesu,Roho mtakatifu alikuwa akiitwa Roho wa Mungu. Naye alikuwa juu ya watu wachache kama wafalme na manabii)

Kazi ya moto jamani ni pana sana. Lakini fahamu kazi moja tu,ni kwamba “ moto huteketeza ” kwa hiyo moto unateketeza uchafu,au uadui n.k Roho mtakatifu naye ni moto akiteketeza dhambi, uchafu na maadui zetu. Unauhitaji moto huu mpendwa.

  1. Upepo.

“ Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.” Matendo 2:2

Kwenye siku ya petekoste,wanafunzi 120 walibatizwa katika Roho mtakatifu. Biblia inasema “upepo wa nguvu ” ndio ulitangulia kisha ndimi za moto. Kawaida ya upepo unapovuma,basi ujue hauwezi kuonekana isipokuwa utakachoweza kukiona ni matokeo yake tu. Na ndivyo Roho mtakatifu alivyo,huwezi ukamwona kwa macho ya nyama,ila utaona matokeo yake. Ukimwita Roho mtakatifu ashuke,utakchokiona ni matokeo yake tu. Roho mtakatifu ni upepo hivyo ni nguvu ya kiungu isiyoonekana kwa macho bali kwa matendo yake.

  1. Hua.

“ Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;“ Mathayo 3:16

Hua ni ndege kama njiwa. Ni ndege fulani mwororo,msafi,mzuri,lakini ni mpole sana. Huyo ndio Roho mtakatifu ambaye Yeye ni mpole,msafi akaaye mahali pasafi. Huchukia dhambi na kamwe hakai kwenye dhambi. Roho mtakatifu ni mzuri,msikivu na ni wa haki. Yeye hufananishwa na ndege “hua“

  1. Muhuri.

Hivi unajua kitendo cha kuokoka tu,umepigwa muhiri na Roho mtakatifu kwamba wewe si mali tena ya shetani bali ni mali ya Bwana.

“naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu. ” 2 Wakorintho 1:22

Tazama hayo maneno mawili “ muhuri na arabuni “. Maneno haya yna maana. Unapookoka Yesu anakupiga chapa yake “muhuri” kuonesha umemilikiwa na mume mwingine ambaye ni Yesu. Lakini “arabuni” ni sawa na “ pete ya uchumba ” ( a guaranteeing ). Pete hiyo ya uchumba inaashiria harusi / sherehe kati yako na mwanakondoo siku ya mwisho. Sasa,chukua picha hii;

Ikiwa binti amevishwa pete ya uchumba,lakini hatulii,mara kachepuka,mara kakutwa kwenye michongoma na jamaa mwingine. Vipi ataolewa huyo ???? Kumbe pete ya uchumba inaweza ikawepo lakini usipotulia,kuolewa utakusikia kwenye bomba la maji,huwezi ukaolewa,lah ukiolewa ni kwa neema tu! Na ndivyo ilivyo,ukiokoka unategemea kwenda mbinguni lakini kama utajisahau utakwenda na maji,hutaiona mbingu. Yeye Roho mtakatifu ni “ muhuri “

Ikiwa fundisho hili limekubariki na umejifunza kitu,basi nifahamishe kupitia namba zangu + 255 683 877 900 

WhatsApp ni +255 746 446 446

Mch. G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page