top of page

MAJARIBU.

“Jamaa hajui kwamba ni mtego huo !!! Hahahaha ” @ Mch Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Nilikuwa nasoma kitabu kimoja hivi juu ya majaribu. Mwandishi amejaribu kuandika kuhusu majaribu kwa sehemu yake,lakini nilipotazama kwa ukaribu makala yake nikagundua kuna makosa fulani hivi,si makosa ya uandishi bali ni makosa ya ufafanuzi alioutoa kuhusu majaribu. Nikasema ikiwa kitabu hiki kimeuzika sana,basi itakuwa watu wengi wamesoma fafanuzi hizo ambazo kwa kweli haziko sahihi. Kwa sababu hiyo ikanilazimu leo nami nitie mkono mkono wangu nikuandikie juu ya eneo hili “majaribu” ili upate ufafanuzi wa kibiblia,kisha tujifunze namna ya kushinda katika majaribu.

  1. Majaribu kibiblia ni nini haswa?

Ni vishawishi vyenye lengo la kukuuangusha dhambini. Vishawishi vya namna hii huletwa na shetani wala sio Mungu,maana Mungu hana vishawishi kwako kwa maana lengo la vishawishi ni kukuangusha dhambini hivyo Mungu hawezi kuwa na lengo la kukuangusha. Jaribu ni zaidi ya mtihani kwa sababu tabia ya mtihani hauna lengo la kukufelisha bali kukupandisha.Hivyo,Jaribu huletwa na shetani ili kukuangusha na ndio maana yeye shetani huitwa “ mjaribu” ( Mathayo 4:3a). Mungu hamjaribu mtu wala hajaribiwi bali Mungu anaweza akaruhusu kujaribiwa kwa lengo zuri ( Yakobo 1:13). 

Siku moja nilipokuwa nina-withdraw (ninachukua)pesa benki. Baada ya kuchukua pesa pale dirishani kwa yule keshia(cashier) mdada fulani hivi,nikaondoka zangu. Nilipofika ofisini kwangu,nikagundua nimezidishiwa milioni moja,sikuamini! Nikarudia kuhesabu tena,na hapo nipo peke yangu ofisini,kweli bhana milioni moja imezidi! Na kumbuka kipindi hicho sikuwa mchungaji nilikuwa kama wewe tu ulivyo sasa. Kitendo cha kuzidishiwa pesa nyingi namna hiyo hakikuwa cha kawaida,wala haikuwa ni mpango wa Mungu. Hivyo hakuwa ni mtihani bali ni “jaribu“

Sasa ona kilichotokea!!! Moyoni mwangu pakawa na sauti mbili nilizizosikia,sauti ya kwanza ikiniambia “rudisha pesa ya watu,maana utamsababishia hasara mdada wa watu leo! ” Bali sauti ya pili ikisema ndani yangu,“ utakuwa mjinga ukirudisha pesa nzuri kama hiyo,usirudishe hiyo pesa maana hujaiba,hata hivyo wewe unadaiwa kodi ya watu laki saba,ondoka nayo hiyo pesa-hakuna shida na wala sio dhambi,hutajulikana!

Baada ya kujiuliza uliza ilifikia wakati nikafanya maamuzi ya kusikia sauti ya kwanza,iliyosema “rudisha pesa ya watu” nikaamua kufunga safari kuipeleka benki hiyo pesa! Haikuwa rahisi maana milioni moja ni kubwa hasa kipindi kigumu kama cha kipindi kile. Hapo nilijaribiwa katika pesa,nami nikalishinda jaribu hilo hali sikuwa na kitu chochote kwa kweli. Lakini cha ajabu,niliporudisha pesa ile sikupewa hata asante ya kifutia jasho Dah! Kweli waswahili hawajakosea kwenye ule msemo usemao “tenda wema uende zako,usingoje shukrani!”. Hivi ungelikuwa wewe ungeliweza kuvuka jaribu hili katika kipindi kigumu kama cha leo? Sijui bhana!!!

  1. Majaribu yanatofauti gani na mitihani?

Miaka fulani hivi nilipokuwa shuleni,kwenye shule ya msingi kama darasa la tano hivi. Mwalimu wetu wa hisabati alikuwa akipenda kutupatia mitihani ya mara kwa mara kwa lengo la kutuhuimarisha ili tupande daraja la ufaulu. Ingawa wengi wetu tulikuwa tukichukizwa na mitihani hiyo,maana wengi tulikuwa hatupendi somo la hisabati. Ulikuwa ni utoto ndio uliokuwa ukitusumbua!!!Sasa nimekuwa ninaelewa kile alichokuwa akikifanya mwalimu wetu,kwamba kilikuwa ni chema sana. Mwalimu alikuwa akitupatia “mitihani” na wala alikuwa hatujaribu. Kwa maana lengo kuu la mwalimu ilikuwa tufaulu ( lakini unapojaribiwa lengo lake ni ufeli)

Mfano ni huu,Yesu Kristo hakujaribiwa na Mungu kwa kupelekwa na Roho kule nyikani kama wengi wetu wanavyoeleza. Yesu alijaribiwa na ibilisi maana ibilisi ndie mjaribu. Tusome hapa kidogo;

“Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.” Mathayo 4:1-3

Neno “ajaribiwe na ibilisi” kama lilivyotumika kwenye mstari wa kwanza hapo. Linatuonesha wazi wazi kwamba ni nani ambaye aletaye majaribu. Neno hilo “ajaribiwe” kwa kiingereza tungelisema “to be tempted” yaani kujaribiwa kwa lengo la kuungushwa sio kwa lengo zuri la kufaulu. Ibilisi hakuwa na mpango mzuri wa kumpandisha Yesu bali alikuwa na mpango mbaya wa kumuangusha kabisa. Na huo ndio mfano mzuri wa majaribu. Utangundua kwamba,mpango wa Mungu ni kukuimarisha,kukupa uimara hivyo Yeye hawezi kukujaribu isipokuwa anaweza akaachilia mitihani kwako kwa lengo zuri.

  1. Majaribu yanatoka wapi?

Majaribu yanatoka kwa shetani maana yeye ndiye mjaribu. Ibilisi alimjaribu Yesu (Mathayo 4:1-3),na ndivyo anavyofanya hata kwako siku ya leo. Mungu si mjaribu ila anaweza akaruhusu ujaribiwe,lakini ujue katika kila jaribu analoluhusu Mungu,ni la kawaida ya wanadamu naye Mungu hawezi kukuacha ujaribiwe kupita uwezo wako,lakini pamoja na hayo atafanya na mlango wa kutukea ( 1Wakorintho 10:13). Ibilisi ndiye mjaribu tangu zamani,lengo lake uanguke kwenye jaribu hilo. Lakini ujue Mungu ameweka mlango katika kila jaribu! Neno lake halijawahi kudaganya,wala halidanganyi wewe amini hivyo tu.

  1. Ni nani ajaribiwaye?

Kila mtu aliyesimama na Mungu hujaribiwa. Kwa mujibu wa biblia wale waliojaribiwa walikuwa na watu wenye imani,watu waliotembea na Mungu na hao ndio waliojaribiwa. Kumbuka jambo muhimu kwamba majaribu ni kazi ya shetani kwa watakatifu wa Mungu,yeye shetani analengo la kuwaangusha watu wa Mungu lakini katika kufanya hivyo watu wa Mungu wanaimarishwa kiimani. Hivi unajua uwezi kusema wewe ni mwaminifu pasipo kujaribiwa katika eneo hili? Wala huwezi kusema wewe ni mpole usiyekuwa na hasira hasira za haraka haraka ikiwa hujachokozwa,au ikiwa ibilisi ajakupitisha kwenye engo ya kukasilishwa!

Hivyo utagundua kwamba kila mmoja wetu anapitishwa kwenye majaribu fulani ili kuithibitisha imani yake. Ibilisi anakazana sana kutupitisha kama kwenye moto ili kusudi tupoteze muelekeo lakini ndipo tubachongwa kuwa bora zaidi.

  1. Aina za majaribu

01. Majaribu juu ya miili yetu. 

Vita kubwa ya kwanza ya shetani ipo katika miili yetu yenye asili ya duniani hii. Katika majaribu ya mwili,ndio tunaona mtu akipitishwa kwenye magonjwa na ,hali ya njaa,kiu,hali ya kukataliwa. Mfano mzuri wa aina hii ya majaribu ni ule wa Ayubu mtu aliyekuwa mkamilifu na mwelekevu,aliyemcha Mungu. Mtu huyu alijaribiwa na ibilisi juu ya mwili wake katika magonjwa makali na makubwa kiasi kwamba hata mkewe akaona bora Ayubu amkufuru Mungu ili afe maana alikuwa katika mateso ya mwenye haki. (Ayubu 1 na sura ya 2’yote) Leo wengi tunapitishwa kwenye majaribu ya namna hii,na ni kwa sababu tuna miili sote,hivyo usipokaa vizuri katika eneo hili unaweza ukakata tamaa na kuangushwa na jaribu. 

02.Majaribu ya zinaa na uasherati.

Ningeliweza kuyaweka majaribu ya namna hii kwenye kundi moja la “majaribu juu ya miili yetu“. Lakini ni muhimu kutenganisha ili kukupa msisitizo.  Ibilisi anawawinda sana watu wa Mungu kuwaangusha katika tamaa za zinaa. Si kwa wanawake wala si kwa wanaume,wote hujaribiwa katika tamaa ya zinaa!. Ukikamatwa na mjaribu katika eneo hili ujue umemalizwa kiujumla ujumla,sababu ni moja ya eneo muhimu sana. Ni lazima ushughulikie ipasavyo jaribu hili. 

03. Upinzani kutoka kwa wenye mamlaka.( Mazingira magumu ya kiuongozi)

Ni aina ya majaribu ya shetani kuwatumia sivyo ndivyo wale waliopewa mamlaka juu yako. Mfano boss wako akawa anahitaji akutumie vibaya nawe uwe upande wake hali ukijua ni makosa,lakini sasa boss wako ana mamlaka juu yako. Au mfano ibilisi anaweza akaikamata serikali yako ili ibane uhuru wa kuabudu mahali ulipo. Ebu angalia mfano mzuri kwa kina Daniel alipokuwa utumwani Babeli (Soma Danieli sura yote ya 6)

04. Mazingira hatari,magumu ya kwako binafsi.

Kuna wakati mwingine hali haikubaliani na wewe. Adui utafuta mwanya wa kukujaribu kuiacha imani na ukubaliane na hali halisi ya mazingira. Mfano chukulia upo kwenye ndoa na ndoa yako inapitia hali ngumu kiuchumi kiasi kwamba unaomba chakula kwa jirani yako ili ulishe watoto. Ukimuangalia mwenzako yaani ni “afadhali ya jana” kachokaaa hali mbaya. alafu  katikati ya mazingira magumu kama hayo unakata tamaa maana unafikiria utakaa mpaka lini katika hali hiyo? Hujui mazingira hayo yameruhusiwa na Mungu akutengeneze uwe hodari kwake,shetani anakuangalia katika jaribu hilo utafanyeje? 

  1. Mifano ya watu waliojaribiwa.

  2. Ayubu (Ayubu 1,2)

  3. Mfalme Daudi -( 2 Samweli 11:2-4)

  4. Daniel ( Danieli 3 yote) 

  5. Yesu (alijaribiwa kupita wote)

  6. Mitume wa Yesu nao walijaribiwa kwa nyakati tofauti tofauti.

  7. Lengo la kujaribiwa.

Lengo la Mungu ni kituimarisha kiimani. Majaribu ni ngazi ya kufanikiwa kwako,ingawa lengo la mjaribu ni kukuangusha kiroho. Mungu anataka katika jaribu hilo ulilonalo uvuke ili kusudi upande utukufu hadi utukufu; Mungu ni mwaminifu sana,maana anakusudia uwe imara.

  1. Nini ufanye unapojaribiwa?

01.Uwe muombaji na mtu wa Neno . ( Luka 22:40)

Yesu akuambia sasa “omba usije ukazama katika majaribu” (Luka 22:40). Hakuwa na maana kwamba ukiomba hutafikwa na majaribu,bali maana kubwa ilikuwa ukiwa muombaji hutazama au kukamatwa au kushindwa na majaribu. Yajapokuja utakuwa na uwezo wa kutoka mara moja. Lakini pia ukumbuke yapo majaribu ambayo yanakuja kwa sababu hauombi maana mengine unapoomba panakosekanika nafasi ya kujaribiwa na ibilisi,ingawa mazingira ya namna hii ni adimu.

02.Vumilia huku ukimtazama Mungu.

Mpendwa usikate tamaa maana hata Yesu alijaribiwa lakini alisonga mbele. Ni kweli yawezekana jaribu lako likawa ni zito sana,lakini wewe vumilia tu huku ukiendelea kuutafuta uso wa Mungu kana kwamba mtu.asiyekujua akikuona anaweza asijue lolote unalopitia. Uvumilivu unaenda na kutunza siri ya jaribu hilo unalopitia,maana ikiwa kweli umekubali kuvumilia basi ni lazima utakaa kimya kutunza siri.Hakuna kwenye biblia aliyejaribiwa nje ya uvumilivu! Unapovumilia zaidi unampa nafasi Mungu atende juu ya majaribu yote unayoyapitia.

G

Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page