MAANDALIZI MEMA YA IBADA.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 30, 2019
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Maandalizi mazuri ya jambo lolote hupelekea matokeo mazuri,maandalizi yenye nguvu huleta matokeo yenye nguvu. Hakuna kitu kizuri pasipokuwa na maandalizi mazuri. Hata ukitaka kufaulu katika alama za juu,basi ujue huna budi ujiandae vyema. Hivyo utagundua kwamba chochote kile chenye matokeo mazuri,kiliandaliwa vyema. Na hapo wala mtu asijidanganye au kudanganywa kwamba anaweza kupata matokeo mazuri bila kujiandaa.
Siku moja nilipokuwa shule ya biblia,tulipokuwa tukisoma somo la “Bible study methods”,mwalimu alituambia tusome kifungu cha Wakolosai 4:2-3 kisha tuje tutafakari kwa pamoja, Lakini tulifanya hivyo,lakini tulipomaliza alisema tena turudie na tusome tena,tukafanya hivyo kwa takribani siku tatu hivi kwa andiko hilo hilo la Wakolosai 4:2-3,mwishoe nikachoka !!!Nikajua tumemaliza,lakini
Naye akasema tena,“endelea kusoma kwa maana kuna mambo utayaona zaidi… ” Sasa,mimi kwa kweli niliboreka sana,kusoma kitu hicho hicho kila siku! Agizo hilo lilinichosha sana hapo mwanzo!!! mpaka nikajiuliza “hivi huyu mwalimu anadhani sisi hatuna kazi ya kufanya? kwa nini asiendelee na kitu kingine?…”
Lakini kweli,tulipoendelea kusoma na kusoma na kutafakari,tuligundua mambo mengi kuliko tulivyosoma mara moja. Nikaanza kuelewa maana ya mwalimu kutuweka kwenye eneo moja kwa muda mrefu,nikagundua alikuwa akituandaa tuwe walimu wazuri wa Neno la Mungu kwa kulichunguza zaidi. Kwangu mimi ilikuwa ni maandalizi mazuri ya kiibada katika neno. Haikuwa rahisi lakini kuna mambo tuliyapata mengi.
Kumbe hata kama unataka kuwa mwalimu mzuri wa Neno la Mungu unahitaji maandalizi ya kutosha katika kila neno unalofundisha. Usichukue neno fulani tu kwa mtazamo wako,na ukalazimisha neno liseme kama utakavyo,bali kuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa kabla ya kusema kitu chochote.
Kuja ibadani ni sawa na kuja na kuonana na Mungu.
Ukweli ni kwamba,ukienda ibadani ni sawa na umeenda kukutana na Mungu,Sasa fikiri ukweli huu. Je utaenda bila kujiandaa hali ukijua kwamba yule ninaemwendea ni Mungu wa miungu? Je utachukulia poa kwenda kuonana na Mungu? Ebu fikira hivi;chukulia unakwenda kuonana na rais wa nchi yako. Kisha raisi akasema “ mimi nitakuja huko huko uliko,hunahaja ya kuja kwangu,bali mimi nitakushukia mahali ulipo,mtaa wako kisha nitaonana na wewe,nitakuja! ” Hivi itakuwaje hapo?
Hautajiandaa kupokea ugeni mkubwa namna hiyo? mimi nakwambia ukweli kabisa,ni lazima utajiandaa katika kila eneo. Hata barabara utaitengeneza vyema,utafanya usafi,unaweza ukapiga na deki hata mahali pasipostahili,utajiandaa ukae sawa sawa kwa sababu tu ya mwanadamu kiongozi anayekujia. Je Mungu si zaidi ya raisi? Mbona hakuna maandalizi unayoyafanya unapokwenda kuonana naye?
Ebu tuangalie Israeli alipoenda kuonana na Mungu,alifanyeje? Biblia inasema “ Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. ” Kutoka 19:10-11.
Bwana anawataka Israeli wote wajitakase kisha wawe tayari. Neno kujitakasa linamaana ya kujisafisha / kuwa safi,hivyo leo hii neno hili lina maana ya “kutubu” kujiweka safi moyoni pale unapokwenda kuonana na Bwana. Pia maana pana ni kuacha uovo. Bwana anachukia uovu,hivyo kila amwendea Bwana na aache uovu wake (Isaya 55:7). Lakini pia “wawe tayari”,Bwana anataka kuona utayari wao. Hata sasa ni lazima utambue kwamba Bwana ni mkuu sana,achukiaye uovu. Unapomwendea ni lazima uache na kutubu. Lakini pia “uwe na moyo wa utayari” kupokea kile alichokiandaa.
Ni kwa namna gani nijiandae?
Kwanza katika ufahamu wako,ujue unapoenda ibadani unakwenda kuonana na Mungu. Hilo ndilo jambo la kwanza la kubadilisha mtazamo wako. Lakini pia zingatia kwamba kiongozi yeyote ibadani humwakilisha Mungu,kwa hiyo nyenyekea kwake ili usikie sauti ya Mungu. Ongezea na mambo yafuatayo kama maandalizi;
Andaa ibada yako kwa maombi – kabla ya siku ya ibada,iombee ibada binafsi,ukiomba kuisikia sauti ya Mungu,isimamishe ibada kimaombi ukiwa huko huko nyumbani kwako.
Andaa matoleo yako mapema – panga matoleo yako katikati ya wiki,usipange sadaka yako jumapili ndani ya ibada kwa maana ukifanya hivyo unaweza kujikuta ukimtolea Bwana kisichostahili au ukashindwa kutoa kabisa! ( Andaa sadaka zote,za watoto wako kama wapo)
Andaa watu wako kwa kuwaeleza kwamba mnakwenda kuonana na Bwana – Usimwache mtu nyumbani kisha wewe ukaenda ibadani mwenyewe pasipo sababu maalumu,kwa maana hata waisraeli walikwenda wote kuonana na Bwana.
Jitakase mapema – unapogundua upo mbali na Bwana,ni vyema ukajitakasa kwa toba ukiwa nyumbani hata kama kanisani mtaomba tena toba kwa pamoja,lakini wewe jenga utaratibu wa kiungu wa kujitakasa mapema. Pia patana na mshtaki wako mapema / uwaachilie wote waliokukosa.
Andaa moyo wako kupokea Neno – (Matendo 14:8-9)
N.K
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.
Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900
Na.Mch. G.Madumla
Whatsapp namba +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments