LINDA NAFASI YA HAKI YA UZALIWA WA KWANZA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 19, 2018
- 4 min read
Updated: Sep 5, 2022

Kwa ufupi…
Mzaliwa wa kwanza ni yeyote aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa. Katika kila kinachozaliwa kina nafasi yake ya kipekee, na ukweli ni kwamba watoto hawafanani kinafasi ingawa wamezaliwa na baba na mama mmoja. Mimi ni mzaliwa wa pili kwenye familia yangu, ninae dada mkubwa na ninao wadogo zangu wawili. Tulipokuwa wadogo, mama yetu alitupa kuku kila mmoja ili tuweze kufuga.
Nakumbuka kuku wangu walianza kutaga mayai wakaendelea kidogo kisha walikufa wote, na kwa dada yangu ikiwa hivyo hivyo, lakini mdogo wangu mmoja anayenifuatia, yeye aliendelea kufuga na kufuga, akazalisha kuku wengi wa kienyeji, mpaka leo yeye ana kuku. Dah! Inapendeza kwa kweli,;
Sasa nakaanza kujiuliza, mbona sote tulikuwa tukifuga kwenye banda moja la kuku, wanakula pamoja lakini kwa nini kuku zetu wote walikufa / uzazi ulipotea kabisa. Nikagundua kwamba tunatofautiana hata katika hali ya kuzalisha na kuendeleza jambo. Na ndio maana ukweli unabakia pale pale ya kwamba watoto hawafanani kiroho.
Mifano ya wazaliwa wa kwanza.
A. Wazaliwa wa kwanza kimwili;
Kaini mzaliwa wa kwanza kwa Abili (Mwanzo 4:1-2)
Yafethi mzaliwa wa kwanza kwa ndugu zake Shemu na Hamu ( Mwanzo 10:21)
Nahori mzaliwa wa kwanza kwa ndugu zake wawili Abramu / Ibrahimu na Harani.
Ishmaeli mzaliwa wa kwanza kwa Isaka
Esau mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo. N. K
B. Wazaliwa wa kwanza kiroho ;
Abili mzaliwa wa kwanza kwa Kaini ( Waebrania 11:4)
Shemu mzaliwa wa kwanza kwa ndugu zake ( Mwanzo 5:32)
Abramu / Ibrahimu mzaliwa wa kwanza kwa ndugu zake Nahori na Harani ( Mwanzo 11:26)
Isaka mzaliwa wa kwanza kwa Ishmaeli ( Ndiye aliyekuwa mtoto wa agano Mwanzo 17:21)
Yakobo mzaliwa wa kwanza kwa Esau ( Mwanzo 25:23)
Yesu Kristo ndiye ndugu mkubwa na mzaliwa wa kwanza kwa wote, maana katika Yeye utimilifu wote wakaa ( Wakolosai 1:18)
Kumbe! ahaa!
Kutokana na tofauti hizo, zinatuleta kuelewa vizuri kwamba kuna mzaliwa wa kwanza kimwili lakini pia kuna mzaliwa wa kwanza kiroho. Mzaliwa wa kwanza kiroho ni yule ambaye yupo kwenye agano na Mungu, kwa kuzaliwa kwa mara ya pili / kuokoka. Yeyote aliyempokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake amehesabiwa haki bure, naye hupewa nafasi ya mzaliwa wa kwanza hata kama kimwili alizaliwa mwisho kwenye familia,
lakini kiroho ni mzaliwa wa kwanza. Na ndio maana “ chunga sana!” usije ukamdharau mtoto wako aliyeokoka, yeye ni mkubwa kiroho kwa wengine watoto wako wasiokoka.
Kwa maana ikiwa Mungu anataka kusema nanyi kwenye familia yako atasema kwanza na huyo mtoto / kijana au binti aliyeokoka ndipo wengine msikie sauti ya Mungu. Usimdharau kwa muonekano wake wa nje, huyo ni mzaliwa wa kwanza!
Nafasi ya uzaliwa wa kwanza ilibeba haki ya;
Kiongozi wa ibada hekaluni au kwenye jamii. Anayesema na Mungu kwanza
Kufanya maamuzi ya mwisho kwa mambo yote ya ukoo. Wakati mwingine kuendesha vikao vya kiukoo na kutoa mashauri juu ya majina ya watoto wanaozaliwa ndani ya ukoo
Kusimamia mali za wazee au ukoo.
Mtawala wa mambo mengi N. K
Hivyo suala la uzaliwa wa kwanza halikuwa la kawaida kawaida fulani hivi, lilikuwa ni suala la “kushikilia haki katika ulimwengu wa roho ” ebu nikupeleke moja kwa moja kwa kisa cha akina Yakobo na Esau, ili Bwana aseme nawe kwenye maeneo hayo. Tunasoma ;
“Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza.
Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.” Mwanzo 25:29-34
Biblia inasema “Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza ” si kana kwamba alikuwa hajui umuhimu wa haki ya mzaliwa wa kwanza, bali alikuwa akijua yote lakini “aliidharau” kwa sababu ya njaa ya muda mfupi tu. Hivyo akakosa nafasi ya kiroho ya kutawala mambo ya ibada, nafasi ya kumiliki mali ya baba yake Isaka kwa kifupi alikosa sehemu kubwa ya mbaraka wake!
Yakobo anaonekana alikuwa akimtafuta siku nyingi “Esau aingie kingi / aingie kwenye kumi na nane zake” maana sio rahisi Yakobo akimbilie kumuuzia chakula tena chakula cha dengu, kwa kupata haki ya uzaliwa wa kwanza. Ni kama “mpango ” fulani alikuwa amekwisha usuka kitambo tu! Esau hajui hayo, yeye hakuona shida kumpa haki ya mzaliwa wa kwanza.
Ebu angalia mstari wa 13,Esau anaapa kwa Mungu yaani alikuwa akijua
kwamba “anaamisha nafasi yake ya uzaliwa wa kwanza kwa ndugu yake”. Kitendo hiki cha “kuapa” ni kuthibitisha kukamilika kwa mauziano yao. Hakuna kitu kibaya kama kiapo kwa mtu aapaye kwa Bwana alafu akarudi baadae anataka kitu chake kirejee!!!
Linda nafasi yako ya uzaliwa wa kwanza kiroho. Ikiwa umeokoka, u mzaliwa wa kwanza ; na ikiwa mtu anatokea na kukwambia mambo yasiyohusu wokovu uyafanye,
alafu nawe unasema kwani kuna shida gani, si ninafanya tu hata kama nimeokoka. Kwa kufanya hivi, unatakuwa ukidharau haki yako ya uzaliwa wa kwanza
Esau hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta sana kwa machozi ( Waebrania 12:16). Ndivyo ilivyo sasa nafasi ya kutubu inaweza kukosekana kwa mtu anayedharau wokovu wake. Ikiwa mtu anayedharau wokovu wake, kisha akafa- sasa atapataje nafasi ya kutubu? Hakuna!
Ni kwa namna gani unaweza ukaidharau haki yako ya uzaliwa wa kwanza?
Kufuata mashauri ya wasio haki ( kukubali kuuacha wokovu kwa sababu ya mambo ya tamaa ya kitambo tu)
Kuigeukia dhambi ambayo ulikwisha samehewa na kuhesabiwa haki bure.
Ni vyema ujifunze kulinda imani yako ya wokovu, kwa kukubali kulipa ghalama yoyote ile. Ebu jiulize; Je utauuza wokovu wako kwa pesa? Je utauuza wokovu wako kwa ukahaba au uhuni? Je utauuza wokovu wako kwa sababu mchumba wako hataki mambo ya kuokoka? Ni mbaya 😭😭😭!!!
Nafasi yako ya kiroho uilinde sana, shika sana ulichonacho! Ni muhimu kukubali kupoteza vingine lakini uwe na Yesu wako. Kwa maana vingine ni vya muda tu kama ilivyo kwa Esau, chakula kilikuwa ni cha muda tu. Angeliweza kuvumilia na asingekufa! Hata wewe unayo nafasi ya kuvumilia na kuendelea na Yesu ambaye atakupa mengi kuliko hilo moja.
Ikiwa umefanikiwa kujifunza kitu hapa kwenye maisha yako, ebu nifahamishe sasa, na ikiwa unahitaji maombi na msaada zaidi, usisite kunipigia kwa ;
+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments