KWANZA NDOA AU FAMILIA, KISHA HUDUMA NDIO IFUATE.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 24, 2018
- 5 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Ndoa ya mtumishi sasa inayumba sana, si ajabu ikavunjika. Hivi juzi juzi tu, maneno yalisikika yakisema mama mtumishi anatembea na mtu nje ya ndoa yake. Mimi na wewe hatujui ukweli uliopo hapo, lakini mambo ya ndoa yao si shwari hata kidogo. Kisa cha ndoa ya mtumishi kuyumba sio kwa sababu haombi, kuomba anaomba sana, ila chanzo ni kwa sababu kaitanguliza huduma sana na kuisahau ndoa yake pamoja na familia yake. Akiamini kwanza afanye huduma ya kiroho kwa watoto wake wa kiroho kanisani alafu ndio amalizie nyumbani. Sasa cha ajabu; akifika nyumbani huwa anachoka sana, na ndoa inamshonda sasa.
Mama mtumishi anamuhitaji mumewe, maana yeye sio roboti bado anahitaji penzi, lakini hapati, mama mtumishi amekosa ukaribu na mumewe mbaye ni mtumishi, na hapo ndio shetani alipoona mwanya wa kumfuata mama mtumishi kwa kupitia mkaka fulani hivi, aliyeanzia mbali kwa lengo la kumfariji mama kwamba avumilie. Lakini mkaka huyu naye kaokoka fulani hivi, hajatulia kwa kweli. Na kwa sababu alikuwa akijua kujali sana, mama mtumishi akakamatika hapo huku baba mtumishi akiendelea na ubize wake wa kihuduma wala hajui kama kuna adui amekwisha ingia. Unajua mimi hapa, Najaribu kufikiria mfano huu wa kufikirika ambao si kisa halisi nilichokiona kanisani, lakini nashuhudiwa ya kwamba wako watumishi wengi wa sampuli hii, ambao ndoa zao haziko sawa kwa sababu mtumishi kasahau ndoa na kaitanguliza huduma. Kwani wewe, U mgeni wa mambo haya? Hukuwai kusikia au kuona ndoa oliyopangalanyika kwa sababu ya ubize tu wa huduma.
Jamani, tuambiane ukweli hapa ; unajua mwenzako wa ndoa naye ni mtu ambaye anakuhitaji sana, anahitaji sana ukaribu wako, anahitaji penzi lako, lakini ikiwa utajifanya uko bize na mambo yako, ujue ni wewe ndio unamtengenezea nafasi ya kutoka nje ya ndoa, au nafasi ya kuangushwa na shetani kwa namna yoyote hile kwa sababu hamjaambatana vizuri. Unakumbuka wanaume tuliambiwa nini kwenye walaka wa Paulo kwa Waefeso 5:25? Nikukumbushe kidogo kilichoandikwa ;
“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake”
Sote tunafahamu Mungu anataka kwanza tumpende Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa roho zetu zote, kwa nguvu zetu zote na kwa akili zetu zote. Lakini kwa habari ya huduma, kwanza tuwapende wake / waume zetu kisha huduma ifuate. Na ndio maana Paulo hapo anasema wanaume wawapende wake zao, sio kulipenda kanisa bali mke / mume awe na nafasi ya juu. Hii haina maana kwamba huduma ya Bwana tuidharau kwa kuiweka mwisho, hapana! Bali ina maana ya kumuhudumia vyema mumeo / mkeo ndipo ukiweza hapo, basi ujue na huduma utaiweza vyema. Ebu fikiria wewe mwenye ndoa, na unajulikana kuwa ni mtumishi fulani hivi, fikiria umeishindwa kuhihudumia vizuri ndoa yako, Je utawezaje kuwahudumia watu wengine? Je haitakuwa unafiki huo?
Fikiria anakujia mwanandoa fulani aliye na matatizo kwenye ndoa yake, mtu huyo amekujia umshauri na kumuongoza lakini na wewe mambo yako ya ndoa yamekushinda, Je hapo kuna Roho wa Mungu kweli? Je hutadanganya danganya yaani ningelitumia neno la kikwetu kwetu “kujibalaguza” Je hutajibalaguza balaguza wewe, uonekane na wewe ni mwenye ndoa nzuri? Sasa utawezaje kumuhudumia huyo? Fikiria hayo mazingira, ndio maana tunasoma hivi ;
“ Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” 1 Timotheo 5:8
Yaani ukishindwa ndoa yako mwenyewe, huwezi kuitatua ndoa ya mwingine. Tena si hilo tu, usipowatunza watu wa nyumbani mwako mwenyewe, huwezi kuwatunza wa nje. Ukishindwa kuwahudumia wa nyumbani kwako mwenyewe, utawezaje kuwahudumia watu wengine wa nje? U mtumishi wa namna gani? Ebu jiulize. Fikiria wewe ni mtu wa huduma na wewe, wewe na huduma, umekata miezi kadhaa hujawahi kutumia masaa kukaa na mwana ndoa mwenzako, tena wakati mwingine hata watoto wako wamekuwa wakihudumiwa zaidi na mwenzako wa ndoa, huyo mkeo ndio kila kitu cha nyumbani afanye wewe, na mbaya zaidi ukirudi upo hoi, mara simu haziishi kuingia “ mtumishi, ninaumwa niombee” mara tena “ mtumishi jana niliota ndoto, ngoja nikusimulie” tena “ babaangu, nikusalimia, kwani umelala? Nilikuwa nataka nikusimulie yaliyonitokea wiki mbili zilizopita baada ya kunoombea, yaani,… We acha tu! Mhh… ” n. k. Huku mkeo yupo hapo anakusubiri umalize mambo yako, mwishoe anapitiwa na usingizi, watoto na wenyewe wamekusubiria mpaka wamejichokea wakaamua wajilalie. Sasa, mhh, sio vibaya vyote hivyo, lakini familia yako je mbona imekosa nafasi kabisa!! Mkeo / mumeo je, mbona amekosa nafasi!!! Kwani nikuulize, mkeo mekukosea nini? Kosa lake liko wapi hata umuweke nyuma hivyo? Au unafikiri Mungu anaiangalia huduma yako zaidi ya ndoa yako?
Watu wengi wamekuwa na mtazamo ambao sio sahihi wala si mtazamo wa Kiungu . Wakitazama Huduma ya Bwana walioitiwa kana kwamba ni ya kwanza kabisa kuliko ndoa au familia zao. Na hapo wamejikuta wakiangukia pabaya, na kuwalaumu wenzi wao. Wakati mwingine watumishi hufikiri mambo ya familia ni mambo ya mwilini, na wao ni watu wa rohoni hivyo haiwapasi kufanya mambo ya mwilini. Jamani!!! Kha,! Hujawahi kuona mtu akisema “ mambo ya mke ni mwilini tu, ” alafu cha ajabu ukimuuliza kwamba ikiwa ni mambo hayo ni ya mwilini mbona umeoa? Au mbona umeoolewa? Biblia imekaza kusisitiza ndoa, na familia kama sehemu ya kwanza ya huduma yako kabla hujaenda kanisani.
Mimi huwa siwaelewi watu wanaowaacha nyuma wake zao. Au wake wanaowaacha nyuma waume zao kisha wao wakikazana kumtafuta Mungu wenyewe wenyewe. Nakwambia ukifanya hivi, huyo Mungu mwenyewe humuoni ng’oo!!! Ni agizo kwako kumpenda mkeo, hii ikiwa na pamoja ya kumtanguliza mbele kihuduma. Isotokee kila uendako uko wewe tu, alafu mama yupo nyumbani eti kwa sababu yeye mama sio mchungaji. Wewe! Utakuja kutegwa na wategaji, alafu ndipo utajuta. Maana kama wewe ni mwanaume ; kuna wadada wazuri ambao ni mawakala wa shetani watakaokutega kimapenzi wakija kama watumishi wenzako, au kama wadada wanaohitaji maombezi kutoka kwako, kumbe wanakuchota tu!!! Wanakuangalia, alafu wanasemezana wao kwa wao “ Mmh, hata kuomba yenyewe hajui, akana hata nguvu ya kumtoa pepo, ngoja sasa tumuingize king, hatujui huyu eeh… ” na ni hivyo hivyo kama wewe ni mwanamke unayemuacha nyuma mumeo eti kwa sababu yeye hajaokoka. Basi kuokoka kwako ndio imekuwa nongwa! Hata unamuona mumeo ni mmataifa fulani hivi, Wewe! Utategwa na utumishi wako!!! Najua unaweza kusema “ sitegeki kabisa ” Waulize walioanguka, wakwambie waliangukaje kama hujaona kwamba na wenyewe walijisahau kwenye ndoa wakatanguliza sana huduma na leo wanalia 😭😭😭
Hivyo, ni vyema ufahamu kwamba, mumeo / mkeo ananafasi kubwa sana kwako kuliko wengine wote. Yeye ndio namba moja yako, pili familia uliyonayo. Na tatu ni huduma huko nje, iwe kanisani iwe ni kwenye fellowship / cell au popote pale. Ukitaka huduma yako ikuwe vyema na kuongezeka upako, anza leo kumpa nafasi mwenzi wako wa ndoa, yaani kumjali na kumfikiria yeye kwa lengo la kuwa pamoja kwenye huduma na hapo utaona badiliko. Wakati mwingine unapoona mambo hayaendi vyema kwenye huduma sio shetani au mchawi kakuloga, bali ni wewe mwenyewe umejikologa kwenye ndoa yako au familia yako. Ebu fikiri, ikiwa mmepishana kiswahili / mmetukanana / hamjaelewana na mwenzako alafu papo hapo ukamwacha nyumbani na kumuona mwenzako ni mjinga tu, kisha ukaenda kuhudumu,
Je hapo kuna nini? Roho mtakatifu yupo hapo kweli kwa kile unachohudumu, au ni maigizo tu? Lakini ndivyo ufanyavyo, au ndivyo wengi hufanya hivyo, na ndio maana leo ibada za kweli ni chache bali nyingi ni maigizo matupu. Yaani ungelipata kuona yale yalitendeka dakika chache kwenye ndoa ya fulani, alafu mtu huyo huyo ndio yupo mbele za Mungu eti akihudumu na kusema “mpende mkeo / mumeo. Kama mimi ninavyompenda mwenzangu, si mmnaona tunavyopendeza bhana,… Hahahaa mpigie Bwana makofi mengii ” Jamani, yaani!!! Ndio kama wewe umefanya hivyo, Mungu anakuaangalia, hakupatii picha kwa sanaa zako za madhabahuni. Sasa, mtangulize mkeo / mumeo kwanza kisha huduma yako ifuate.
Kwa msaada zaidi, pamoja na maombezi, waweza kunipigia sasa kwa namba zangu zilizopo hapo juu kabisa. Hapo ipo namba ya whatsapp pia kama utapenda kutumia.
Namba +255 683 877 900
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Commentaires