KWA NINI UNAJIUA? – 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 7, 2018
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Kuna wakati fulani nilikuwa napenda kitu kinachoitwa “soda” na soda yungu haikuwa nyingine bali ni “pepsi” yaani hawa jamaa wa sijui waliniwekea nini,kwa sababu nikiiona tu pepsi haswa ile ya bariiidi,basi hapo napate kiwewe,koo langu lilikuwa halitulii,nitafanya jitihada zangu zote mpaka niipate. Alafu cha ajabu hata nikinywa mbili,baada ya muda kiu ipo pale pale,kwa kweli ninyi watu wa soda “mnachofanyaga Mungu ujue anawaona” kwa sababu kiu haikatiki,sasa mnachanganyaga mavitu gani kwenye soda? Pepsi alikuwa mpenzi wangu aliyenisumbua sana,kwa kuniangaisha nimtafute!!!
Lakini ilifika wakati nikagundua madhara ya utumiaji wa soda,nilishtuka kidogo. Nikagundua kwamba nilikuwa ninajiua mimi mwenyewe. Maana niliona hatari ambayo ingelikuja baadae,na hapo nikafanya maamuzi magumu ya kupunguza matumizi makubwa ya soda pamoja na sukari. Siku moja nilikuwa nafuatilia takwimu za vifo duniani,nikatambua vifo vingi vinatokana na maamuzi yetu ya kujiua pole pole hasa kwa vyakula tunavyotumia. Jaribu kucheki watu wanavyoanguka katika hatari ya vyakula huko barani ulaya,kwa mavyakula ya kopo…Ni hatari nakwambia. Cheki kansa inavyotafuna huko magharibi ( katika nchi zilizoendelea).
Wewe je unajiua kwa kutumia nini?
Karibuni 85% ya watu duniani wanajiua wao wenyewe kwa matumizi mabaya ya vyakula na vinywaji pamoja na hali ya hewa. Hali inatisha kwa kweli!!! Kitu cha ajabu ni kwamba,kila unachotaka kutumia;tayari umekwisha pewa maonyo/tahadhari. Tena tahadhari hizo ni mbaya kwa afya yako,lakini wewe bado unangangania kutumia hali ukijua nini kitafuata baadae “ huku ndiko kujiua pole pole,mwenyewe ” Ebu angalia hilo!!!
Ni dhambi kama ukijiua
Kujiua kwa namna yoyote ni dhambi mbele za Mungu kwa sababu hukupewa mwili uutumie vibaya kwa matumizi yako yasiyofaa. Biblia inasema;
“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;“ 1 Wakorintho 6:19
Ikiwa mwili wako nk hekalu la Roho mtakakatifu,basi ujue ukiliharibu hekalu hilo,ni lazima utatoa hesabu zake siku ya hukumu. Kuna watu wanatumia vinywaji vyenye sumu kwa lengo wanalodai la kujifurahisha au kuondoa mawazo,na inafika wakati wanapata shida kwenye miili yao,wengine hupata magonjwa,wengine wakiunguza mapafu,ini,figo n.k Maskini hawajui,watakuja kudaiwa hiyo miili kwa sababu ni mali ya Mungu. Ebu fikiria mtu ambaye ni wa kula kula tu bila mpangilio mzuri,Je atakuwaje? Bila shaka utamkuta ni mnene,presha hapo utaikuta,kuchoka na magonjwa mengine nyemelezi lazima uyakute hapo. Je huko sio kujiua mwenyewe???
Umeshawahi kujiuliza kwamba; kwa nini unatumia sana kinywaji ambacho unajua madhara yake! Au utumiaji wa vyakula ambavyo kwa kweli umekwisha pewa madhara yake !! Ikiwa ndivyo,kwa nini basi unaendelea mpaka sasa? Una mpango gani na maisha yako? Au unafikiri baada ya miaka 10 utakuwa wapi,afya yako itakuwaje?
Kujiua si lazima ujinyonge au unywe sumu bali kile unachotumia chenye kuua taratibu kinga zako za mwili.
Ni vyema utambue ya kwamba,yule atakayejinyonga amejiua na yule anayetumia kitu hali akijua madhara yake kwamba yatampelekea pabaya naye amejiua. Hivyo kama huyu mmoja aliyejinyonga atahukumiwa wewe je unayetumia kitu kinachokuangamiza taratibu utapona na hukumj hiyo? Ukipiga hesabu vizuri utakuja kujua kwamba, kuna kitu unachopenda kukitumia ambacho kwa kweli kinakupeleka kaburini tu. Na ndio maana leo vifo vimeongezeka sana. Nenda hospitali leo na kuuliza magonjwa yametokea wapi kama hujaambiwa ni vyakula,vinywaji na hewa tunayovuta kama chanzo kikuu cha magonjwa na vifo.
Vile unavyoweza kuepuka,viepuke kuanzia leo.
Kuna matumizi ambayo unaweza kabisa kuyaacha. Kwa mfano ulaji wa vyakula vya kusindika,unywaji wa kupindukia wa soda na vinywaji vya sukari nyingi. Au kwa mfano,uvutaji wa sigala,pombe ,bangi n.k Havina umuhimu wowote kwenye mwili wako sana sana vitakumaliza tu,na mwisho wa siku utahukumiwa na Mungu. Hata hivyo kwa hali ya leo ya dunia yetu iliyoharibika tayari,kuna mambo fulani ni vigumu kuyakwepa,mfano vyakula vingi tunavyonunua vimekwisha wekewa dawa hasa katika uandaaji wake huko shambani. Leo ukila nyanya huipati ile radha halisi ya nyanya kwa sababu upandwaji wake umetawaliwa na madawa mengi. Au ukila wali “ubwabwa” haunogi kivile,kale kawali ka kipindi kile hakipo tena,maana mpanga wa leo ni dawa ndio imetumika huko,ni vivyo hivyo kwa vyakula / mahitaji mengine. Katika haya huna budi kuyatumia hivyo hivyo kwa msaada wa Mungu tu,atulinde.
Lakini kwa nini unajiua hali ukijua unajiua kwa mambo ya kuepukika?. Watu wengi wakiangukia ugonjwa,hapo ndipo utakapowaona wakienda huku na kule kwenye huduma za maombi. Ujue maarifa yalikosekana hapo mwanzo,na kwa sababu hiyo watu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Hakuna haja ya kujiua kwa maana bado hujamaliza kazi ya Bwana. Hivi unajua huwezi kuifanya kazi ya Bwana kikamilifu ukiwa ni mgonjwa? Ndio… Anza leo kupunguza na kuacha kabisa matumizi yanayokuangamiza…
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezi pia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 655 111 149 / 683 877 900 / 762 414 446.
WhatsApp ni +255 655 111 149.
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments