ANAYETAKA KUWA MKUBWA,NA AWE MTUMISHI.
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 27, 2018
- 2 min read
Shalom, shalom…
Kwa ufupi sana.
“ Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.“ Mathayo 20:26-28
Je unataka kuwa mkubwa? Je unataka kuwa mtu wa kunyenyekewa? Je unataka kuwa kiongozi mzuri? Je unataka kuwa mfano wa kuigwa? N.K Basi ujue kuna gharama ya kukubali kushuka na kunyenyekea kwa kuwa mtumishi wa watu, na kutumika.
Maandiko hayo hapo juu yanatuonesha namna ambavyo watu hupenda kuwa wakubwa,watu kupenda kutumikiwa,watu kupenda kuwa wa juu juu. Lakini Yesu anatufundisha jambo tofauti kabisa na vile watu hupenda Kitu kilichomsumbua mama yule mama wa wana wa Zebedayo ni ubinasfi na uchu wa madaraka kutaka wanae wawe juu ya wengine ( Mathayo 20:20-28)
Kile ambacho Yesu anakufundisha leo kwamba, kama kweli unataka leo uwe wa kwanza,basi ukubali kuwa mtumwa na kama unataka kuwa mkubwa basi ukubali kuwa mtumwa.Ebu fikiria wazo hilo! Yesu anajua jinsi gani watu hupenda kuwa wakubwa kama ilivyokuwa kwa wana wa Zebedayo,ambao mama yao alimwomba Yesu awaketishe wanae kwenye viti vya juu.
Kumbe,Yesu hakuja kutumikiwa bali kutumika. Na hii ndio siri ya ushindi ya huduma ya Yesu. Yeye mwenyewe aliweka mfano wa namna ambavyo mtumishi wa Mungu anavyotakiwa. Anaonesha alikubali kutumika na kutoa nafsi yake kuwa fidia ya wengi. Yesu alikubali kuwanawisha miguu wanafunzi wake,kuweka mfano wa kutumika wala sio kutumikiwa. Na huyu ndio kiongozi tunayemtaka.
Maskini jamani!!! Hali imebadilika leo !!! Watu wengi tena bahati mbaya ni watumishi wa Mungu wanatafuta kwa kila njia waonekane wakubwa kuliko wengine, wengine hutoa na pesa kutengeneza hata miujiza feki ili wapate majina. Jamani!!! Ndivyo tunavyofundishwa na Yesu? Wengine hupenda kuwa wakubwa makanisani waonekane wao kuwa ni bora na ni wa juu kuliko wengine.
Mimi sioni shida ikiwa utakubali kushuka na kupenda kutumika hata kama u nani. Kwani unapungukiwa nini ikiwa utakuwa mtumishi wa wengine? Je si zaidi sana utainuliwa? Laiti kama unanielewa leo,basi kubali kutumika na kataa kabisa kutumikiwa,na inawezekana. Yupo wapi mtu kama Yesu, anayekubali kuitwa Rabi tu? Bila kuitwa majina ya ajabu ajabu wanayojipachika watumishi wa leo majina kama; buldozer,kiboko ya wachawi,mzee wa…,dr.professional nakadhalika.
Yaani ukweli kama mtu aliyestahili kuitwa majina hayo alikuwa ni Yesu kwa kuwa anastahili kuwa daktari,na majina yote. Lakini ebu cheki,jinsi ya unyenyekevu aliokuwa nao,bali alitaka nafsi yake iwe fidia ya wengi. Je wewe unaweza kuwa kama Yesu? Mbona unapenda makuu?
Mimi nashangaa kuona watu wenye kupenda makuu alafu hawana lolote!!! Utakuta mtu katoa pepo mmoja tu,basi ndio watu hatusemi! Kesho kashabadili na jina tena na mwondoko!!! Jamani khaa! Kapepo kamoja tu kanakupandisha mabega? Haifai. Kubali kujishusha na utauona mkono wa Bwana. Unanielewa lakini?
Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezi pia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 683 877 900
WhatsApp ni .+255 746 446 446
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments