KWA NINI UMETANGULIZA HOSPITALI MBELE YAKO BADALA YA KUMTANGULIZA MUNGU KATIKA HUO UDHAIFU?
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 14, 2017
- 4 min read

Na Mch.G.Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa nini unapopata homa kidogo unaanza kukimbilia hospitali? Kwa nini unapojisikia mafua tu unakimbilia duka la dawa? Kwa nini unapojisikia vibaya unakimbilia duka la dawa au hospitali? Je unafikiri Mungu hawezi kuponya? Au Je unafikiri Mungu anaponya mambo ya kichawi kichawi tu? Je hujui hata katika hayo mabadiliko madogo madogo ya kujisikia vibaya yapo katika uwezo wa Mungu?
Lazima ifike wakati ufahamu na uamini kwamba hakuna lisilowezekana kwake aaminiye ( Marko 9:23). Kila aina ya ugonjwa au udhaifu wowote ule,Mungu katika Jina la Yesu Kristo anaweza kukuponya. Hakuna jambo gumu asiloliweza Mungu. Ikiwa ni hivyo basi kwa nini usimuamini Mungu katika huo udhaifu,ugonjwa kwa kuwa ni Yeye ndie awezaye kuponya. Lakini nimeliona tatizo la watu wengi hata wale wapendwa wamekamatwa na tatizo hili,nalo ni “ kukimbilia hospitali na sio kukimbilia hospitali ”
Tumekuwa wepesi sana kukimbilia hospitali na sio kukimbilia kwa Mungu,maana tumebadilishwa akili na ufahamu wetu hata kufikiri kwamba Mungu hawezi kutuponya bali madactari. Je ni kweli? Kama si kweli na ni kwa nini hata wewe umekuwa na haraka sana kumuendea daktari au kununua dawa kila ujisikiapo vibaya na kuhacha kuomba ? Ikiwa utalifahamu hili ninalokuambia leo,hakika utatoka katika eneo moja na kuvuka hata eneo la pili kiimani.
Kama umejaribu sana kwenda kwa matatibu wengi na umekosa msaada wa kweli naomba nikushauri siku ya leo kwamba sasa mgeukie Mungu Yeye Mungu atakuponya,wewe amini tu hivyo na itakuwa kwako. Lakini katika hili,liwe kwako kama fundisho kwamba chochote unachopitia usianze na mkono wa mwadamu bali Mungu. ukiamka na kujisika haoko vizuri,hapo usikimbilie dawa bali mkimbilie Mungu katika maombi na maombezi. Nataka nikuambie ukijizoeza katika jambo hili,basi utamuona Mungu akitenda makuu maishani mwako.
Biblia inatuambia nini juu ya uponyaji katika magonjwa kama homa n.k. Tusome andiko moja kati ya mengi yanayoeleza kuhusu uponyaji;“ Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.” Matendo 28:8
Biblia haituambii kwamba baba yake Publio alikuwa amelogwa,wala hatuambiwi kwamba ugonjwa wake uliletwa na mapepo bali tunaambiwa alikuwa akiumwa homa ya kawaida na alikuwa akihara damu. Hayo ni magonjwa ya kawaida kabisa ambayo hata katika jamii yetu yapo. Na ni magonjwa ambayo yamkini unayapitia mara kwa mara,Lakini swali la kujiuliza Je unapopata homa tu,unafanya ni nini? Je unaomba au unaanza kuelekea hospitali alafu ukishatibiwa ndio unaomba? Neno la Mungu halitufundishi hivyo kwamba ukijisikia vibaya uanze na hospitali au dawa bali Neno linatufundisha ukijikia vibaya,tuanze na Mungu katika maombi; tazama jinsi ambavyo neno linavyosema; “… Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.” Paulo alipoomba,ile homa na kuhara kwa damu kulikatika. Kumbe hutakiwi kuiweka hospitali namba moja.
Je nikiumwa nisiende hospitali? Au kwenda hospitali ni kupungukiwa na imani? Au je kwenda hospitali ni dhambi?
Jibu; Kwenda hospitali sio dhambi wala sio kupungukiwa na imani kwa sababu Mungu ameruhusu watu wake wawe na ujuzi wa kutibu lakini katika tiba ni Yeye Mungu ndiye aponyaye. Waweza kwenda hospitali unapohitaji kwenda, lakini hospitali isiwe ngome ndani yako kiasi kwamba unapojisikia vibaya kuanza nayo. Unatakiwa unapopata homa uanze na Mungu kabla ya chochote.
Ni makosa kuanza kutumia dawa au kwenda hospitalini ikiwa bado hujaomba. Ukiomba vizuri hata kama utaenda hospitali basi uwe na uhakika kwamba utapata wepesi wa uponyaji wako.Paulo anamuombea mtu ambaye anaumwa homa tu. Na anakaza kumuwekea mikono ili apokee uponyaji,akikufundisha kwamba hata upatapo homa tu,unahitaji usimame katika maombi. Ikiwa wewe ni mtumishi wa Mungu,hupaswi kuwaelekeza watu waende hospitali kama kigezo cha kwanza bali uwaombee kwanza.
Ni kawaida yetu watu wengi tunapojihisi vibaya;tunaanza na kwenda kuchukua vipimo vya kidackari na tunamsahau Mungu. Tena baada ya kutibiwa na kuona hatuponi vizuri ndio huwa tunageuka kwa Mungu na kuanza kukimbia katika maombezi!!! Ikiwa na wewe unafanya hivi,badi itakuwa ni sawa na kumuweka Mungu nafasi ya mwisho. Kwa maana umeitanguliza hospitali alafu ukishindwa huko ndipo ukimbilie kwa Maombezi.
Leo Bwana anakutaka ugeuze mtazamo wako katika kila udhaifu,iwe ni malaria,homa,mafua n.k. mtazamo wako umtazame Mungu kwanza mambo mengibe yafuate.Mimi ninasemaga kila siku kwamba ikiwa kama tutamtanguliza Mungu vyema katika maombi sawa sawa na msukumo wa Roho mtakatifu basi ni dhahili maduka ya dawa yasingelikuwa na wateja wengi hivyo,tena hospitali zisingelikuwa na wateja (wagonjwa) wengi kiasi tulichonacho leo.
Je unafikiria wote waliopo hospitalini ni wagonjwa? Au Je unafikiria wote wanaookimbilia kumeza dawa ni wagonjwa wote ?
Hapana,si kweli kwamba wote ni wagonjwa. shetani ni muongo siku zote,kwa maana wengi wanajisikia kuumwa lakini kwa kweli hawaumwi. Sasa,kwa sababu shetani anakusudia kuwaangusha na anapanda wazo la ugonjwa,na hapo ndipo unajikuta unafungwa akili na ufahamu wako katika maombi. Unajikuta huombi kabisa na gafula unakimbilia hospitali. Laiti kana ungeliomba yamkini usingelienda huko hospitali. Laiti ungeombewa na mtumishi yamkini usingekuwa na uhitaji wa hospitali kabisa.
Kuna nguvu katika maombi yanayoongozwa na Roho mtakatifu,na ndio maana shetani hapendi kuona unaombewa,au unaomba juu ya udhaifu au ugonjwa. Yeye Yesu alipigwa msalabanj ili wewe upone (Isaya 53:5)Fundisho hili limekuja kwako kipekee ili ubadilishe njia zako katika imani. Badilisha kule uendako na uanze na Bwana katika kila jambo. Pale unapopata udhaifu wa aina yoyote ile,anza na Mungu katika jina la Bwana Yesu Kristo maana ndivyo tulivyoagizwa “ kila ufanyalo kwa neno au kwa tendo fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu....” Wakolosai 3:17
Kwa msaada wa maombezi piga sasa +255 683 877 900
Mch. Gasper Madumla.
What’s app number ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments