KUTEMBEA NA MUNGU. ~01
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 8, 2018
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Mojawapo ya siri ya kutembea na Mungu kwenye maisha yako ni ushindi dhidi ya maadui zako. Pale usipodhania kwamba kuna mahali fulani umetegwa, na wamekuchimbia na mashimo utumbukie lakini hapo ndipo wanatumbukia wenyewe alafu unashangaa!, kwa maana kwa sababu hukuwatumbukiza wewe kwenye mashimo yao wenyewe bali Mungu amewatumbukiza kwa maana madui zako wamekuwa ni maadui za Mungu. Pale ambapo vikao vinakaliwa kwa shauri la hila juu yako, lakini ndio hapo hapo Mungu husimama kinyume na mashauri yao, kisha hata hapo unapigwa na butwa!!!
Kuona wakichanganyana wao kwa wao, maana Mungu yupo pamoja nawe. Ebu angalia mti aliousimamisha Hamani mtesi wa Wayahudi kwa ajili ya kumtundika Mordekai, badala yake yeye mwenyewe ndio alitundikwa kwenye mti alioufanya mwenyewe ( Esta 7:7-10). Wakati adui yako amepanga mabaya juu yako, ndio wakati Mungu humgeuzia hayo mabaya mwenyewe, na ndio maana ni hatari sana kushindana na mtu anayetembea na Mungu, ogopa yale uyawazayo, uyanenayo au uyafanyayo juu yake yasije yakakurudia mwenyewe ukapata aibu!!!
Ikiwa wamekaa kwa ajili kutengeneza uongo juu yako, usihofu katika hilo- wewe endelea kumwadhimisha Bwana kwa furaha yote kwa kuwa hakuna baya litakalofanikiwa, bali utashinda katika hilo. Ni kuamini tu, na hiyo ndio mojawapo ya siri ya kutembea na Mungu. Unamjua Yakobo? Ngoja nikwambie habari zake kidogo. Yakobo yule aliyechukua mbaraka wa nduguye Esau kwa kuwa Esau aliudharau. Yakobo alikuwa ni mbarikiwa na mtu mwenye neema ijapokuwa alidanganya danganya. Bwana Mungu alimwambia Yakobo arudi kwenye nchi ya baba yake pale muda ulipoisha kwa kumtumikia Labani. Neno linasema;
“ Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; ” Mwanzo 32:9
Yakobo alipokuwa akitoka kwa mjoba yake Labani alikuwa akitembea na Mungu kwa maana aliifanyia kazi sauti ya Mungu ya kutoka na biblia inasema “Bwana atamtendea mema” hii ni sawa Bwana alikuwa pamoja naye katika safari yake ndefu. Haikuwa rahisi safari hii, kwa sababu Yakobo alikuwa na kundi kubwa la watu aliowapata kwa Labani wakiwemo watoto, wake,
vijakazi, mifugo. Safari ilikuwa nzito na isitoshe ilikuwa jangwani lakini watoto walikuwa ni wadogo wa kunyonya, mifugo na yenyewe ikuwa ni mingi na baadhi ya wanyama walikuwa wananyonyesha. Katika safari kama hii, bado Mungu alikuwa pamoja na Yakobo kumtendea mema. Unaweza ukawa na safari ndefu sana katika maisha yako, lakini assurance / uhakika wako ni Mungu kuwa nawe, na hapo ndipo utaona wepesi wako.
Kipindi ambacho Esau amepanga kuonana na nduguye Yakobo kilikuwa ni kipindi kigumu sana, kwa sababu Esau alikuwa akitafuta kumuua Yakobo na ndio chanzo cha Yakobo kukimbilia kwa Labani. Sasa fikiria mazingira kama hayo, Yakobo kuonana na Esau mtu ambaye anatafuta kumuua, haikuwa rahisi hata kidogo. Na kwa sababu hiyo ilimwogopesha Yakobo hata ikafika wakati Yakobo akapolomosha maombi kweli kweli mbele za Bwana ( Mwanzo 32:10-12).
Kumbuka ndugu hawa wawili Yakobo na Esau wameachana muda mrefu, sasa Yakobo hajui kilichokuwepo ndani ya Esau, lakini bila shaka Yakobo alikuwa akiiona hasira ya Esau, tena akiona kifo chake au watoto na kundi la mifugo yake, anawaza na kuwazua afanye nini hata aepukane na mkono wa Esau, na Esau ndio huyo yupo karibu anakuja na watu mia nne pamoja naye.
Hivi unaelewa kweli ninachokueleza hapa? Hivi ungelikuwa ndio wewe umesimama kwenye nafasi ya Yakobo ungelifanyeje? Usingekimbia kweli na kuliacha kundi ili uiponye nafsi yako? Bila shaka mkristo wa leo angetimuka mbio, ajiponye nafsi yake. Sasa angalia siri iliyopo ndani ya mtu anayetembea na Mungu, ni ushindi dhidi ya adui zake. Yakobo alipokaribia kundi la Esau, gafla Esau huyu hapa! Wote wawili wakaangukiana shingo, biblia inasema “Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu, nao wakalia. ” Mwanzo 33:4
Esau aliyekuwa akitazamiwa kuleta tufani ya kifo lakini ndio huyo huyo amekuwa wa kwanza kumlaki nduguye Yakobo tena kwa kumbusu na kulia machozi mwa! mwa! mwa! Ni nani angetegemea kuona hili? Bwana Mungu alisimama upande wa Yakobo kiasi kwamba adui yake akawa ni rafiki. Hapa pana siri, sio kawaida tu,maana haiwezekani kwa mtu ambaye Yakobo alimkimbia muda mrefu kuja kwa staili hii,
kama si Mungu kuwa pamoja na Yakobo, basi ni kweli Esau angemmaliza Yakobo na yote aliyokuwanayo! Siri hii ni ya ajabu, yashangaza sana; kwa maana Mungu aliweka wepesi na njia kuhakikisha adui amekamatwa tena na kudhibitiwa ipasavyo. Lakini ebu jiulize ; Je Mungu asingelikuwa na Yakobo, Je Yakobo na mali zake zingepona? Je Esau angewatenda nini? Mimi Nafikiri Esau angewatenda vibaya sana hata kuwaangamiza wote akina Yakobo.
Ipo siri ya ushindi mbele ya adui zako pindi unapotembea na Mungu. Unajua Yakobo hakutoka kwa Labani kwa mashauri au maamuzi yake mwenyewe bali alitoka kwa kuisikia sauti ya Mungu naye akatii, na kwa hiyo adui yoyote aliyopo mbele yake alikuwa ni adui wa Mungu kwa sababu Yakobo yupo kwenye sauti ya Mungu kama barabara anayotembelea.
Mimi sijui upande wako kama unatembea kwenye barabara ya Mungu / unatembea na Mungu katika kusikia na kuyafanya yote unayoambiwa. Unajua wakati mwingine adui wako wanatepeteshwa / wanasawazishwa na Mungu pasipo wewe kujua kwa kuwa upo pamoja naye. Ushawahi ona mtu aliyekuwa akitafuta akuangamize lakini ndio huyo anakuangukia akilia mbele zako na kuhitaji msaada wako? Je hiyo siri ni ya nani kama si siri ya kutembea na Mungu?
Kwa msaada zaidi na maombezi pamoja na maongezi tafadhari piga
Kwa +255 683 877 900.
What’s app ni +255 746 446 446
ITAENDELEA…
UBARIKIWE.
Comments