KUTEMBEA NA MUNGU. ~ 02
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 13, 2018
- 2 min read
… Karibu,
Kwa ufupi.,
Nuhu alitembea na Mungu (Mwanzo 6:9),lakini ukweli ni kwamba ni Mungu ndie aliyemwezesha Nuhu kuishi kikamilifu,katika hili hatuna shaka kwa sababu huwezi kumpendeza Mungu pasipo kuwezeshwa na Mungu mwenyewe na ndio tunaiita neema. Ila ni lazima ukubali pia kuna nafasi yako ya kutembea na Mungu na hapo ndipo kuna siri za ajabu tunazojifunza.
02. Unyenyekevu.
Tabia ya kwanza ambayo itaonekana wazi kwa mtu yule anayetembea na Mungu vizuri ni kuwa na `Unyenyekevu wa moyo ” tabia hii haifichiki. Yesu naye ni mfano wa mtu mnyenyekevu aliyeishi hapa duniani (Mathayo 11:28). Unyenyekevu haupimwi kwa sababu ya jina zuri ulilopewa na wazazi au haupimwi kwa sababu ya kushiriki ibada za Jumapili,la hasha!! Bali unyenyekevu unaonekana wazi unapokubali kutii. Ukitii maelekezo ya Mungu basi ni dhahili utakuwa ni mnyenyekevu.
Unyenyekevu sio upole,bali unyenyekevu ni tabia ya Mungu ya kushuka na kuwatanguliza wengine,kuwaona wengine wanafaa,wazuri,si tabia ya mashindano bali unyenyekevu ni kinyume cha “kiburi ”. Unajua kiburi ni tabia ya shetani?
Na kiburi ndicho kinachotesa watu hasa watumishi wa Mungu,yaani kule kupenda sifa,kujiinua,kujiangalia mwenyewe tu.ebu angalia mfano huu ; Siku moja tukiwa tumetoka kwenye mkutano wa injili Jangwani- Dar es salaam,tukiwa tumepanda gari ya pamoja DCM madaladala,ndani ya bus tulikuwa wengi na wengi tulikuwa watumishi wa makanisa mbali mbali.
Sasa nilibahatika kupata siti nami nikakaa,gafla mama mmoja akaanza kunisemesha nami nikamsikiliza. Yule mama alikuwa ni mchungaji maana ndivyo alivyojitambulisha bila hata kuulizwa,Sasa, akaanza kunionesha video na picha za kanisani kwake akiwa “anawafungua watu mbali mbali waliokuwa wamefungwa na nguvu za giza”,kisha akasema “Mungu ananitumia sana katika eneo la kufungua waliofungwa ”. Nami nilikuwa kimya namsikiliza kwa makini sana,nione atakapoishia habari hizo;
Alipomaliza kunisimulia yote anayoyafanya,Nikasema `` Waaooh hongera sana mama’ngu,Mungu ni mwema ‘‘ Baadae naye akatamani kusikia kutoka kwangu,akitegemea labda na mimi nitasema namna Mungu anavyonitumia kwa viwango vya juu kama alivyeeleza yeye. Lakini haikuwa hivyo kwangu maana mimi sina la kujisifia hata moja.!! Akaniuliza kama mimi pia ni mtumishi,nikamjibu “ndio mimi ni mtumishi wa kawaida tu”
Ndipo aliponiuliza “ unaabudu kanisa gani,upo kwa mchungaji gani na upoje pale,wewe ni mtenda kazi au ni nini unafanya hapo? ” kabla sijamjibu akaongeza na kusema “ unatakiwa uokoke ndugu yangu ”
Nikaona isiwe shida,nikamwambia “mimi pia ni mchungaji” aliposikia hivyo,akanikazia macho,akitaraji nimuoneshe picha za mahali ninapochunga kwa maana alitaka kulinganisha na kanisa lake kwa sababu katika maelezo yake alisifia sana kanisa lake pamoja na karama ya maombezi ya kufungua wale waliokuwa wamefungwa na nguvu za giza.
Kilichofuata!!! Nilipomuonesha picha mbili tatu hivi za kanisani kwetu,gafla nikamwona mtu kanywea kama paka aliyemwagiwa maji ya baridi!!!! Unajua majivuno hayana maana kabisa,tena usimwone mtu ukamdharau na kumpima kumbe huyo unayemdharau yupo juu yako sana kuliko unavyodhani.
Kwa ufupi huo mama mchungaji alikosa unyenyekevu,bali alikuwa akijiinua sasa amekutana na mtu ambaye alikuwa kimya akimcheki tu,ambaye yeye hamfikii hata kidogo mtu huyo. Tujifunze jamani,kujiinua hakuna maana!!!
ITAENDELEA.
Na Mch.Gasper Madumla.
Kwa msaada zaidi,tafadhali piga+255 683 877 900
What’s app +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments