top of page

KUTEMBEA NA MUNGU KATIKA UTII~02

Na Mch. Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi…

02. Kiburi cha uzima.

Kiburi ni mojawapo ya sababu kubwa inayowafanya wengi kushindwa kuishi maisha ya utii. Kiburi cha uzima ni hali ya kutomuhitaji Mungu kwa sababu una utele fulani hivi, kwamba wewe ni mzima, mambo yako unaona yanaenda vizuri hivi, sasa unajikuta ukishindwa kufanya mapenzi ya Mungu. 

Mtu mwenye kiburi cha uzima, kamwe hawezi kutembea na Mungu wake katika utii. Kwa sababu anajiuliza maswali mengi, kama vile “kuna haja gani ya kuomba wakati nina kila kitu ndani?” Mfano ; mchungaji wake akimwambia afunge na kuomba,utakuta hawezi kwa sababu ya kiburi cha uzima alichonacho. Sijui kama unanielewa? 

Si watu wote wenye mali hawana utii,wala si watu wote walio na afya njema wamekosa utii,bali wengi wa wenye mali hawana utii wa neno la Mungu ipasavyo na ndio maana hata Yesu alisema kwamba ni shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni ( Mathayo 19:23). Na si tajiri tu bali wengi wetu wenye afya nzuri tunasumbuliwa na kiburi cha uzima,kwa hiyo maagizo ya Bwana hatuyatilii mkazo kwa sababu tu wazima leo, lakini tumesahau kwamba ikiwa leo tu wazima kesho tunaweza kuwa wagonjwa.!

Wewe je,upoje katika eneo hili? Je ni kweli inajitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu au unaacha kwa sababu upo na uzima sasa. Ni mara ngapi unakaidi sauti ya Mungu kwa kinywa cha mchungaji wako pale akuambiapo neno la Mungu? Kisha usifanye sawasawa na badala yake ukafanya mambo yako? 

Nimeona wengi wakitembea nje ya utii wa sauti ya Mungu kwa kinywa cha wachungaji wao. Wengine husema sina muda sasa kufanya hivyo mchungaji atakavyo,lakini papo hapo ana muda wa kufanya mambo yake tena wakati mwingine hayo mambo yake ni mambo machafu!!! Ikiwa ni hivi basi mtu wa namna hii amekosa utii wa kawaida kabisa. Na kundi la namna hii lipo kubwa sana makanisani mwetu, lakini ni kwa sababu ya kuwa na kiburi cha uzima.

Biblia inakutaka usije ukamsahau Bwana Mungu wako pindi utakapofanikiwa kwa namna yoyote ile ( Kumbukumbu 8:11-17). Ukiwa katika afya uliyonayo hapo ndipo ujitoe zaidi kwa Bwana Mungu katika kuhakikisha unafanya yote akuagizayo Bwana Mungu wako. 

Kumbuka Mungu huwapinga wenye kiburi (1 Petro 5:5). Hii ikiwa na maana wenye kiburi wamekosa nafasi kwa Mungu wamekataliwa. Kwa sababu kiburi chochote kile ni tabia ya shetani. Ibilisi hali akijua kwamba ili ushindwe kuwa pamoja na Mungu basi amepanda kiburi kama roho ndani yako kwa kusudi wewe umekosea Mungu ushindwe kuwa mtii.

Kiburi cha uzima ni hatari sana;

Siku moja nilikuwa nikiongea na mmoja wa mtoto wangu wa kiroho aliyekuwa akiishi nje ya nchi. Ulikuwa akiishi ulaya huko katikati ya wazungu ingawa yeye ni mtanzania mwenzangu. Sasa ananiambia kwamba mahali alipo hakuna kabisa mambo ya ibada za kiroho kama hizi tuzifanyazo huku kwetu Tanzania maana yeye alikuwa ameokoka. Alitegemea kuwakuta wazungu wa mahali pale alipo kwamba ni watu ambao watakuwa na hofu na Mungu,wakiwa ni wapendwa waliookoka; lakini hakukuta hivyo 

Bali alikuta kila mzungu ana maisha yake kivyake vyake wala hakuna mambo ya ibada za kiroho. Kwa maana hao watu waliomzunguka hawakuona sababu ya kuomba omba kwa Mungu maana wana kila kitu ndani. Wana magari,pesa.! Hivyo hata wengine hawaamini wokovu. Ndio, wanaamini kuwa Mungu yupo lakini so what ! Kama yupo. 

Hivyo hana haja hata ya kwenda kanisani. Ananiambia kwamba wale wenye kuenda kanisani ni wazee fulani hivi tena ni wachache tu tena hakuna kanisa la kiroho bali yapo tu kanisa la kawaida kabisa wanafanya ibada kifamilia hivi kisha wanaondoka zao. 

Sasa,kinachowasumbua hawa watu ni kiburi cha uzima kama moja ya sababu ya kuwafanya watu hao wasifanye mapenzi ya Mungu kwa dhati maana wanajiona wamekamilika. Lakini mimi nataka nikuambie,hatutembei kwenye utii kwa sababu tunahitaji kuwa na majumba au magari au mali fulani! Bali tunayafanya mapenzi ya Mungu kwa sababu ya kukamilishwa katika wokovu wetu maana utii ni njia ya wokovu kamili.

Mpendwa,ebu jichunguze uone kana kwamba una tabia hii ya kiburi cha uzima kwa sababu ya afya,mali,ulizonazo. Kumbuka kwamba afya,pesa,mali zote ni za Bwana Mungu. Yeye Mungu amekuaminisha tu,wala si za kwako maana akitaka kuzichukua anaweza kuzichukua saa yoyote ile na hakuna mahali pale kushtaki!

Ile namna ya kuwa na kiburi ni pandikizi la shetani ndani yako. Ile namna ya kujiona wewe ni bora zaidi ya wengine kunakufanya usimfuate Mungu ipasavyo. Kwa nini unapuuzia sauti ya Mungu? Mfano; umehubiriwa vya kutosha kuhusu wokovu lakini unakataa na kuona kwamba kuokoka ni mambo ya hao wasio na kazi maalumu,au unaona masuala ya Mungu ni ya watu maskini hivi! Wewe kwamba huna muda huo wa kukaa na watu wasio na elimu,watu wachovu wachovu hivi! Ukiwa na mawazo ya namna hiyo basi ni kiburi cha uzima ndicho kinachokusumbua

Lengo kuu la ujumbe huu ni kukufanya sasa ushuke na unyenyekee kwa Bwana ukihakikisha unayafanya mapenzi ya Mungu kwa bidii na huko ndiko kutembea na Mungu katika utii ninakokuzungumzia.

Kilichowafanya akina Adamu kuanguka ni wazo la kiburi kutoka kwa ibilisi nyoka aliwaambia  “mkila matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, mtafumbuliwa macho na kuwa kama Mungu”  akina Adamu  wakatamani kuwa kama Mungu hali wao ni wanadamu ikiwa wanafanana sana na Mungu. Kule kutaka kuwa kama Mungu alivyo ni kiburi ndani yao. 

Sasa,ikiwa unahisi hali fulani ya kushindwa kutembea katika njia ya utii kwa sababu kuna hali fulani ya kiburi,(au hali yoyote ile) basi nipigie simu yangu hizi;

ITAENDELEA….

Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900

Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page