KUTEMBEA NA MUNGU KATIKA UTII~01
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 17, 2017
- 6 min read

Na Mch. Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Katika mwezi wa tatu baada ya wana wa Israel kutoka utumwani Misri,siku hiyo hiyo wakafika kwenye jangwa la Sinai. Nao wakapiga kambi huko wakiukabili mlima Sinai,Musa akapanda juu ya mlima kuzungumza na Mungu maana Mungu alishuka juu ya mlima huo.
Jambo la kwanza ambalo Mungu anasema na Musa ni jambo la utii wao,kama moja ya nguzo kubwa ya kufanikiwa kwao. Anasema;
“Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,” Kutoka 19:5
Bwana Mungu anawaambia kwamba ikiwa wataitii sauti yake,basi watakuwa wa thamani mbele zake,watakuwa bora kuliko watu wengine wote. Kumbe wana wa Israel hawakuhitaji mambo mengi ili wafanikiwe bali walihitaji kutembea na Mungu katika utii tu,kisha Mungu Yeye mwenyewe atawapigania.
Musa akawaambia israel wote,kisha akapanda tena huko juu ya mlima ili apokee maagizo na sheria kutoka kwa Mungu. Siku zikapita yapata muda wa siku arobaini hivi,Musa akiwa juu ya mlima. Wale waliopo chini wakasema Musa amekufa mlimani,wengine wakasema hatujui lililompata huyo Musa.
Wakamwambia Haruni awatengenezee ndama ya dhahabu naye Haruni akafanya hivyo ( Kutoka 32:1-6). Nao wakaanza kuisujudia na hapo hasira ya Mungu ikawaka juu yao. Kumbuka,ni watu wale wale ambao waliambiwa watii wawe bora kuliko watu wengine duniani. Lakni sasa wamepotoka,wamerudi nyuma.
Kurudi nyuma kwao kulileta maangamizo makubwa,kwa maana yapata watu elfu tatu wakafa.Biblia haituambii kwamba watu hao walipata maangamizo hayo kwa sababu walilogwa.! Bali uchawi wao ulikuwa ni “kushindwa kuitii sauti ya Mungu” Na hili ndilo tatizo la wengi siku ya leo.
Leo hatuishi tena chini ya sheria,bali Mungu ameziandika sheria zake kwenye vibao vya mioyo yetu ( Yeremia 31:31-34). Lakini bado tunaona hata sasa tunapitia kwenye maangamizo makubwa kwa sababu ya kuishi kinyume na sauti ya Mungu. Wengi wetu leo hatujalogwa lakini tupo katika mateso makali kwa sababu ya kushindwa kutembea na Mungu katika utii.
Si mpango wa Mungu kwetu,tuangamizwe na mateso makali. Bali Mungu anatutaka tufanikiwe zaidi ya hapa. Vile ulivyo sasa bado,Bwana Mungu anataka ukafanikiwe sana,lakini pale utakapoweza kuishi naye kwenye utii wa sauti yake. Biblia inasema;
“ lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.” Yeremia7:23. Soma pia Isaya 1:19
Sasa,ikiwa umekwama katika eneo lolote lile,kabla ya kuomba kwa kupambana na shetani,kwanza jiangalie umekaaje na Mungu katika utii? Je wewe ni mtii wa sauti yake? Mimi nataka nikuambie,hujakaa vizuri na ndio maana unapitia hayo yote.
Utii ni tabia ya Yesu;
“ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” Wafilipi 2:6-8
Katika kitabu cha Waebrania 5:8-10 inatuambia kwamba “ ingawa ni mwana alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata” Huyo ni Yesu,Yeye aliyejifunza kutii tena kwa mateso makubwa. Ikiwa Yeye alishuka hata akaitii sauti ya Mungu wewe ni nani leo ukatae/ushindwe kutii sauti ya Mungu????
Yesu alitii hata mauti ya msalaba kwa ajili yako wewe na mimi. Bwana akamwidhimisha baada ya utii huo. Hata wewe ukihitaji kupanda kiroho huna budi kushuka kwa kujifunza kunyenyekea na kutii kama alivyofanya Yesu. Huwezi kuwa mtumishi mzuri wa Mungu ikiwa huna utii wa kushuka na kukubali kufanya yote unayoagizwa kufanya.
Ni Yesu ndiye aliyekubali kushuka sana ili auokoe ulimwengu,Ni Yesu alibeba jukumu lote la ukombozi maana alikuwa mtii. Ukitaka kutembea na Mungu kikamilifu katika imani yako,huna budi kuwa mtii katika mambo yote yamuhusuyo Mungu. Utagundua kwamba Mungu alifanya kazi na wala tu waliokuwa ni watii kwake, hata wewe unaweza kufanya kazi pamoja na Mungu sasa lakini endapo utakuwa ni mtii kwa mambo yote yamuhusuyo Mungu.
Tafsiri nyepesi ya utii ni hali ya kusikia kwa umakini na kutenda yote kama ulivyoagizwa. Bwana Yesu yote aliyoyasema katika kufundisha na kuhubiri alisikia kwa Baba,naye hakufanya jambo lolote asilolifanya Baba ( Yohana 5:19,30). Mtu mtii ni yule ambaye aweza kusikia kwa umakini na kutenda sawasawa na alichoagizwa/alichosikia.
Hakuna mahali popote katika biblia palikoelezwa kwamba Yesu alijitendea mambo yake mwenyewe,bali Yeye aliyafanya yote sawasawa na yote aliyoambiwa kufanya. Hivyo basi utii ni zaidi ya kusikia bali ni kutenda pia. Wengi leo husikia sana hali si watendaji wa neno,watu wote wa namna hii sio “watiifu“. Bwana Yesu amekuja kutuonesha namna ambavyo tunavyostahili kuishi. Huna mwingine wa kujifunza kwake isipokuwa ni Yesu tu ( Mathayo 11:28-29)
Hivyo basi kutembea na Mungu ni kitendo cha kuyafanya mapenzi ya Mungu sawa sawa na yote akuagizayo. Utii wa sauti ya Mungu ni vile kufanya mapenzi ya Mungu yote. Si rahisi kuwa mtiifu bila msaada wa Roho mtakatifu kwanza,kwa maana ni yeye atakayekuwezesha kusikia na kutenda yote kama ulivyoagizwa. Unamuhitaji Roho mtakatifu kwa kiwango cha juu sana.
Siku zote,wale watiifu walikuwa ni rafiki wa karibu wa Mungu. Mtazame Ibrahim mtu aliyekuwa mtii hata Mungu akamwita rafiki.Mungu alimwambia amtoe Isaka mwanaye wa pekee awe dhabihu ya kuteketezwa ( Mwanzo 22:1-14) naye akawa mtii kwa hilo japo kwa maumivu makubwa. Biblia inamuita Ibrahimu ni rafiki wa Mungu;
“Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.” Yakobo 2:23
Yupo pia Nuhu mtu aliyekuwa ni mtii maana Mungu aliweza kusema naye atengeneze safina katika kipindi cha gari ( wakati wa jua kali pasipo kuwa na mvua hata dalili ya mvua) naye anatengeneza vivyo hivyo kama alivyoagizwa,mtu huyu alikuwa na karama ya imani na alitembea na Mungu katika utii. Maana safina aliijenga muda wa miaka 100,si jambo dogo hilo kama huna utii wa sauti ya Mungu.
Mojawapo ya hila za shetani ni kukufanya kutokuwa mtii wa neno la Mungu. Kwa maana anajua siku utakapokuwa mtii,basi utampinga na utakuwa adui yake mkubwa. Maana shetani hana shida na wale wasiotii neno,hao wapo upande wake, isipokuwa kwa watii tu. Hii ni kweli,maana hata wewe ukiwa na mtu aliye upande wako huwezi kuwa na shida naye.
Utii huja kwa pendo“… mtu akinipenda,atalishika neno langu…” Yohana 14:23 ; Kwa lugha nyepesi ni sawa na kusema yoyote asiye mtii ni yule aliyempenda Bwana. Hii ni kweli; hata wewe ikiwa utampenda mtu wa kawaida kabisa basi ni lazima utalishika neno lake na kufanya kama atakavyo mtu huyo. Mimi huwa ninasema siku zote kwamba “ ukimpenda Mungu lazima utakuwa na utii wa neno lake bila shuruti“
Lakini sasa kwa nini wewe si mtii kama kama alivyokusudia Mungu?
Awali ya yote kurudi nyuma na kuwaangalia Adam na Hawa watu wa kwanza kabisa ambao nao walikosa kutii sauti ya Mungu. Kulikuwa na sababu zilizowafanya kutotii;na sababu hizo hizo ndizo zinazokufanya wewe pia ushindwe kutii,nazo ni;
01.Hila za shetani
Hila ni njama mbaya au ni mpango mbaya unaopangwa kwa lengo la kukuangusha. Mara nyingi njama za namna hii huwa ni za uongo uongo.Mwenyekiti wa kamati za mipango ya hila ni shetani, yeye ni mwenye hila tokea zamani maana ndiye baba wa uongo ( Yohana 8:44). Kulikuwa na hila ya kuwaangusha akina Adam na Hawa pale bustanini;maana nyoka alimdanganya mwanamke hata akadanganyika mwanaume naye akajikuta amenaswa dhambini.
Bwana Mungu alisema “…siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” shetani anasema “ hakika hamtakufa” umeona hapo jinsi ambavyo ibilisi alivyogeuza maelezo kwa kusudi la kumfanya mtu asitii sauti ya Mungu. Hivi unajua kwamba Adamu na mkewe hawakupanga kutokutii? Bali kwa sababu ya hila za yule mwovu ziliwafanya washindwe kutii,wakaasi. Sababu hii ndiyo ifanyayo kazi hata kwako,kwa maana jiulize ni mara ngapi unashindwa kutii neno la Bwana kwa sababu ya hila zilizokunasa?
Nyoka ni roho ya udanganyifu yenye lengo la kukufanya usitii ulivyoagizwa na Mungu. Ebu angalia,ni mara ngapi unashindwa kutii hata maagizo ya mchungaji wako kwa maana umesikia madanganyifu mengi juu yake? Ibilisi hutumia mbinu hii kwako. Unaweza ukaambiwa ulipe fungu la kumi, lakini papo hapo ibilisi akakuinulia mtu na kukuambia kinyume kwamba “ usilipe kwa sababu mchungaji anakula hiyo pesa yako,unaona hata anavyopendezaga siku hizi ni kwa ajili ya matoleo yako…” Ukiona mtu anakuambia hivyo ujue hiyo ni hila ya shetani. Chukua hatua mara moja ya kuipinga hila hiyo kwa gharama yoyote ile.
Yeye asiyetii ni yule ayafanyae matakwa yake binafsi wala sio ya Mungu. Muangalie Yona,mtu aliyetumwa na Mungu lakini alikaidi kutotii kisha na kuelekea alikokutaka yeye mwenyewe ( Yona 1:1-3). Ibilisi amejawa na hila nyingi,na kila hila aifanyayo kwako ni kukutoa kwenye kusudi la Mungu kwa kutokutii. Maana utii ndio njia kuu ya kuelekea kwenye kusudi lako. Adamu walipoteza kusudi zima kwa sababu tu na kuasi kulikokuja baada ya kushindwa kutii. Hata wewe waweza kupoteza au kuishi nje ya kusudi la Mungu kwa sababu ya kutokuwa mtii. Leo ibilisi amekuja kidigitali zaidi ili kusudi usiwe mtii tu.
Laiti kama Adamu na Hawa wangeligundua hila ya ibilisi,basi ni dhahiri wasingelidanganywa. Mimi sijui kwako kuna kitu gani hata unashindwa kuishi katika utii. Lakini nataka nikuambie kwamba lazima kutakuwa na hila za yule mwovu tu. ibilisi aliwadanganya,maana hata anamwambia Hawa,ukila matunda mtafumbuliwa macho nanyi mtakuwa kama Mungu mkijua mema na mabaya ( Mwanzo 3:5). Ibilisi hakujua akina Adamu waliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu ikiwa na maana wanafanana tayari Mungu wao. Yaani jinsi alivyo Mungu ndivyo walivyo wao. Sasa kufanana kwingine anakokuleta shetani ni kipi huko kama si uongo uliojaa hila ndani yake?!!!!
Kwa msaada zaidi waweza kunipigia simu au kunicheki kwenye whastaap yangu kwa mawasiliano yafuatayo;
ITAENDELEA….
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE..
Comentarios