top of page

KUOKOKA KUNA MAANA GANI HASA?

Updated: Sep 5, 2022

Na Mch Gasper Madumla.



Kulikuwa na vijana watatu ambao waliokuwa wana desturi ya kwenda kuogelea kwenye bahari kwenye misimu ya sikukuu. Siku moja kwenye sikukuu,wenyewe wakiwa “wameulamba” tayari kwa mtoto wao kwenda bichi kuogelea. Wakiwa tayari wote watatu wamebadili nguo zao kisha wakawa “ wakipiga mbizi“,’mara wote watatu wakapelekwa mbali na mawimbi makali siku hiyo. Wakiwa katika hali ya kuhitaji msaada,mara wawili wao wakafanikiwa kutoka katika yale maji,lakini walichoka sana!


Wakawa wakimuangalia mwenzao mmoja lakini hawakumuaona kwa wakati ule sababu amepelekwa mbali na mawimbi makali. Basi wakarudi hadi nchi kavu wakimsononekea mwenzao maana wamempoteza majini. Kumbe yule mwenzao akawa akitapa tapa.kwenye maji huku akiita “ naomba msaada,niokoe… ninakufa” lakini maskini! Hakuna aliyesikia kabisa. Alikazana kuita kwa sauti kubwa! Mara wavuvi wawili waliokuwa wakiandaa nyavu zao,wakasikia sauti hiyo. Wakaja kasi na mtumbwi wao mdogo.


Wakamuona yule mtoto,kisha wakamtoa kwenye maji ambayo kwa kweli yalimzidi nguvu. Wakamtoa mpaka ufuoni akiwa mzima lakini amechoka fulani hivi!. Hivyo mtoto huyo “ aliokoka na kifo“. Mtoto huyu hakuwa na uwezo wa’“ kujiokoa” bali aliokolewa; kifo kilimuachia. Nataka uone hapo nini maana hasa ya kuokoka kupitia mfano huo. Mtoto huyo alitolewa kwenye wigo la mawimbi na hatimaye kuletwa nchi kavu mahali salama.


Hivyo kuokoka maana yake ni kutolewa ,kuhamishwa kutoka kwenye utawala wa giza na kuingizwa kwenye utawala nuru,kwenye ufalme wa Mwana wa pendo lake. Kama ilivyokuwa katika mfano wa huyo mtoto.aliyeokolewa,kwamba“ aliokolewa” sio kujiokoa ndivyo ilivyo katika kuokoka,hatujiokoi kwa sababu ya elimu yetu,hadhi yetu,au kwa sababu ya status ya wazazi wetu,hapana! Bali nasi “ tunaokolewa” na Mungu maana ni kipawa cha Mungu kwa njia ya imani ( Waefeso 2:8) 


Kuokoka sio dini mpya wala sio dini kwa sababu kuokoka ni mpango wa Mungu wa kumwokoa mwanadamu kwa njia ya imani ndani ya Yesu Kristo,Yeye Mungu aliyefanyika mwili na kuzaliwa chini ya sheria ali kusudi atuokoe sisi tuliokuwa chini ya sheria.

Kuokoka ni kuzaliwa upya kwa mara ya pili. ( Yoh.3:3). Kumbuka kilichozaliwa kwa mwili ni mwili na kilichozaliwa kwa roho ni roho.


Ikiwa ulizaliwa na baba na mama yako,huna budi kuzaliwa upya kwa roho; hivyo basi;Neno “kuokoka” maana yake ni kufanyika kiumbe kipya ndani ya Yesu Kristo. Kumbuka,Yeyote amwaminie Yesu na kumpokea,Yesu huanza makao mapya ndani ya mtu huyo. Utagundua kwamba kuokoka ni maisha halisi kwa sababu Yesu naye yupo hai,halisi akiishi ndani yetu.

Watu wengi leo wamefungwa na shetani kwamba wasiokoke yaani wawe nje ya mpango wa Mungu kwa sababu mpango wa Mungu ni kuwaokoa watu wote kupitia Yesu Kristo ( 1 Timotheo 2:3-4).


Ni lazima ifike wakati ufanye maamuzi ya kumpokea Yesu Kristo kwa sababu tupo kwenye nyakati za mwisho. Wengi wanaopuuzia wokovu,kuna siku moja ambayo watayakumbuka maneno haya yote.

Nilipokuwa kwenye dini yangu kabla sijaokoka nilijiona kuwa niko sahihi sana kwa sababu nilikuwa mtu mwenye bidii na dini yangu,sikudhani kwamba kuna maisha mapya ndani ya Yesu Kristo. Lakini nilipookoka ndipo nilitambua kwamba Yupo Yesu halisi kiishi hata sasa. Mambo ya wokovu wakati mwingine hayaelezeki kabisa,sababu ni ya kiroho sana. Maisha ya wokovu ni mchakato mrefu wa kutunza utakatifu,maana pasipo huo hakuna awezaye kumuona Mungu – ( Waebrania 12:14)


Wakati mwingine kuokoka nakufananisha na“ kupata tiketi” ya kusafiria. Ebu chukulia hili,ikiwa unahitaji kusafiri ni lazima uwe na tiketi halali,lakini ikiwa huna basi ujue huwezi kusafiri na utabaki! Lakini mwenye tiketi anapaswa kuitunza tiketi yake isipotee,isiliwe na panya,isichanwe chanwe,au isichafuliwe chafuliwe n.k hata akiitunza vizuri na siku ya kusafiri itafika na itamuwezesha kufika aendako.


Lakini ikiwa msafiri akaichafua chafua,akaichana chana tiketi yake,ujue atazuiliwa asisafili au atakuwa na kwazo.

Hivyo ndivyo ilivyo hata katika wokovu,unapookoka ni kama vile umepewa tiketi ya kuingia kwenye ufalme wa Mungu,lakini kuokoka kwako hakukupi garantee kwamba utaingia mbinguni ikiwa hutajitunza kwa Bwana. Kumbe kuokoka kunakupa nafasi ya kuingia mbinguni,lakini nafasi hiyo inatunzwa katika “ utakatifu“.Kuokoka kuna maana pana kwa sababu ni zaidi ya hayo. Na ndio maana hata kama ningeeleza nisingelimaliza. Lakini nataka ujue kwamba nini maana ya kuokoka. 


Ulimkubali Yesu kwa kinywa chako kwamba Mungu alimfufua katika wafu,na ni Bwana na mwokozi wa maisha yako;huku moyoni mwako ukiamini (kwamba Mungu alimfufua katika wafu) Utaokoka. ( Warumi 10:9). Furaha kubwa ndani ya mwanadamu ni kumpokea Yesu Kristo yaani kuokoka tu. Wala hakuna furaha nyingine iliyokuwa kubwa.Kumbuka;watu wote tulihesabiwa adhabu na ghadhabu ya kali ya Mungu juu ya dhambi maana mshahara wa dhambi ni mauti( Warumi 6:24). 


Lakini kwa neema ya Bwana ametuhurumia hata akatengeneza mpango wa wokovu,na akamtuma Yesu Kristo afanyike ukombozi wetu. Unajua ukiwa tayari unasubiria kupata adhabu juu ya makosa yako,alafu papo hapo chukulia akaja mtu kwako ambaye amekubali kubeba mateso yako yote ili wewe uwe huru ndani yake. Lakini ikiwa utamkataa huyo mtu,basi ujue umekwisha hukumiwa na hauna udhuru katika hilo ( Yohana 3:18).“Kuokoka ” ~ ni neema ya Bwana juu ya watu wote waepukane na moto wa milele baada ya maisha haya. Ikiwa ni neema ya Bwana,basi huna sababu ya kukataa neema hiyo iliyokuja kwako bure! 


Unapookoka umezaliwa upya,na ikiwa umezaliwa upya basi u mtoto mchanga kiroho. Mtoto anakadiriwa akue na kuongezeka! Kama ilivyo kwamba ili mtoto aweze kukua anahitaji chakula halisi cha mama yake yaani“maziwa yasiyoghoshiwa ”  katika wokovu Neno ndio chakula halisi cha roho yako.


Hivyo fanya maamuzi leo kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.,waweza kunipigia nikuongoze sala ya toba sasa;


Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446


Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page