KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU.
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 3, 2015
- 4 min read

Mchungaji Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Imeandikwa;
“ Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. ” Mathayo 12:32
Kupitia neno la Mungu lilo hapo juu,tunaona kumbe zipo dhambi ambazo twaweza kusamehewa,lakini pia iko dhambi moja ambayo kwa hiyo haiwezekani kusamehewa,dhambi hiyo ni kumkufuru Roho mtakatifu ndivyo tusomavyo katika biblia. Mungu atusaidie sana tusifikie kuitenda dhambi hiyo ya kufuru.
Kumbuka jambo hili; katika Yeye Yesu ilipendeza ukamilifu wote ukae (Wakolosai 1:19 ) hii ikiwa ina maana kwamba ndani ya Yesu Kristo,yupo Roho mtakatifu,pia yupo Mungu Baba,maana Yeye ni Mungu aliyefanyika mwili akazaliwa chini ya sheria kwa ajili ya kutukomboa sisi tuliokuwa chini ya sheria ya dhambi na mauti (Yoh.1:14).
Katika andiko letu hapo juu Mathayo 12:32a,~ Yesu anasema “ Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa,…” ikiwa na maana kwamba yeyote atakaye nena neno kwake juu ya mwili aliouvaa,(ingawa alikuwa ni Mungu),mwili mfano wa mwanadamu ya kwamba mtu huyo atasamehewa.
Ndio maana akatumia neno “Mwana wa adamu” ili kutofautisha kati ya dhambi yenye uwezo wa kusamehewa na ile isiyoweza kusamehewa. Neno “Mwana wa Adamu” linawakilisha Yesu kufanyika mwili. Waweza kuona kwamba wale wote waliomdhiaki Bwana Yesu katika mwili waliweza kusamehewa ikiwa kama walirejea kwa toba.
Lakini tazama hata Wayahudi walipokuwa wakimtukana na kuutesa mwili wake alipokuwa akiuendea msalaba akawaambia “Baba,uwasamehe,kwa kuwa hawajui watendalo.” Luka 23:34
Ikiwa na maana kwamba watu wale wote wenye kuutesa mwili wa Mwana wa adamu wanaweza kusamehewa ndio maana Yesu Kristo alipowatazama akawahurumia akawaombea msamaha.
Lakini kwa habari ya kumkufuru Roho mtakatifu ndipo hakuna msamaha.Hivyo basi kabla ya mambo yote yakupasa kujua nini maana ya neno kukufuru.
Kukufuru ni;kutukana,kudhihaki,kufedhehesha,kunenea mabaya katika wema uliokuwepo kana kwamba haupo.N.K
Hivyo basi;
▪ Kumkufuru Roho mtakatifu ni kuzitukana kazi za Roho mtakatifu zilizokuwepo awali ndani ya huyo mwenye kukufuru hali akijua alitendalo. Tena,~ kumkufuru Roho mtakatifu ni kuzikataa,kuzifedhehesha,kukejeri kwa dhihaka kazi zote za Roho mtakatifu zilizokuwepo ndani ya mwamini aliyekuwa mwenye kujawa nazo lakini akaanguka kwa kuzitukana kazi zote za Roho mtakatifu hali akijua alitendalo.
“ Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri. ” Waebrania 6:4-6
Kumbuka ya kwamba watu wa namna hii ni wale ambao walikuwa na ushirika mkubwa sana na MUNGU. Kazi zote za Roho mtakatifu zilikuwa zimedhihirishwa ndani yao,wenye kuisikia radha ya kipawa cha mbinguni,wenye kuwasiliana na Mungu kupitia Roho mtakatifu. Alafu wakaanguka haiwezekani wakafanywa upya hata wakatubu.
Tafsiri sahihi ya neno “kuanguka” ni kuiacha imani ya kweli na kurudia dhambi kwa kujua kwamba ni dhambi.Lakini neno hili “kuanguka” lina maana pana sababu mtu yeyote akiwa amefanya dhambi yoyote ile hapo tunasema “ameanguka dhambini”. Lakini neno hili “ Kuanguka ” kama lilivyotumika katika Waebrania 6:4-6 lina maana ya kuanguka katika dhambi ya kukufuru Roho mtakatifu tu na wala halina maana ya kuanguka katika dhambi za kawaida ambazo zina msamaha baada ya kutubiwa.
Hivyo basi utagundua ya kwamba akipatikana mtu wa namna hii ambaye hapo awali alikuwa akizijua siri za ufalme wa Mungu,yeye ambaye kazi za Roho mtakatifu zipo ndani yake,yeye ambaye mwenye kujua kweli,tena ameonja kipawa cha mbinguni.N.K mtu huyo akianguka katika dhambi ya kukufuru kazi hizo zote za Roho mtakatifu,hapo sasa Roho wa BWANA humkimbia mtu huyo,na hatimaye hata akitubu katika hali hiyo hawezi kupokea msamaha sababu hakuna tena Roho wa BWANA wa msamaha.
Labda tuangalie biblia inasemaje zaidi kwa habari ya kumkufuru Roho mtakatifu;
“ Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia.
Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; ” Warumi 1:18-20, & Waebrania 10:26-27
Biblia inatuambia watu ambao wamekwisha wekewa ghadhabu ya Mungu tayari kwa sababu watu hao wanaifahamu kweli yote ya kazi ya Mungu kwa msaada wa Roho mtakatifu,lakini wakiipinga kweli kwa uovu.
Watu wa namna hii,biblia inasema Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa,wafanye yasiyowapasa. Kwa lugha nyingine ni kwamba watu wa namna hii huwezi kuwafanya upya hata wakatubu,maana wamemkataa MUNGU wa kweli kabisaa hali hapo mwanzo kazi ya Mungu ilidhihilika ndani yao.
▪ Mtu aweza kumkufuru Roho mtakatifu pale anapoanza kwa kumuhuzunisha Roho mtakatifu kwa dhambi tena dhambi zile azifanyazo kwa siri sana Mfano,mtumishi wa Mungu aliyejaa nguvu za Mungu kweli kweli,mtu safi rohoni lakini utakuta alipojisahau kidogo akanguka dhambini~dhambi ikamnogea na hapo sasa akawa anaifanya kwa siri sana.
Mtumishi huyu hufanya dhambi chini kwa chini hali akiendelea kuhudumu,hapo sasa ameanza kumuhuzunisha Roho mtakatifu. Gafla Roho huondoka na karama zake,hali ya mtumishi huyo nayo hubadilika na kuwa mbaya kiroho maana hakuna Roho wa BWANA tena~na hapo hujikuta akianza kupotosha kweli ya Mungu kwa uovu ulio ndani yake na kuzitukana kazi za Roho mtakatifu yaani akikufuru kabisa ~hapo sasa ndipo pabaya,maana amekufuru.
Kwa huduma ya maombezi waweza kunipigia sasa,
nipigie +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments