KULIISHI NENO.
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 24, 2018
- 6 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi. ( Somo la Jumapili ya tar.22 Aprili 2018 kutoka kwa Mch. G. Madumla kwenye madhabahu ya BBFC)
Kuna utofauti uliopo kati ya kuwa na “kiu ya neno” na “kuliishi neno” kwa sababu yeye mwenye kiu ya neno ni yule ambaye ndani yake anatamani neno la Kristo lijae kwa wingi ( Wakolosai 3:16). Lakini yule ambaye mwenye kuliishi neno ni yule anayeliweka neno kwenye matendo baada ya kuwa na kiu ya neno. Na ndio maana biblia inatuambia;
“Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote;mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.” 2 Wakorintho 3:2-3
Hii ikiwa na maana kwamba maisha yako yote yanajulikana na kusomwa na watu wote hata kama utatenda jambo lolote kwa siri,ujue itafika wakati watu watajua na kuyasoma maisha yako. Ikiwa umeitwa “barua ya Kristo” basi huna budi kujua kazi ya barua ni nini haswa. Bila shaka kazi kubwa ya barua ni “kubeba ujumbe “kisha “kusomwa” ukiwa kama barua ya Kristo basi ni dhahiri watu wanapaswa kusoma habari za Yesu kwako,ndio maana biblia inaeleza kuwa watu waitafute sheria (neno)kinywani mwako ( Malaki 2:7). Maisha yako ni lazima yawe halisi kama neno lisemwavyo,na huko ndiko kuwa barua ya Kristo.
Hivyo “kuliishi neno” ni kitendo cha kulichukua neno kama lilivyo na kuliweka kwenye matendo. Vile neno lilivyo bila kuongeza wala kupunguza ndivyo maisha yako ya wokovu yanapaswa kuwa. Kwa lugha nyepesi “kuliishi neno” ni kumuishia Kristo,kumuishia Mungu,na kufanyika barua ya Kristo. Hiyo ndio maana halisi ya kuliishi neno. Ikiwa neno linasema,omba bila kukoma basi huna budi kuomba bila kukoma! Ikiwa neno linasema, ikimbieni zinaa basi ujue huna budi kuikimbia zinaa ( sio kuikimbilia,bali kuikimbia),!! Ikiwa neno linasema, usiifuatishe dunia na mambo yake,huna budi kuiacha dunia na mambo yake! N.k Lakini swali la kujiuliza;
Je ni kweli unafanya hivyo? Je ni kweli unaliishi neno? Je ni kweli unalipa gharama ya kuicha dunia na mambo yake ? Ikiwa la! Hufanyi hivyo na papo hapo unaifahamu kweli,lakini upo mbali nayo,basi ujue huna tofauti na“Farisayo” kitabia. Kwa sababu tabia kubwa ya Farisayo ni kuinena kweli pasipo kuiishi.l ( Mathayo 23:1-3) Ni pale ambapo mpendwa anayefahamu neno litakavyo lakini yeye mwenyewe haliishi hilo neno. Ebu jifunze kwa mfano huu alioutoa Bwana Yesu.
“ Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu.Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende.Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda.Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.” Mathayo 21:28-31
Mfano huo unazungumzia watu watoto wawili waliopewa waliopewa neno (kazi)ili kusudi walitendee kazi. Yule wa kwanza alikubali lakini hakulifanyia kazi,huyu anafanana na wewe uliyepewa neema ya wokovu. Umelisikia neno,na unajifunza kila siku lakini hulifanyii kazi!!! Yule mtoto wa pili alikataa hilo neno,lakini akatubu kisha akalifanyia kazi ni sawa na wale wote wenye dhambi wasiopata neema ya wokovu lakini wakatubu kisha wakafanyia kazi neno. Je ni yupi aliyefanya mapenzi ya Bwana? Bila shaka ni yule wa pili.!
Kumbe kuyafanya mapenzi ya Mungu ni kitendo cha kuliishi neno. Kinyume na hapo hakuna mapenzi ya Mungu. Mfano huu upo hata kwa familia yako,yule mtoto anayeshika neno lako na kujitahidi kuliishi katika utendaji kazi hakika huyo ndiye afanyaye mapenzi yako.
Watu wengi ni wasikilizaji wazuri wa neno na sio watendaji( maana msikilizaji ni tofauti na msikiaji,na hili ni somo jingine). Lakini biblia inakutaka usiwe msikilizaji bali “mtendaji wa neno” ,yaani uweze kuliishi neno ( Yakobo 1:22). Katika kitabu cha Warumi 2:13 neno lake hapo linapana ya kushangaza. Maana kumbe watakao hesabiwa haki kikamilifu ni wale tu watakao liishi neno. Haki hii ni zaidi ya haki ile ya kwanza baada ya kuokoka (maana ukiokoka unahesabiwa haki bure kwa njia ya imani)’. Uhusiano wako na Mungu unatengemea na kiwango chako cha kuliishi neno na si vinginevyo,na hiyo ndiyo maana halisi. Kumbuka;
Yule asikiaye neno na kulitendea kazi,amefananishwa na mtu mwenye “akili” bali yule asikiaye neno bila kulitendea kazi anafananishwa na “mpumbavu” ( Mathayo 7:24-27). Je wewe ni mwenye akili au mpumbavu? Tofauti ya watu hawa wawili ipo katika utendaji kazi kwa sababu ni kweli wote wamesikia neno! Kumbe hata sasa tunaweza kujua mwenye akili ni yupi na ni yupi mpumbavu!!! Ni heri uwe mwenye akili maana yajapo mafuriko kwenye maisha yako ujue hayatakuweza kwa sababu umejengwa juu ya mwamba Yesu. Ooh I feel preaching!!!😁😁😁
Sikia; “ thamani ya wokovu wako ipo katika kuliishi neno tu! Na hapo ndipo patakutofautisha na watu wa dini,watu wa imani nyingine,na watu wote” na inawezekana kuliishi neno! Kwa maana ukiliishi neno ipasavyo ni sawa na kuishi ndani ya Kristo na Kristo ndani yako,na hapo si wewe uishie bali Kristo ndani yako ( Wagalatia 2:20)
Lakini kwa nini watu wengi waliookoka wanashindwa kuliishi neno?
Wakati najiuliza hivyo,nikagundua kwanza ni kweli kabisa wengi hushindwa kuliishi neno. Na nikatafuta sababu zinazowafanya watu kuwa mbali na neno. Nikagundua sababu zifuatazo;
01. Hali ya kuizoelea dhambi na kuipenda dhambi kuliko kumpenda Mungu.
Hii ndio sababu kubwa kuliko sababu zote. Niwe wazi kwako na mbele za Mungu! Maana ukiwa umezoelea dhambi na kuipenda tena waitenda kwa siri,wala huna bidii kuiacha ujue kamwe huwezi kuliishi neno katika mazingira hayo. Na ndio maana unajikuta kwa sehemu umeishikilia dhambi na kwa sehemu upo kwa Bwana. Sasa hapo haiwezekani kuliishi neno ikiwa hujafanya maamuzi ya dhati kuacha dhambi hiyo!!!! Ebu angalia mwenyewe,ukiwa unanogewa na uchafu fulani,na papo hapo neno linakutaka uuache umuelekee Mungu,nawe hutaki,Je inawezekanaje kuliishi neno? Je thamani ya ukristo wako ipoje? Je unatofauti gani na yule asiyeokoka au yule kahaba,mwizi,n.k?
Ni mara ngapi unafundishwa njia sahihi za kumuishia Mungu,lakini mbona huziishi? Ni mara ngapi neno limesema nawe kwa habari ya kuacha hayo unayoyafanya lakini mbona hutaki? Ebu jifunze kwa mke wa Lutu aliyegeuka chumvi ya jiwe (Mwanzo 19:17-26). Ambaye yeye alipenda mazingira ya dhambi,Bwana alisema waondoke maeneo hayo yataangamizwa na wasigeuke nyuma wajiponye wenyewe lakini huyu mama aligeuka nyuma kama kwamba alitamani kurudi,nae akaangamia. Hivyo ukiipenda dhambi huku ukiwa unaijua kweli,ujue utaangamia tu.
02. Hali ya kuzoelea neno.
Ikifika wakati ukalizoelea neno kiasi kwamba unaona ni la kawaida tu,au kuona halikuhusu wewe hata ukafikiria ni neno la fulani na fulani lakini sio la kwako,ujue unatakuwa na shida sana!!! Na hapo huwezi kuliishi hilo neno. Wakati mwingine unaweza ukadhani unajua neno hilo,lakini sio kweli bado hujui!!! Kw maana hakuna duniani ajuae neno lote isipokuwa Roho mtakatifu anatufunulia kwa sehemu tu. Hata mimi bado sijui ni mwanafunzi wa Roho mtakatifu na nitabaki kuwa mwanafunzi siku zote za maisha yangu. Sasa wewe U nani? Hata kulidharau neno? Kumbuka,Mungu husema nasi mala moja,naam hata mara mbili japo hatujali kwa lengo la kututaka tuliishi neno lake ( Ayubu 33:14-15)
03. Kufungwa kwa nguvu za giza.
Yeyote aliyefungwa na nguvu za giza hawezi kiliishia neno kwa sababu shetani na mapepo yake hatamruhusu atende sawa sawa na Mungu atakavyo. Ukiona kutaka kutenda jema unataka lakini unajikuta ukitenda lililo ovu,tena ukiona unalolipenda hutenda bali usilolipenda ndilo ulitendalo basi ujue si wewe bali kuna nguvu inayokupelekesha usije ukatenda jema ukaokoka / ukahesabiwa haki. Hivyo ni lazima uchukue hatua mara moja ya kukimbilia kwa Bwana kwa mikono ya wachungaji watakao kufungua katika eneo hilo. Wala usione aibu maana sote tumetokea huko,tuliombewa na sasa tupo huru!
Nini cha kufanya zaidi ili uweze kuliishi neno?
Ingia kwenye toba ( ni vyema ukaongozwa na mchungaji atakayekupitisha kwenye maeneo halisi)
Jitahidi kumuomba Roho mtakatifu akusaidie kukupa nguvu ya kuliishi neno sababu bila Yeye Roho wa BWANA huwezi.
Fanyia mazoezi kila neno ambalo Mungu anasema nawe anza kuliweka kwenye matendo,kumbuka mazoezi ya mwili yanafaa lakini mazoezi ya roho yanafaa zaidi.
Faida kubwa sana ya kuliishi neno ni “kupokea baraka” Luka 11:28,Kutoka 19:5. Pia ukiliishi neno utakuwa na nguvu za ajabu sana za Mungu kwa sababu utakuwa upo ndani ya Yesu na Yesu ndani yako. Katika kuliishi neno ndipo mahali haswa pa kuishi maisha ya ushindi dhidi ya nguvu za giza na majaribu ya kila namna. Lakini ipo hasara kubwa kwa mtu aliye nje ya neno ni kudumaa kiroho na kuyumbishwa yumbishwa na upepo wa kila aina. Mungu akusaidie wewe unasoma neno hili,uweze kufikia hatua ya kuliishi.
Nataka niongee na wewe pamoja na niombe nawe ikiwa umesoma ujumbe huu muhimu sana kwako siku ya leo. Mimi ninajua kuna kusudi kubwa la Mungu kwako siku ya leo hata kuweza kusoma hapa. Basi waweza kunipigia kwa;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Kommentarer