top of page

KAZI YA NENO ~02

Na Mch. G.Madumla.


16. Neno linafanya kazi ya kueleza uhalisia wetu,kwamba tulitokea wapi na tutaishia wapi.

Ni kwa njia ya Neno la Mungu ndipo tunaweza kujua uhalisia wa kila kitu. Tunaweza kujua kwamba mwanadamu katokea wapi yaani chanzo chake kimetokea wapi hata mimi na wewe leo hii tupo hivi tulivyo. Na pia kwa njia ya Neno tunapata kujua kule tunapoelekea. Hivyo utagundua kwamba maarifa yote tunayapata katika Neno,na ikiwa ndivyo basi ni dhahili tunakubali kwamba tunalihitaji sana neno hili tuweze kujua nini haswa cha kufanya na nini cha kutokufanya ili mwisho wetu uwe mzuri.

Neno ni njia,kweli na uzima maana Yesu alisema Yeye ni njia,kweli na uzima.Hii ikiwa na maana kwamba Yesu ndiye Neno,na akiwa Yeye ni neno basi neno ni njia,kweli na uzima. Umeshawahi kufikiri hivyo? Ebu angalia Yoh.14:6 kisha linganisha na Yoh.1:1 na Yoh.1:14 (utaligundua hilo). Ukweli ni kwamba neno linatuongoza katika uzima wa kweli kwa maana lenyewe ni uzima.

Neno la Mungu linatuambia sisi ni akina nani,tulitokea wapi,tupo wapi sasa,na ni wapi tunapoelekea. Ukisoma maandiko matakatifu utagundua kwamba mwanadamu aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ( Mwanzo 1:26). Lakini mfanano ulipotea baada ya dhambi,na kusababisha wanadamu wote kupotea lakini kwa sababu Mungu alitupenda,akafanya mpango mkakati wa kutukomboa kwa njia ya mwana wake Yesu Kristo ambaye Yeye alilipa gharama yote ya ukombozi pale msalabani kwa kusudi moja tu,“kutukomboa sote,tutakao muamini na kumpokea Yeye,awe Bwana na mwokozi wa maisha yetu”

Habari hizi zote za ukombozi zimeandikwa katika biblia,neno likatueleza yote hayo. Tena na zaidi ya hayo tumejulishwa kwa maana ikiwa kama tutamkataa Yeye Yesu,naye atatubagua ( 2 Timotheo 2:12). Sasa,swali la kujiuliza ni kwamba “ Je bila neno la Mungu tungeyajuaje hayo yote?”

Mungu hajatuficha kitu chochote kwa maana ametuonesha na kutueleza sana kwamba ukitenda mabaya utaishia pabaya kwenye moto wa milele,na kama ukitenda mema utaurithi uzima wa milele katika maana ya maisha unayoishi hivi sasa ndiyo yataamua uelekee wapi!!! Nisemapo ukitenda mabaya nina maana ya kuishi nje ya wokovu na utakatifu wa kweli,na hapo utaishia kwenye moto wa milele bali ukiishi sawa sawa na mapenzi ya Mungu katika wokovu na utakatifu wa kweli utaishia kwenye uzima wa milele.

Hayo yote yamekwisha nenwa na kuandika katika biblia tuisomayo. Na ndio maana hakuna excuse/msamaha katika hilo,kwamba ukiwa umeelezwa usiishi hivi,nawe ukaishi hivyo basi ujue siku ya mwisho utahukumiwa jinsi ulivyoishi na kamwe hutakuwa na nafasi ya kutubu maana Neno linasema baada ya kifo ni hukumu ( Waebrania 9:27)

Jihoji mwenyewe sasa,Je hukuelezwa yote katika neno la Mungu? Je hukuelezwa mema na mabaya na jinsi ya kuyaepuka mabaya ili uyatende mema? Mungu wetu anatupenda “upeo” na ndio maana ametueleza mambo yote kwa kina katika neno lake kusudi tusiteketee.

Ukisoma Neno kwa umakini na kuongozwa na Roho mtakatifu utagundua mambo mengi sana. Mojawapo ya jambo utakalogundua ni hili “ Mungu anatueleza kwa namna ambayo anatamani asipotee hata mmoja,maana ametueleza hata mambo yaliyopita kwa mifano ili kutufundisha sisi tulio na maisha sasa”

“Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.” 1 Wakorintho 10:11

17. Neno linaleta ujasiri katika roho yako.

Je unajua kwamba hukuumbiwa roho ya woga? Je unajua ya kwamba hukuumbiwa hofu na mashaka? ( 2 Timotheo 1:7). Tafsiri nyepesi ya neno “ujasiri” ni nguvu ya Roho mtakatifu ya kujiamini katika kila jambo ulifanyalo katika Bwana. Mfano wa kazi za Bwana tulizonazo,zenye kuhitaji ujasiri wa roho ni;

  1. Kufundisha au kuhubiri neno.

  2. Kusifu na kuabudu

  3. Maombi ktk Roho.

  4. Kutoa unabii

  5. Upandaji wa makanisa pamoja na Uchungaji. N.K

Kumbuka ; Roho mtakatifu huachilia nguvu ya kujiamini ndani ya mtu mwenye kiwango cha juu cha neno. Waefeso 3:12

Biblia inasema katika Yeye tunao “ ujasiri” yaani katika Yesu (Neno) tunao ujasiri (Waefeso 3:12). Hii ni sawa na kusema ujasiri wa kiroho katika kutenda kazi ya Bwana unajengwa katika neno,au unapatikana katika neno. Na tunao ushahidi mwingi katika hili maana tunaposoma matendo ya mitume yote tunaona jinsi ambavyo mitume waliweza kumshuhudia Yesu kwa ujasiri mkubwa kwa sababu Roho mtakatifu aliwaongoza sawa sawa na kiwango cha neno ndani yao ( Matendo 28:31,4:13,18:26)

Bwana Mungu anamuagiza Yoshua awaongoze wana wa Israeli kwenda kwenye nchi ya ahadi akiwavukisha kwanza mto Yordani. Akimpa neno Yoshua kwamba “ awe hodari na moyo wa ushujaa ” ( Yoshua 1:6). Lakini anamueleza pia Yoshua siri ya kuwa hodari,shujaa,jasiri kwamba Neno la Mungu lisiondoke kinywanyi mwake ( Yoshua) bali alitafakari usiku na mchana ndipo atakapofanikiwa sana ( Yoshua 1:8).

Kumbe siri kubwa ya kuvikwa ujasiri katika roho yako,ni kulitafakari neno la Mungu usiku na mchana. Ni neno tu likupalo ujasiri katika kazi ya Bwana. Je wewe unafanya hivyo kulitafakari neno kila siku ili kusudu upate ujasiri katika kazi ya bwana uifanyayo?

Kwa msaada zaidi pamoja na maombi,piga +255 683 877 900

Mch. G. Madumla.

What’s app ni +255 746 446 446

UBARIKIWE

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page