KUKUA KIROHO.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 16, 2017
- 4 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi..
Kila kilichozaliwa kinatazamiwa kukua. Kwa sababu ni hali ya kawaida ya kukua kwa chochote kile chenye uhai ndani yake. Si hali ya kawaida kuona kilichozaliwa hakikui,na ikiwa kimekosa kukua ni lazima tutajiuliza, kulikoni?.
Nilipookoka nilitamani nikuwe mara moja maana roho yangu iliwaka! Lakini kumbe haikuwa rahisi hivyo,kwa sababu kuna mchakato fulani wa ukuaji lazima niupitie,kama vile unavyomwona mtoto mchanga aliyezaliwa sasa,ili akue kuna hatua lazima azipitie vyema,hivyo ukuaji si jambo la mara moja,bali ni la mchakato mrefu.
Sasa,nimegundua siri za ukuaji pamoja na maadui wanaozuia ama kukwamisha ukuaji. Wafuatao ni maadui wakubwa wanaopigana kukuzuia usikue,(ni baadi tu ya maadui wakubwa)
Maadui wa ukuaji kiroho;
01. Maisha nje ya Yesu.
Ukuaji wa kiroho unaanzia katika wokovu (Kumpokea Yesu,kuokoka). Kwa sababu ukiokoka unakuwa umezaliwa mara ya pili,si kwa mwili bali kwa Roho wa Bwana. Katika maisha ya wokovu,kuna ukuaji wa kumfahamu sana Mwana wa Mungu,hata kuwa mtu mkamilifu,hata kwenye cheo cha kimo cha ukamilifu wa Kristo (Waefeso 4:13).
Kumbe kuna kiwango cha ukuaji hata kufikia ukamilifu wa Kristo,Kiwango hiki kimewekwa kwako,ikiwa kama umekwisha mpokea Kristo Yesu,Yeye awezeshaye kukua kiroho. Wengi wamekwama hapa,katika ukuaji wao kwa maana wanampenda Mungu lakini bado hawajaokoka. Kumbuka ; kuokoka ndio chanzo cha kwanza cha ukuaji
02.Vifungo.
Ikiwa umeokoka lakini bado unaishi chini ya vifungo vya nguvu za giza,bila shaka ukuaji wako utasuasua sana,ni mpaka ufunguliwe. Kwa sababu kuna mambo utakuwa ukiyafanya pasipo kupenda kwa kulazimishwa na nguvu hizo. Mapepo yakiwa yanakusumbua yatakuzuia kukua kiroho,hivyo kuna kutakuwa na uzito wa kusonga mbele kiimani. Ni vyema ukaombewa ili uwe huru,ukuaji wako usiingiliwe kabisa.
03. roho ya kutangatanga kwenye makanisa/kukosa utulivu wa kiroho.
Wale wote wanaotangatanga makanisani,yaani wakihama hama kutoka kanisa hta kanisa wakitafuta upako,kawaida hawawezi kukua vyema ipasavyo. Kwa sababu ukuaji unategemea hali ya utulivu wa kiroho wa kutulia hasa kwenye eneo lililo sahihi. Ni kweli kwamba,kuhama kanisa si dhambi,lakini ukifanikiwa kupata kanisa sahihi,basi hapo tulia ujifunze ili ukue.
Lakini wapo watu ambao wanasumbuliwa na roho ya kutangatanga makanisani,wao hawatulii kabisa hata kama watafanikiwa kupata kanisa sahihi lakini hata hapo watahama tu na kwenda kanisa jingine na huko utakuta wanakaa miezi miwili au mitatu kisha wanahama tena,kwa hiyo inakuwa mchezo wa kuingia na kutoka kanisa hadi kanisa. Hali hii inasumbua ukuaji!!!!
04. Kukosekana kwa mafundisho ya awali
Inawezekana ukawa kwenye kanisa moja tu miaka na miaka,lakini ukawa umekosa darasa la mafundisho ya awali katika kukuza imani yako,hapo pia huwezi kukua vizuri katika roho yako. Unahitaji mafundisho ya kwanza ( Waebrania 5:12). Watu wengi hawajapitia madarasa ya wokovu,ili kujenga misingi yao ya wokovu,hivyo kuna mambo ya msingi hawataweza kuyajua kwa maana mambo hayo hayatahubiliwa jumapili kwenye ibada.Hivyo ni vyema ujiunge sasa na darasa la kuukulia wokovu wako hapo kanisani kwako.
05. Kukosa utii ( wa neno na kukosa utii kwa ujumla wake)
Huwezi kukua nje ya utii! Hata kama unafikiri umekua lakini kama huna utii wa kukubali kuongozwa na neno la Mungu,huwezi kukua. Neno ndio chakula cha roho yako unapolisoma ama kufundishwa ni lazima ukubali kulitii / kuliishi neno hilo ili ukue na kumfahamu sana Mungu. Hiki ni kizuizi kikubwa sana cha ukuaji,kwa maana utii wa Neno ni utii wa sauti ya Mungu.
06. Kukosa maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ( 1 Petro 2:2)
Neno ni maziwa ya ukuwaji. Na maziwa ya mama yasiyochakachuliwa ndio chakula sahihi cha ukuaji kwa mtoto. Ikiwa maziwa ya mama yakichakachuliwa/yakiongezwa ama kupunguzwa virutubisho vyake,basi ni dhahiri ukuaji wa mtoto utasua sua sana.Na ndivyo ilivyo,Neno la Bwana likichakachuliwa,haliwezi kumfanya mtoto wa Mungu kukua ipasavyo
kwa maana mtoto huyo atakuwa akipokea vitu visivyo sahihi,na hatimaye ataamini yasiyo sahihi,tena hatakuwa ipasavyo. Walimu lazima wawe makini na kile wakifundishacho,na wanafunzi wawe makini na kile wakipokeacho!
07.Kukosa wazazi wa kiroho
Ukiwa huna baba wala mama wa kiroho,huwezi kukua vizuri. Ukiokoka ni lazima uwe chini ya usimamizi wa baba au mama wa kiroho naye akuongoze vyema katika kukuza kiroho. Wao wana asilimia ndogo ya kuchangia ukuaji wako wa kiroho,unawahitaji sana. Kwa maana ni wazazi hao watakaoweza kukukemea pale inapobidi ili kusudi uende katika njia ikupasayo. Huu ni utaratibu wa Kiungu. Mfano tunaona watu walioongozwa na wazazi wao hata baadae wakajitegemea wao wenyewe kama vile;
Samweli chini ya Eli ( 1 Samweli 3:1)
Yoshua chini ya Musa ( Kutoka 24:12-18)
Elisha chini ya Eliya (2 Wafalme 2:9)
Sauli (Paulo mtume) chini ya Anania na Gamalieli ( Matendo 9:10-16,22:3)
N.k
08.Kushindwa kuwakubali wazazi wa kiroho
Ukishindwa kuwakubali wazazi wako wa kiroho utakuwa unapishana na baraka zako,na hapo utazuiliwa ukuaji wako. Wapo watu ambao hawakui ipasavyo kwa sababu wamekuwa na migongano na wazazi wao wa kiroho. Utakuta mtu hamkubali baba yake wa kiroho lakini bado yupo chini yake,kwa hiyo chochote baba yake wa kiroho akifundisha yeye hawezi kukipokea,sasa kwa mtazamo huo tu,mtu huyo atakuwaje kiroho? wengine wamewakataa baba zao/mama zao wa kiroho na kuwaona kwamba hawajui kitu zaidi yao wenyewe,kwa hiyo kule kutaa kuwapokea,kumewazuilia. Jihoji,Je ni kiasi gani unampokea baba/mama yako wa kiroho?
09. Kukaukiwa maombi / Kukosa maombi na mifungo.
Kuna nguvu katika maombi,mkristo aliyekosa mwombaji hawezi kukua kabisa,kwa maana kupitia maombi ndipo kiwango cha imani hujengwa,na udhihilisho wa nguvu za Mungu uonekana. Kukosa maombi na mifungo ya mara kwa mara kunadumaza imani ya mkristo,kiasi kwamba mkristo anakuwa ``mwepesi”kiimani.Ukihitaji kukua hakikisha unajikita kwenye maombi na kufunga,hapo utachochea nguvu za Mungu kwako,na kutakuwa na wepesi katika ukuaji wako
Matokeo mawili ya ukuaji wa kiroho
Kufunuliwa siri za ufalme wa Mungu na kuwa rafiki wa Mungu.
Roho ya kicho kuumbika n.k
Matokeo ya kudumaa kiroho
Kudanganywa na elimu ya kila namna (Waefeso 4:14)
Kukosa kutembea kwenye kusudi lako ipasavyo!
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments