KUJENGA UPYA MISINGI ~ 02
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 6, 2019
- 3 min read
Updated: Sep 2, 2022

Kwa ufupi;
Misingi ikiharibika basi ujue hata jengo huaribika, fikiria jengo ambalo msingi wake umeharibika, je jengo hilo litakuwa na uimara gani? Hata kama jengo ni zuri kwa mwonekano, lakini iwapo misingi yake ni mibovu, uzuri wa jengo hauna maana. Hujawai kuona serikali ikivunja majengo mazuri kwa sababu misingi yao ni mibovu, inahatarisha maisha ya wananchi. Ukweli ni kwamba msingi mzuri ni kipimo cha uhai wa jengo.
Misingi ya wazee wetu, imetuangusha wengi!
Wapo wazee waliojenga misingi imara na mizuri kwa familia zao, koo zao. Na kupitia misingi hiyo, wengine wamejikuta wakisimama vyema na kusonga mbele. Lakini pia wapo watu ambao wameangushwa na misingi ya wazee wao. Kundi hili ni kubwa la waliokwama au kuangushwa na misingi mibaya kwa sababu wazee wengi hawakuwa na Mungu, misingi yao ya kifamilia ilitegemea miungu na mambo yao binafsi. Baadhi ya misingi mibaya kwenye familia zilizo nyingi ni kama ifuatavyo;
01) Msingi wa matengano na chuki.
Kuna baadhi ya koo zimetengana kwa miaka mingi. Utakuta ndani ya ukoo mmoja watu hawajuani, yaani watoto wa baba mkubwa ni wa baba mkubwa na watoto wa baba mdogo ni wa baba mdogo!! Na si tu watoto kutengana kwa watoto bali karibia nusu ya watu wa ukoo hawajuani, wametengana. Ukifuatilizia tatizo hili, utagundua ni misingi mibaya ya mafarakano na matengano iliyowekwa na wazee waliotangulia. Kama wazee walikuwa hawapatani, kisha kila mmoja katika mji wake akasema kwa kizazi chake “ninaomba wanangu msiende kwa mama yenu mkubwa ni mkolofi hata siku ya kufa kwangu naomba asije kunizika... ” Sasa je, huu si msingi mbaya unaojengwa kwa watoto?
02) Misingi ya ushirikina!
Hujawahi ona mtu akiamini dawa za kiejeji kupita maelezo, na huwezi kumtoa huko anakoamini kirahisi rahisi! Kwa sababu tangu anakulia nyumbani kwao walikuwa wakitumia madawa ya kienyeji enyeji. Hujawahi kuona mtu wa namna hii? Ambaye lolote likimpata gafla hukimbilia kucheki kwa mganga! Wakati mwingine anaweza akawa anatembea na dawa za miti shamba lakini wala haumwi, basi tu! Kwa sababu ya misingi ya wazee wake waliomjengea. Sasa mbaya zaidi siku moja uzitupe dawa zake; hapo nakwambia patachimbika kwa maana imani yake yote ipo kwenye hizo dawa!!! Misingi mibaya hii ya wazee, imepofusha akili!
03) Misingi ya tabia mbaya!
Tabia kama vile uzinzi na uasherati, ni moja ya tabia mbaya inayowezwa kujengwa na wazee waliotangulia. Wao wakiwa wanaamini, kutembea na mwanamke zaidi ya mmoja ndio uanaume, na kwa wanawake huamini kuwa mambo hukaa sawa. Hivyo watoto wao wanapoendelea kukua, hujikuta wakifundishwa michezo mibaya ya mapenzi, na wanakulia humo hatimaye watoto wakiharibika!! Hujawahi kuona wazaze wakiwanunulia watoto wao kondomu/ mipira ya kiume kisha na kuwapa!!! Wakijua wanawafundisha mazuri watoto wao na kumbe wanawajengea misingi mibaya ya uzinzi na uasherati. Hata hivyo yapo mengi mabaya yaliyojengwa kwa watoto kama msingi!
Hivyo, huna budi kuivunja misingi mibovu ya namna hiyo na kuijenga upya misingi mizuri. Inawezekana kuivunja hata kama ulijengewa na watu ambao sasa hawapo. Kusema ukweli ni kwamba wengi wetu, tumejenga kwenye misingi mibaya! Ebu fikiria!jinsi Adamu alivyoharibu msingi wa Bwana, na hatimaye sote tukazaliwa kwenye msingi ulioharibika. Lakini kwa huruma za Bwana alimtuma Adamu wa mwisho Yesu Kristo aje kuweka msingi ambao hakuna awezaye kuweka kama huo, kwa kusudi la kuurekebisha ule msingi wa Mwanzo Adamu aliouharibu ( 1 Wakorintho 15:45-49, 3:11, Waefeso 2:20)
Je ni nani anayestahili kuivunja misingi mibovu?
Si kila mtu anastahili kuvunja misingi mibaya, bali ni wale tu wenye nguvu (rohoni) na wenye ufahamu juu ya mambo haya kisha walioamua kwa dhati. Suala la misingi ni pana sana na linahitaji uelewa mpana! Bila shaka, wewe ni mmojawapo unayestahili kuvunja misingi mibovu ya ukoo wako. Kumbuka hili; ili ujenge msingi mpya itakupasa ule wa zamani uvunjwe!
Unapotambua kosa fulani, ni vyema ukalishughulikia mapema, kwa maana waswahili husema “usipozibaa ufa, utajenga ukuta”. Wewe ni mmoja wa kutengeneza palipobomoka ( Ezekieli 22:30)
ITAENDELEA…
Ikiwa kama umebarikiwe, nifahamishe.
Kwa huduma ya MAOMBI piga kwa namba hizi hizi; +255 683 877 900
What’s namba +255 746 446 446
Na Mch. G.Madumla
UBARIKIWE.
Kommentare