top of page

KUJENGA UPYA MISINGI.~ 01

Updated: Sep 2, 2022


“Kama misingi ikiharibika mwenye haki atafanya nini? ” Zab. 11:3


hilo ndilo swali ambalo huna budi kujua jibu lake kwanza, kabla ya kujifunza namna ya kuijenga misingi mpya. Kwa maana hatujengi misingi mipya ikiwa misingi ya zamani ipo, isipokuwa msingi uliopo kama ni mbovu, umeaharibika basi kazi itakayohitajika ni kuukarabati. Lakini kuna wakati msingi hautaji kukarabatiwa isipokuwa kujengwa upya. Biblia inauliza swali muhimu sana. Kitu kimoja unachopaswa kujua kwanza ni kwamba; “kila kitu chini ya jua kina msingi wake”. Bishara, kazi, familia, huduma, yote ina misingi yake. Hata nchi ina misingi yake ( Mithali 3:19)


Lakini misingi hii yote inaweza kuharibika kwa kuiharibu wewe mwenyewe ikaharibiwa na mwingine. Ikiwa ndivyo, basi suala halitakuwa kuharibika, bali suala litakuwa unafanya nini baada ya kuharibika kwa misingi? Je utaiacha na kukimbia? Au je utaomba? Au Je utaimalizia kuharibika kabisa! 😭😭😭


Katika swali hili ( Zab. 11:3), misingi iliyokuwa ikizungumziwa ni misingi ya sheria na haki ya Bwana iliyoharibiwa na Sauli na uongozi wake. Daudi kama mtu wa haki, atafanya nini? Ebu fikiria ikiwa wewe umesimama kwenye nafasi ya Daudi, kisha ukagundua kwamba neno la Bwana halikufuatwa ipasavyo na mtawala wako/ kiongozi aliye juu yako! Swali ndipo linakuja, sasa wewe mwenye haki utafanya nini? ( Sio kazi rahisi kurekebisha msingi ulioharibika, hasa kuharibiwa na mwenye mamlaka zidi yako)


Kumbuka katika utawala wake Daudi kama mfamle, ulikuwa umejengwa kwenye msingi uliokuwa umeharibika kwa sehemu fulani. Na kwa sababu hiyo, Bwana akaachilia njaa ya muda wa miaka mitatu mfululizo, mwaka kwa mwaka, biblia inasema; “ Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema,


Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.” 2 Samweli 21:1. Bwana alikuwa akisema na Daudi, kwamba tatizo la njaa sio wewe, wala sio viongozi wako, bali ni kwa sababu ya yule aliyekuwapo madalakani ( Sauli) kabla yako wewe.Hivyo Bwana ni kama vile anamwambia Daudi, “ msingi umeharibika… ”


  • Njaa iliachiliwa kwa kumnyenyekeza Daudi.


“tatizo la njaa ” lilimnyenyekeza Daudi kuutafuta uso wa Bwana, kwa maana kama kusingelitokea njaa hii kali, labda Daudi asingelitafuta uso Bwana. Wakati mwingine Bwana anapohitaji kukufunulia au kusema nawe, huachilia gumu moja ili kwa ilo ushuke na uombe. Kanuni hii hutumika hata sasa. Ukiona kuna tatizo kubwa mithili la njaa ya kipundi cha Daudi, basi unapaswa kuutafuta uso wa Bwana, ukishuka na kumsihi Bwana akufunulie nini chanzo. Kabla hujachukua hatua yoyote ile, omba si kwa kuvunja na kuharibu nguvu za giza bali tafuta kujua nini chanzo? Inawezekana msingi uliopo ni mbovu, na unahitaji kujua kwanza.


  • Daudi mwenye haki, kapitishwa kwenye njaa ya miaka mitatu


Ikiwa mtu wa Mungu kama Daudi alipitishwa kwenye njaa katika utawala wake. Basi na wewe unaweza kupitishwa kwenye njaa vile vile. Inawezekana ikawa si njaa lakini kukawa na jambo mfano wa njaa. Hii yote ni kuonesha, mtu wa Mungu anaweza akapitishwa kwenye ugumu fulani bila kosa au chukizo lolote. Lakini ili uweze kuimarishwa unahitaji kupitia kwenye kila hali. Hata hivyo Bwana anakufunza kwamba anakusubili akujibu ikiwa kama kutaachiliwa gumu lolote ( Zab. 20:1-4)


  • Daudi aliutafuta uso wa Bwana, Bwana akamjibu.


Daudi kama mfalme mwenye watu chini yake, alikuwa akiweza kujitahidi kimwili / kifikra kuzuia njaa. Labda angeweza kuunda timu kubwa ya kuchunguza tatizo la njaa, angeliweza kuandaa fedha za kuthibiti njaa n. k Lakini biblia haituambii kama alifanya hivyo, ila kile tunachokisoma ni kwamba Daudi aliutafuta uso wa Bwana.


Daudi anatoa somo kubwa, kwako pale unapopitishwa kwenye shida ambayo labda ungeweza kujipangia mikakati yako. Lakini ebu ona kile alichokifanya Daudi, aliomba kwanza. Ukiona kama mtu anaweza kuomba kwanza dhidi ya tatizo, basi ujue mtu huyo anajua nini alifanyalo, anajua nini atakachopata kutoka kwa Bwana Mungu, ana hofu na Mungu.


Daudi alipomwendea Mungu, Mungu alimjibu kuonesha “kujibu” ni kawaida ya Mungu ( Zab. 118:5). Unapoomba ujue ya kwamba Bwana Mungu atakujibu lakini atakujibu kwa wakati wake. Misingi iliyokuwepo kabla ya Daudi haikuwa sawa, ilimlazimu Daudi kuishughulikia kwa kumwuuliza Mungu. Na huo ni mfano mmoja tu,


unaotuonesha jinsi ambavyo mtu wa haki anapaswa kushughulikia misingi iliyoharibika. Tunaposema “ mtu wa haki,” tuna maana mtu yeyote aliyeokoka ni “mwenye haki”. Hivyo, swali hili linamuhusu mtu wa namna hiyo….


ITAENDELEA… 


 Ikiwa kama umebarikiwe, nifahamishe.


Kwa huduma ya MAOMBI piga kwa namba hizi ; +255 683 877 900


What’s namba .+255 746 446 446


Na Mch. G.Madumla 


UBARIKIWE.  

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page